Na Mwandishi Wetu
MABADILIKO makubwa bado yanakikabili Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kukipa dira tofauti na kumaliza makundi yaliyomo ndani yake. Chama hiki kinatimiza miaka 30 mwezi ujao na kitakuwa na Uchaguzi Mkuu wake mwaka huu.
CCM inafanya uchaguzi wake mkuu mwaka huu na uchaguzi huo unatarajiwa kutawaliwa na makundi, hasa yale yaliyoibuka wakati wa mchakato wa kumsaka mgombea urais kupitia chama hicho, ambapo kundi la wanamtandao liliibuka kidedea.
Wanamtandao wanaonekana kunufaika na nafasi za madaraka na wale ambao wako nje ya kundi hilo, wanaishi kwa matumaini, hali inayowafanya nao kuanza mikakati ya kupigania nafasi za uongozi katika chama hicho hasa uchaguzi unaokuja.
Ni wazi kuwa, uchaguzi ujao utakuwa vita kati ya CCM wanamtandao, na wale wa makundi mengine ambayo yanaona yamejeruhiwa na wanapigania kurejea ili yaweze kupata nafasi ya kuwa na maamuzi katika chama.
Hadi sasa CCM haijafanikiwa kubainisha vyanzo vyake vya mapato na matumizi licha ya kuwa mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete alishaonyesha nia ya kukifanya chama hiki kijitegemee.
Uswahiba wa CCM na wafanyabiashara wakubwa umeendelea kukumbatiwa, hali inayotia mashaka kama kunawezekana wakachunguzwa namna wanavyofanya biashara zao licha ya kuwa na malalamiko ya baadhi yao kuhusika na biashara chafu.
CCM ina mali nyingi ilizochukua wakati wa mfumo wa chama kimoja na kisha kujibinafsishia. Hadi sasa ni tume moja tu iliyowekwa kuchunguza matumizi ya fedha za chama hicho, jijini Mwanza. Kufa kwa Shirika la SUKITA hakujawahi kutolewa majibu achilia mbali mali nyingine za chama hicho yakiwemo magari yaliyotapakaa kila mkoa.
Upo ushahidi wa kimazingira unaoonyesha kutokuwepo dira ya CCM hii iliyopo. Watendaji wake wa sasa wanaweza pia kuwa kikwazo cha kupatikana kwa dira hiyo, kufuatia athari zinazotokana na uwezo wao binafsi, elimu na hata mazingira ya wakati.
Utanuaji wa vitengo vya CCM na kuanzishwa kwa kitengo cha Idara ya Mambo ya Nje, kunaweza pia kutoa fursa ya kutumia mwavuli wa chama hicho kufanya mambo yasiyoweza kuhojiwa hasa makusanyo ya fedha. Chama hiki kimesajili tawi lake jijini London na kina mpango wa kuwa na matawi zaidi.
Inawezekana kabisa kusiwepo tofauti kati ya CCM hii na zilizotangulia hasa zile zilizowahi kuongozwa na Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini (TAKURU), imeanza kuangaza macho yake kwa wafanyabiashara wakubwa; na hivi karibuni imemfikisha kigogo mmoja mahakamani. Harakati hizi zinaweza kugonga mwamba kufuatia wafanyabiashara ambao baadhi yao mafaili yao yako PCB, kuhusishwa na shughuli mbalimbali za kuchangia CCM kama vile viongozi wa chama hicho hawana habari ya wafanyabiashara hao kuchunguzwa.
Hadi sasa kunabakia kuwa, baadhi ya wafanyabiashara wanakitumia chama hiki kama ngao yao, jambo linalomdunisha mnyonge wa nchi hii.
Kitendo cha hivi karibuni cha Halmashauri ya CCM kupitisha kwa kauli moja kuwavua madiwani wawili na kumwondolea nafasi ya umeya, Meya wa jiji la Arusha, inaelezwa ni hatua ya kujisafisha ingawa baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa wameeleza kubeza kitendo hiki kwa kuwa kinaonekana kama adhabu kwa madiwani hao ambao hawamo katika kundi la wanamtandao.
Bado kuna kuogopana na kutoambiana ukweli. Kundi linalopata furasa sasa ni lile la wanamtandao ambao wanazidi kutawanyika kila kona. Kauli kama ile ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aliyoisema visiwani Zanzibar akiwatuhumu viongozi wenzie wa juu katika CCM kutoka visiwani humo kutompatia ushirikiano inaelezwa kuwa inatokana na kutanuka zaidi kwa makundi katika chama hiki, makundi ambayo Makamba hawezi kuyamaliza hadi anaamua kuutangazia umma.
CCM ya Kikwete imeshatangaza kukusanya taarifa za mali ya chama na pia kutoa mwongozo wa chama kupanga miradi yake ili kiweze kujiendesha tofauti na zamani. Mafanikio ya mkakati huu bado hayapo kufuatia pia wafanyakazi wa chama hicho kubakia na mishahara duni kulinganisha na taasisi nyingine licha ya pia kuwa, chama hicho kinapokea ruzuku kubwa mno kulinganisha na vyama vingine.
Inawezekana chama hiki kikawa kinatimiza miaka 30 hivi karibuni huku kikikabiliwa na tafakari mpya hasa masuala ya rushwa katika uchaguzi ambayo yamekuwa yakikikumba mara kwa mara. Uhakika uliopo bado kutakuwa na matumizi ya fedha katika kununua madaraka ya chama hicho. Waathirika wanaweza kubakia wale ambao wanatoka nje ya kundi la wanamtandao.
Ni CCM iliyopendekeza kuhalalisha rushwa ya uchaguzi na kuipa jina la takrima. Licha ya sheria hii kupingwa na kubatilishwa na mahakama, bado inakiumiza zaidi CCM kufuatia wanachama wake wengi wanaoomba madaraka kutumia fedha kufuatia chama hiki kushindwa kuwa na mfumo mzuri wa kupata wagombea wake hasa katika kura za maoni na kisha baadaye wakati wa ushindanishwaji na vyama vingine.