Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wanafunzi vyuo vikuu wamgeuka Kikwete
Wanafunzi vyuo vikuu wamgeuka Kikwete
By Habari Tanzania | Published  01/29/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Waandishi Wetu

WANAFUNZI wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam jana walifanya maandamano ya amani, kupinga kuchangia asilimia 40 katika gharama za masomo yao huku serikali ikiwakopesha asilimia 60.

Katika maandamano hayo yaliyoanzia Mlimani na kushia katika viwanja vya Jangwani ambapo walifanya mkutano wa hadhara, wanafunzi hao walisema kuwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla, wanashirikiana kuinyonga elimu ya juu.

Wanafunzi walioandamana ni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo kikuu cha Ardhi na Usanifu Majengo (UCLAS), Chuo Kikuu cha Elimu Dar esSalaam (DUCE), Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUCHS) na Chuo kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Wanafunzi hao walibeba mabango mbalimbali yenye ujumbe tofauti, huku wakiimba nyimbo kuwa Rais Kikwete na Profesa Msolla wamewasaliti na wanainyonga elimu ya juu, kutokana na msimamo wa serikali kwamba wanapaswa kuchangia asilimia 40.

Kupitia mabango na nyimbo hizo, wanafunzi hao walisema kutokana na msimamo wa kutakiwa kulipa asilimia 40, hata Mwalimu Julius Nyerere angefufuka, angewachapa viboko viongozi hao kwa sababu walisomeshwa bure.

Kupitia mabango, wanafunzi hao walisema kama serikali haina fedha, iuze ndege ya Rais na rada ili waweze kulipiwa ada kwa asilimia 100 na kwamba isiwafanyie hivyo kwa sababu vingozi hao walioko madarakani walisoma kwa kodi za wananchi bila kulipia gharama zozote.

Walisema pia endapo Rais Kikwete, Dk Asha Rose Migiro na viongozi wengine wangetakiwa kujilipia ada wakati huo, leo wasingekuwa katika nyadhifa walizonazo kitaifa na kimataifa.

Pamoja na nyimbo hizo zilizokuwa zikishutumu serikali kuua Elimu ya Juu, wanafunzi hao waliimba nyimbo za kumsifu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa juhudi zake za kutoa elimu bure kwa watanzania wote.

Wakihutubia mkutano huo, viongozi wa vyuo hivyo kwa nyakati tofauti, waliitaka serikali kuwalipia mkopo kwa asilimia 100, kwa sababu hawana uwezo wa kuchangia asilimia 40.

Rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Magesa Mwita, alizitaja sababu zilizosababisha wao kuandamana kwamba karibu wote wanatoka katika familia maskini, ambazo haziwezi kumudu gharama hizo.

"Sisi wanafunzi si watoto wa raia wa kigeni, ni watoto wa wakulima na wafugaji wadogo. Tufikirie mara mbili. Je, suala la kulipia asilimia 40 linawezekana? Jibu ni hapana," alisema Mwita.

Mwita alisema suala lingine, serikali inapaswa kutoa mikopo kwa wanafunzi waliopata daraja la tatu kwa sababu walisoma katika mazingira magumu tofauti na wengine walisoma katika shule bora.

Alisema uamuzi wa serikali kuchukua wanafunzi wa daraja la kwanza na la pili, unapingana na taratibu za vyuo vikuu kwamba mwanafunzi anayepata daraja la tatu nao wanapaswa kupewa mkopo kwa kuwa wanasifa ya kupiwa mkopo.

Alisema serikali pia irudishe huduma za afya na isiiachie Bodi ya Mikopo pekee, kwa kuwa fedha zinazotolewa hazikidhi mahitaji yao kwani hali hiyo inasababisha idadi ya vifo kuongezeka kwa kukosa fedha za matibabu.

Akizungumzia mpango wa serikali wa kutoa kipaumbele kwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma kozi za ualimu, uhandisi na madaktari, Mwita alisema serikali inafanya dhambi kubwa kwa kuwabagua wanaosoma kozi nyingine, kwa sababu nazo zina umuhimu kama kozi nyingine.

Kwa upande wake, Waziri wa Walemavu wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO), Amon Mpanju, alisema sheria ya mkopo ya mwaka 2004 haiwajali walemavu, kwani inawataka walipe asilimia 60 ya vifaa na asilimia 40 walipe wenyewe wakati wanatumia Sh6 milioni kwa kununulia vifaa.

Nao marais, Elias Hassan wa DUCE, Magesa Paulo (MUCHS) na Ndatwa Ndelabuzwa wa UCLAS, waliwataka wanafunzi hao kuendelea na msimamo wa kuishinikiza serikali iwalipie ada kwa asilimia 100, kwa kuwa hawaridhiki kulipa asilimia 40 na hawana uwezo wa kulipia kiasi hicho.

Wakitoa msimamo wao kwa nyakati tofauti, Rais wa DARUSO, alisema watatoa taarifa ya maandishi wiki hii kuhusiana hatua zitakazochukuliwa na Rais wa DUCE, alisema endapo serikali haitabadilisha msimamo wake, basi wao watasitisha kuingia darasani hadi serikali itakapowalipia ada kwa asilimia 100.

Wakati huo; serikali imesisitiza msimamo wake wa kuwataka wanafunzi wa Elimu ya Juu kuchangia gharama za masomo yao kwa asilimia 40 na kamwe haitabadili msimamo huo.

Profesa Msolla, alisema jana kuwa wanafunzi hao wanapaswa kuchangia sehemu ya gharama za masomo yao, ili kutoa nafasi kwa watanzania wengi wenye sifa kunufaika na ufadhili wa serikali.

"Uchangiaji wa gharama za masomo ni utekelezwaji wa sera ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999 na msimamo wa serikali ni ule ule, kwamba uchangiaji wa elimu hiyo utaendelea, ili kutoa nafasi kwa watanzania wengi kujinga na elimu ya juu," alisema Waziri Msolla.

Alisema kiasi cha Sh63.5 bilioni kilichoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya kuwafadhili wanafunzi kwa mwaka wa fedha wa 2006/7, hakitoshi kugharamia masomo ya wanafunzi hao kwa asilimia 100 na kwamba njia pekee ya kikidhi mahitaji hayo ni kwa wanafunzi hao kuendelea kuchangia.

Hata hivyo, alisema serikali bado inajitahidi kuongeza bajeti ya Wizara hiyo kwa asilimia 75.3 ambayo itasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi watakaofadhiliwa masomo yao na serikali.

"Fedha hiyo bado haitoshi kutokana na uongezeko la udahili wa wanafunzi walio na sifa za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, kutokana na ongezeko la mahitaji ya fedha kwa ajili ya mikopo ya chakula, malazi na ongezeko la muda wa mafunzo kwa vitendo kulingana na mitaala ya vyuo", alisema Msolla.

Alisema kutokana na uhaba wa fedha serikali imebadili utaratibu wa kuwafadhili wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kuanza kutoa ufadhili huo kwa wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza tu kwa wavulana na daraja la kwanza na pili kwa wasichana.

Msolla alisema kuwa kwa kuzingatia juhudi za Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), serikali imeamua kutoa mikopo kwa wanafunzi wote waliochukua mafunzo ya ualimu katika vyuo vikuu vya umma na binafsi.

Alisema kundi lingine litakalonufaika na mikopo hiyo ni la wanafunzi waliosajiliwa kuchukua taaluma za sayansi za kilimo, uhandisi, wanafunzi waliosajiliwa kusoma katika chuo cha usanifu wa Majengo cha (UCLAS) na wale waliokwishaingia kwenye utaratibu wa kulipiwa na serikali tangu mwaka wa masomo wa 2005.

Alisema wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakopeshwa hadi asilimia 60 katika ada ya mafunzo, mafunzo kwa vitendo na mahitaji maalumu ya vitivo na wao (wanafunzi) watatakiwa kuchangia asilimia 40 iliyobaki katika gharama zote za masomo.

Alifahamisha kuwa wanafunzi hao watakopeshwa asilimia 100 katika chakula na malazi, vitabu na viandikio na utafiti.

Profesa Msolla alisisitiza kuwa, kulingana na kifungu Na. 19 na 19A cha Sheria Na. 9 ya mwaka 2004, wanafunzi hao watatakiwa kurejesha mikopo hao kupitia kwa waajiri wao.

Alisema kwa sasa serikali imeanza kuwafuatilia na kukusanya madeni ya mikopo iliyotoa kwa wanafunzi waliomaliza masomo ya elimu ya juu mwaka 1994 na 1995.

Januari 16, mwaka huu wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, (SUA) waliandamana kutoka chuoni kwao Morogoro hadi jijini Dar es Salaam kupinga kuhusishwa na ulipaji wa asilimia hizo.

Alhamisi iliyopita wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chang'ombe walianza mgomo wa masomo, wakiwa na hoja hiyo hiyo na jana waliungana na wenzao wa vyuo vya UDSM, UCLAS, MUCHS na OUT


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.