SHULE ya Msingi Digalama, iliyoko wilayani Mvomero, ambayo ina mwalimu mmoja anayefundisha zaidi ya wanafunzi 280, haijawahi kufaulisha mwanafunzi hata mmoja kwenda
sekondari kwa miaka 29.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa elimu kilichoitishwa na Mbunge wa Mvomero, Suleman
Saddiq, Mwenyekiti wa Kijiji cha Digalama, Ibrahimu Mussa, alisema shule hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yake tangu ilipoanzishwa 1976, ilifaulisha wanafunzi wanne mwaka jana.
Mwenyekiti huyo alisema hali hiyo inasababishwa na uhaba wa walimu na mazingira mabovu ya kufundishia na kujifunzia, ambapo katika miaka hiyo, idadi ya walimu imekuwa haikidhi mahitaji ya wanafunzi kutokana na walimu wanaopangwa kwenye shule hiyo kugoma kwenda.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo aliilaumu Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kushindwa kutatua tatizo hilo, hasa la walimu kugoma kwenda kufundisha katika shule hiyo kwa kutoa sababu zisizokuwa za msingi, ili wapelekwe shule nyingine.
“Walimu wengi wanaopangiwa kufundisha katika shule hiyo wamekuwa wakija kuripoti na kisha kuondoka kimoja na halmshauri wamekuwa hawachukui hatua yoyote dhidi ya walimu wa aina hii,” alisema mwenyekiti huyo.
Alisema mwalimu pekee aliyepo katika shule hiyo amekuwa akifanya kazi ya ziada kufundisha wanafunzi wote kuanzia darasa la kwanza hadi la saba kila siku, hivyo kumfanya achoke sana. Hata hivyo tunashukuru, mwaka jana jitihada zake zilizaa matunda baada ya kufaulisha watoto wanne.
Kutokana na mazingira magumu ya kujifunzia na watoto kutofaulu, baadhi ya wazazi, hukataa kuchangia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Diongoya inayojengwa kwa nguvu za wananchi.
Alisema wananchi wengi wa kijiji hicho wamegoma kuchangia ujenzi wa sekondari, hiyo kwa madai kuwa hawaoni faida wanayoipata, kwa kuwa watoto wao hawawezi kusoma hapo kutokana na kutofaulu.