Na Salma Said, Zanzibar
KAMATI ya kukusanya maoni ya Uharakishaji wa Kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki imekatisha muda wake visiwani Zanzibar, kwa madai kuwa muda waliopanga hautoshi na wananchi wameonekana hawaelewi kinachotakiwa kufanyika
Kutokana na sababu hizo zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Samwel Wangwe, kamati hiyo imetumai siku mbili tu badala ya siku tano zilizokuwa zimepangwa.
Alisema kamati hiyo haikutarajia kukuta uelewa wa wananchi katika visiwa hivyo kuhusiana na Shirikisho la Afrika Mashariki kuwa chini namna hiyo, hivyo aliwataka waendelea kujifunza na kupata ufahamu zaidi ili kamati hiyo itakaporudia baadaye waweze kuchangia vizuri zaidi.
Profesa Wangwe alisema shughuli za ukusanyaji wa maoni Zanzibar zilisitishwa kuanzia jana.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo alisema kamati yake itazidi kutoa elimu ya kuwahamasisha wananchi mbalimbali kutumia fursa hiyo kutoa maoni na alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kujiandaa kutoa maoni hapo baadaye kamati hiyo itakaporudi tena visiwani katika kipindi cha mwezi Aprili na Mei.
Kamati hiyo imetoa uamuzi huo, ikiwa tayari imekusanya maoni ya baadhi ya wananchi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliotoa maoni kwa kamati hiyo na kuonyesha wasiwasi wa Zanzibar kumezwa katika Shirikisho hilo.
Wengi wao, bila kujali itikadi zao za kisiasa, waliungana kupinga shirikisho hilo na kushauri kwamba kama ni lazima Tanzania kujiunga basi ni vyema Zanzibar ikajiunga kama Taifa linalojitemegea.
Miongoni mwa watu wazito waliolizungumzia shirikishi hilo, ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, ambaye alisema Zanzibar bado inakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo lile la mgogoro wa kisiasa na kero za muungano hivyo ni vyema mambo hayo yakatafutiwa ufumbuzi kwanza kabla ya kujiunga na shirikisho la Afrika Mashariki.
Kificho aliyasema hayo jana wakati wa kutoa maoni juu ya kuanzishwa kwa shirikisho la Afrika Mashariki katika ukumbi wa baraza la wawakilishi jana mjini hapa.
Alisema ni jambo zuri kujiunga na shirikisho, lakini ni mapema na kwa Zanzibar inayokabiliwa na mambo mengi hivi sasa.
Alisema kutokana na michango ya wajumbe wengi waliochangia inaonesha dhahiri kwamba hawakatai shirikisho moja kwa moja lakini walichoogopa ni wakati huu, kwa vile ni mapema mno nchi kama Tanzania kujiunga na umoja huo.
Kamati hiyo itandelea na kukusanya maoni ya Watanzania kwa upande wa Mikoa ya Tanzania Bara. Hadi sasa ni wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam ndio waliokwisha toa maoni yao.