WILAYA ya Korogwe iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya utungaji wa sheria ndogo itakayowabana watu wanaokwepa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa, alieleza hayo mwishoni mwa wiki alipofungua kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Alisema hatua hiyo inalenga kuwabana watu ambao wamekuwa hawataki kushiriki katika uchangiaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa sababu ya kukosekana kwa sheria inayowabana.
Betty alisema endapo sheria hiyo itakamilika na kupata baraka za vikao husika na uongozi wa juu itasaidia kuwabana wazembe na watu wasiotaka kutoa michango ikiwemo ile ya ujenzi wa shule za sekondari na msingi.
Alisema lengo ni kutaka kuwapo utaratibu endelevu wa kuwafanya wakazi wa Korogwe waone kuwa suala ya kuchangia shughuli za maendeleo ni jukumu lao.
Katika hatua nyingine, uongozi wa wilaya hiyo umeamua kufufua Mfuko wa Elimu wa Wilaya ya Korogwe kama hatua muhimu katika kuchochea maendeleo ya ujenzi wa shule za sekondari na uboreshaji wa elimu katika wilaya hiyo.
Mkwasa alisema hatua hiyo inalenga pia kuondoa upungufu katika usimamiaji na kukusanya fedha za ujenzi wa madarasa.