Na Nora Damian
UPELELEZI wa kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ditopile Mzuzuri umekamilika na jalada lake limepelekwa kwa
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Mwendesha Mashitaka, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyella, aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upande huo wa mashtaka umeshakamilisha upelelezi wake na kwamba hatma ya kesi hiyo sasa ipo mikononi mwa DPP.
Alisema jalada halisi la polisi kuhusiana na upelelezi huo limepelekwa kwa DPP ili kutolewa maelekezo zaidi.
“Tunayo heshima kuifahamisha mahakama yako tukufu kwamba upelelezi wa shauri hili katika ngazi ya polisi umekamilika, hata hivyo kwa kuwa bado tunasubiri maelekezo ya DPP tunaomba shauri hili liendelee kutajwa” alisema Kenyella.
Nao upande wa utetezi ambao jana ulikuwa unaongozwa na wakili Cuthbert Tenga, ulieleza kufurahishwa na hatua iliyofikiwa na upande wa mashitaka na ukautaka upande huo uhakikishe jalada hilo halikai kwa muda mrefu kwa DPP.
Kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya mwisho kabla ya kuendelea tena jana, upande wa mashitaka uliieleza mahakama kuwa jalada hilo lilikuwa kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kabla ya hapo lilikuwa kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Ditopile alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 6, chini ya ulinzi mkali wa polisi akikabiliwa na shitaka la mauaji ya dereva wa daladala Hassan Mbonde.
Inadaiwa kuwa alifanya mauaji ya dereva huyo wa daladala Novemba 4, saa 1:00 usiku katika eneo la njia panda ya Bagamoyo na Kawe wilayani Kinondoni.
Kabla ya Ditopile kupandishwa kizimbani jana, watu wanaodaiwa kuwa nduguze, walisababisha mtafaruku mkubwa katika Mahakama ya Kisutu baada ya kufanya fujo na kuwatukana waandishi wa habari kwa madai kuwa wanafuatilia sana kesi hiyo.
Watu hao walianza vurumai hizo majira ya saa 4:26 asubuhi wakati Ditopile alipofikishwa mahakamani hapo. Wakati mtuhumiwa huyo akiingia mahakamani baadhi ya ndugu hao walianza vioja vyao kwa kumvamia na kumfunika kwa kanga ili kuwazuia wapiga picha wasimpige picha.
Ndugu hao wakiongozwa na mwanamke na mwanaume walimfunika Ditopile kwa kanga hadi ndani ya chumba cha mahakama.
Huku wengine wakiwa wameshika kanga hizo ndugu wengine waliokuwa wamekaa kwenye viti walianza kutoa lugha chafu na za kejeli kwa waandishi wa habari huku wakitoa matusi mazito dhidi ya waandishi hao waliokuwa kazini.
“Nyie washenzi kweli, kila siku Ditopile kwani hamna kesi nyingine...tena mwende mkaandike 'ndugu wa Ditopile wafanya fujo mahakamani',” alisikika mmoja wa ndugu hao (mwanamke) akisema na kutaja matusi mazito yasiyoandikika gazetini.
Vurugu za ndugu hao wa Ditopile zilizowashirikisha watu wanane wakiwemo wanaume sita na wanawake wawili, zilisababisha mtafaruku mkubwa mahakamani hapo kwa muda wa takribani robo saa kabla ya kuanza kwa mahakama.
Majira ya saa 4:49 asubuhi wakati Ditopile akiwa amekaa katika dawati ndani ya chumba cha mahakama kusubiri kesi yake ianze, ghafla mama mmoja aliyedai kuwa ni dada yake aliinuka na kanga na kwenda kumfunika huku mtuhumiwa huyo akiwa ameinamisha kichwa chini.
Dakika chache baadaye ndugu mwingine aliyekuwa amejitanda mtandio mweusi naye aliutoa mtandao wake na kwenda kuungana na mama huyo na kumfunika ili kukwepa asipigwe picha na waandishi wa habari. Hata hivyo baadaye kidogo walimfunua na kuanza kumpepea.
Dakika tano baadaye Ditopile alipanda kizimbani, mbele ya Hakimu Michael Luguru na hapo ndipo mahakama ilipotulia.
mwisho