Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mawazo Sanifu: Vijana changamkieni kilimo kuleta mapinduzi ya uchumi
Mawazo Sanifu: Vijana changamkieni kilimo kuleta mapinduzi ya uchumi
By Habari Tanzania | Published  01/28/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Profesa Leonard K. Shayo

 

KUKUA kwa uchumi wa nchi, ni sawa na kukua kwa mwili wa binadamu, ama viumbe wengine! Kama kulivyo na uwiano wa kukua kwa viungo vyote vya mwili, usio na kilema, ni lazima kuwe na uwiano katika kukua kwa sekta zote za uchumi wa nchi, isipokuwa kama sera zinazoongoza zina kilema!

Kwa maana nyingine, kukosekana kwa uwiano katika kukua kwa sekta za uchumi wa nchi, ni ushahidi wa kutumia sera potofu za uchumi. Kwa upande wa Tanzania, hakuna uwiano wa kukua kwa sekta ya kilimo na sekta nyingine, kama za biashara! Kulikoni? Je, sera zetu zimekuwa na kasoro gani?

Baada ya vita vya pili vya dunia, nchi za Ulaya ziliharibiwa vibaya sana, kiasi cha kulazimisha kuundwa kwa mpango wa “Marshal Plan” kwa ajili ya kuzijenga upya nchi hizo! Mpango huu ulijumuisha ujenzi wa viwanda, na ulifanikiwa kama inavyodhihirishwa na wingi wa viwanda vilivyopo hadi leo!

Kwa lugha nyepesi, maendeleo ya nchi za Ulaya ni matokeo ya mpango wa “Marshal Plan”! Tunashangaa ni kwa nini mipango inayofanana na ule wa “Marshal Plan” haijabuniwa na kutumika kwenye harakati za kutokomeza umaskini katika nchi kama Tanzania! Badala yake tunaletewa sera za uwekezaji, ambazo kwa hakika ni sera za uhamishaji wa rasilimali zetu!

Hali mbaya ya mashamba mengi, katika vijiji vya nchi maskini kama Tanzania, inaashiria kuwepo kwa vita vya tatu vya dunia, ambavyo viliyaharibu mashamba hayo! Vita hivi vya tatu ni vya uchumi, na vilijumuisha ujenzi wa viwanda, vya mazao ya kilimo, katika nchi tajiri peke yake, kwa kiwango kikubwa!

Vilijumuisha rushwa, kwa wasomi, viongozi na wafanyabiashara wa nchi maskini, kwa ajili ya kuwalaghai wasigundue udanganyifu wa kimataifa! Vilijumuisha ukoloni mamboleo, na mauaji ya uzalendo! Majumuisho haya, na mengine, yameufanya uharibifu uliosababishwa na vita hivi vya tatu, katika mashamba yetu, kuwa mbaya kuliko uharibifu uliosababishwa na vita vya pili huko Ulaya!

Kwa kuzingatia ukweli huu, tunahoji kwamba, njia ya kurekebisha hali ya mashamba yetu ni lazima ijumuishe kubuni mipango inayofanana na mpango wa “Marshal Plan”!

Pamoja na hila za kimataifa kuchangia katika kuzorota kwa kilimo chetu, mila na desturi zetu pia zimefanya hali kuwa ya kutisha zaidi! Tumekuwa na tabia ya kuridhika na mambo madogo-madogo, na hivyo mashamba mengi yamekuwa madogo! Yakilinganishwa na mashamba ya nchi zilizoendelea, yataitwa bustani zilizotelekezwa!

Tumekuwa na utaratibu wa kizazi kinachotoweka kugawa shamba kwa watoto wengi, na hivyo kusababisha mashamba ya kaya za leo kuwa madogo kuliko mashamba ya kaya za jana! Hii ni desturi ya kuongeza umaskini, maana kaya ya leo inakuwa maskini kuliko kaya ya jana! Tumeendekeza tabia ya kutegemea teknolojia duni, ya jembe la mkono na mvua!

Tumekuwa na tabia ya kung’ang’ania mazao tuliyorithi kwa mababu, tena bila kuotesha mimea mipya, kwa miaka mingi, kwa mazao kama kahawa na korosho! Hali hii imekuwa ikisababisha mavuno ya kila mmea kupungua, kadri mmea ulivyokuwa unazeeka!

Kwa bahati mbaya pia, tumerithi tabia ya kuogopa mabadiliko! Tabia hii iko pia kwenye maeneo mengine, kama ya siasa na uchumi! Kwa mfano, tumekuwa na minazi tangu enzi za kale, na wanasayansi wameshaainisha matumizi mengi endelevu ya minazi, lakini tumelala usingizi mnono, kama tusiokuwepo!

Je, tulihitaji mwekezaji kuja kutuonyesha kwamba, mbao za mnazi ni mali ndani na nje ya nchi? Tumekuwa tukiuza mazao ya kilimo na ufugaji bila kuyaongezea thamani, licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi na uchumi duniani! Hata pale tuliposaidiwa viwanda, kama kile cha kusindika nyama, kilichokuwa kinaitwa “Tanganyika Packers”, viwanda vya nguo na viwanda vya korosho, tulivitelekeza! Hizi ni tabia za mataifa yenye vijana waliolala usingizi!

Mabadiliko yanaanzia kwenye akili, za viongozi walioelimishwa kubadilika na kuhimiza mabadiliko kwa watu wengine! Hawa ni viongozi wanaopenda maendeleo ya watu, na wanaoweka maslahi ya umma mbele ya maslahi binafsi! Hawa ni viongozi wanaoelewa kwamba, umma ukiendelea, basi na wao wataendelea, maana wao pia ni sehemu ya umma!

Uelewa huu ni muhimu, maana unaashiria kwamba, daima kiongozi atashirikiana na wanasayansi kwa ajili ya kupata matokeo ya tafiti za kuboresha maisha ya wananchi wote! Je, kusinyaa kwa mabadiliko katika kilimo na ufugaji, licha ya matokeo kem kem ya tafiti za wanasayansi, ambayo yamebadili uchumi wa wakulima na wafugaji katika nchi zilizoendelea, kunatuambia nini kuhusu aina ya viongozi wetu walio wengi?

Kwa mfano, tulisikia sifa za kilimo cha uyoga, kama upepo unavyovuma na kupotea! Tumesikia sifa za ng’ombe wa maziwa wa kisasa, lakini bado ng’ombe wa nundu anatawala! Tatizo hapa ni ubinafsi, ufinyu wa mawazo, na falsafa potofu ya kuweka siasa mbele ya maendeleo ya umma! Tunawashauri viongozi waache ubinafsi wa kuchangamkia mimea na mifugo mipya, na waache kuhodhi masoko!

Tunawashauri viongozi wabuni mipango ya kuendeleza wilaya na mikoa, badala ya kutamba kwenye vyombo vya habari kwa hatua zao za kugawa ng’ombe wawili kwa kaya! Kama ni miradi ya kuotesha miti, basi tuoteshe kwa mamilioni! Kama ni miradi ya kuotesha zao jipya, basi uwe ni kwa wananchi wote wa wilaya ama mkoa, na uwe na michanganuo ya upatikanaji wa soko la uhakika, pamoja na uwezekano wa kujenga viwanda vya kuongeza thamani!

Watafiti wa mimea duniani, wakiwemo watanzania, wameshaainisha zaidi ya aina 510 za mimea ya madawa! Mengi ya mimea hii ipo pia hapa Tanzania, kama sehemu ya mapori na misitu ya asili! Ule mmea wa ajabu, “Aloe Vera”, uliotumika kutibu magonjwa mbali mbali miaka zaidi ya 2000 iliyopita, hadi leo, upo pia hapa Tanzania, na unatumiwa kutibu magonjwa mengi!

Je, ni kwa nini viongozi wetu hawajahamasisha vijana ili waoteshe mimea hii, kwa ajili ya kuboresha uchumi wao? Je, ni kwa nini vijana hawajawapa viongozi changamoto ya kutafuta mazao mapya, na kuwashauri ni yapi ya kuotesha, kwa kiwango gani, na kwa kutumia tekinolojia gani?

Ni kwa nini vijana hawajawahoji viongozi wao kuhusu wimbi la watafiti wa kigeni, wanaokuja kupora mitishamba yetu, na matokeo ya tafiti za wanasayansi wetu, eti kwenda kumalizia walipobakiza? Yaani wafadhili wanahakikisha kwamba, vifaa vya kumalizia tafiti za mitishamba haviletwi Tanzania, ili sehemu ya mwisho, ya kutoa dawa, ifanyike kwao! Je, ni kwa nini watafiti wetu wawekwe rehani kiasi hiki, badala ya serikali kuwapatia vifaa vyote vya utafiti? Changamoto za aina hii zitawafanya wababaishaji wasitafute nafasi za uongozi!

Maendeleo ya uhakika hayawezi kupatikana kama tutaendelea na tabia ya kupingana na kanuni za sayansi! Kwa mfano, ni kitendawili kwa serikali kuruhusu mtu yeyote kutangaza kwamba, ana dawa ya kutibu ugonjwa ambao serikali imeshatangaza kwamba hautibiki!

Kanuni za kisayansi zinataka matangazo ya aina hii yafanywe na jopo la wataalam, baada ya majaribio kwenye maabara! Kanuni za kisayansi zinakataza siri katika uvumbuzi! Ndiyo maana kuna majarida mengi ya kuchapisha matokeo ya tafiti, ili ziendelezwe na watafiti wengine kwa faida ya binadamu wote!

Pengine wakati umefika wa kupiga marufuku ubinafsi wa kuficha dawa za mitishamba, na uholela wa kutangaza tiba! Je, ni vipi tunaruhusu watu watangaze kwamba wanatibu hata ukimwi, bila kuwataka wadhihirishe uwezo wao?

Kwa kuwa dunia iko kwenye mchakato wa kutafuta dawa ya ukimwi, na kwa kuwa mgunduzi wa dawa hiyo ataifanya nchi yake iwe tajiri, ni dhahiri kwamba, ukimya wa wanasayansi, na serikali, kunaashiria kuyapuuza matangazo ya tiba hizo!

Kwa maana nyingine, serikali inaruhusu uhuni katika afya za wananchi kwa kuruhusu matangazo hayo! Ushauri nasaha ni kupiga marufuku tiba zinazofanywa na watu wasiri wa tekinolojia zao! Watu wote wanaotoa tiba watakiwe kisheria kutoa dawa zao kwa uchunguzi katika maabara za vyuo vikuu, na sehemu nyingine, ili tulinde afya za jamii!

Kwa mfano, mtu mhuni anaweza kuchanganya dawa za kisasa za malaria na mitishamba, halafu akatangaza kwamba anatibu malaria! Ukweli ni kwamba, mtumiaji wa dawa hiyo anaweza kupona, hata kama amepewa dawa nyingi kuliko inavyotakiwa! Uhuni wa aina hii ni hatari kwa afya za jamii!

Ni uhuni pia kuhodhi taarifa muhimu, kwa maendeleo ya jamii! Kwa mfano, tumesikia kuwepo kwa mti unaotoa mbegu zenye mafuta yanayowaka kama diesel! Mti huu unaitwa “jatropha” na umewahi kutumika katika nchi za kiafrika kuwasha taa na kutoa moto wa kupikia! Isitoshe, magamba yake yanatumika kutoa sabuni!

Uko pia hapa Tanzania, na unaota hata katika mazingira ya ukame! Cha kushangaza ni kwamba, licha ya matumizi wa mti huu barani Afrika, kwa muda mrefu, tafiti za kubaini uwezekano wa kuutumia badala ya diesel, ama kwa kuchanganya mafuta yake na diesel, zimefanywa nje ya Afrika! Ni vema kama watafiti wetu wangechangamkia tenda hii, ili watushauri kama ni muafaka kwa wananchi kuulima kitaalam na kwa wingi! Yapo pia mazao mengine yanayohitaji utafiti kwa lengo la kutoa ushauri nasaha kwa wakulima!

Kwa kuhitimisha, tunanena kwamba, ni kitendawili kwa wananchi wetu kuwa maskini, wakati tuna eneo kubwa la ardhi isiyotumika, na wakati kuna matokeo mengi, ya tafiti za kisayansi, yanayoweza kutumiwa na wataalam kuwapa wakulima ushauri nasaha! Kwa bahati mbaya, tumekimbilia madini yaliyo chini ya ardhi, kabla hatujawekeza juu ya ardhi!

Tunajitetea kwamba, kuwakaribisha wageni, kuja kuchota madini hayo, hakungeepukika kutokana na uwezo wetu wa kuchimba madini kuwa mdogo! Tulichosahau ni kwamba, uwezo wa kuchimba madini chini ya ardhi unapatikana tu baada ya kuwekeza vya kutosha juu ya ardhi! Yaani uwekezaji juu ya ardhi, ukijumuisha ndani ya akili pia, unatoa uwezo wa kuwekeza chini ya ardhi, na hatimaye uwezo wa kuwekeza angani!

Tunatoa wito kwa viongozi wetu kuhimiza wataalam wawageukie wakulima, badala ya kuranda mijini wakitafuta njia za panya za kupata utajiri wa haraka, lakini haram! Wakulima wanahitaji mwongozo wa kufanikisha mapinduzi katika uchumi wao, ikiwa ni pamoja na ushauri wa kuotesha mazao mapya, kutafuta soko, na kujenga viwanda! Tunashauri kuwe na kima cha chini cha eneo la shamba kwa kaya, kama tunavyohimiza kima cha chini cha mishahara!

Profesa Shayo
Mtaalam wa Hisabati na Program za Komputa
Mobile Phone: 0754 288 179


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.