Na Mwandishi Wetu
WABUNGE kadhaa wamepania kuamsha mjadala wa suala la kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond Development Corporation (sasa Dowans) bungeni katika mkutano unaoanza keshokutwa, lakini kwa kutegemea zaidi kudra za Spika.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, hadi sasa kuna makundi mawili makubwa yenye maoni yanayokinzana kuhusu Richmond, moja likijielekeza kutaka suala hilo liwekwe wazi lakini jingine likitaka lifunikwe kwa staili ya kulindana.
Wabunge hao wanategemea kudra za Spika, Samuel Sitta kutokana na kushindwa kutimiza kanuni za Bunge za kuwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni ya 45 inayotaka kutolewa kwa taarifa ya hoja binafsi kimaandishi siku mbili za kazi kabla ya mkutano husika wa Bunge haujaanza.
Kwa maana hiyo, ili hoja hii ya Richmond ipokelewe na kujadiliwa, ilipaswa kutolewa taarifa ya maandishi na kuwasilishwa kwa Katibu wa Bunge walau juzi, Ijumaa.
Hata hivyo, nafasi pekee iliyoko sasa ambayo wabunge hao wanaitegemea, ni maelezo ya sehemu ya kanuni hiyo yanayompa Spika madaraka kuamua kama hoja husika ni ya dharura na hivyo kuweza kuwasilisha bila kuzingatia umuhimu wa siku mbili za kazi.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili sambamba na taarifa zilizokusanywa kwa wiki sasa, unaonyesha kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa hoja hiyo kuwasilishwa kutokana na idadi kubwa ya wabunge kutaka suala hilo liwekwe wazi, na ikiwezekana kuundwa kwa kamati ya kulichunguza.
Taarifa za ndani ambazo gazeti hili limezipata, zinaeleza kuwapo kwa mpango uliokamilika unaowajumuisha wabunge wa CCM na wale wa upinzani, ili kuibua hoja hiyo kama hoja binafsi ambayo italitaka Bunge, kutoa maamuzi ya kuundwa tume ya uchunguzi wa suala la Richmond.
Ingawa wabunge hao wanataka suala hilo liwekwe hadharani ili kubainisha kama kweli kuna wakubwa wamehusika katika mkataba ambao si tu umesababisha hasara kubwa kwa taifa, bali pia kuongeza aibu juu ya umakini wa watendaji serikalini katika kutayarisha mikataba, wapo wanaotaka kulindana na hawa wanaelezwa kuwa na nguvu zaidi.
Wabunge wenye nguvu wengine wakiwa ni mawaziri, wanaelezwa ndio waliowafanya wabunge hawa wasitumie utaratibu wa kuwasilisha hoja hiyo siku mbili za kazi kabla ya mkutano wa Bunge ujao, kwa hofu ya kupigwa dafrau.
Kutokana na hali hiyo, wabunge sasa wamepania kuishtukizia serikali, lakini kama maamuzi ya Spika yatawasaidia kwa kulichukulia suala lao kama ni la dharura kwa mujibu wa kanuni ya 45.
Msukumo mkubwa wa wabunge wanataka kuwasilishwa kwa hoja hiyo, ni ukweli kwamba kumekuwa na minong'ono mingi mitaani kwamba wakubwa serikalini wana mikono yao katika mkataba huo, wanaodhaniwa kwamba wanaweza kuua mjadala huu usifanikiwe kujadiliwa bungeni au ufikie hatima ya kuunda kamati ya uchunguzi.
Kama mjadala huu utafanikiwa, lengo la wabunge hawa ni kuona vigogo hao wanaumbuliwa kufuatia uchu wao wa mali za haraka haraka. "Suala la kwanza ni kufikisha hoja hii, hilo la namna tutakavyofanikisha kuundwa kwa kamati litafuata mbele kwa mbele," alisikika mmoja wa wabunge hao akizungumza juzi.
Uchunguzi huo umeonyesha kwamba hoja hiyo imepangwa kuwasilishwa kwa staili tofauti, lengo likiwa pengine ni kukwepa vikwazo vya urasimu wa Bunge. "Uhakika uliopo ni kuwa itawasilishwa na mbunge wa kambi ya upinzani," kilisema chanzo chetu.
Richmond iliingia mkataba na Tanesco wa kuzalisha megawati 100 za umeme kwa kutumia gesi asilia, lakini imekuwa ikikumbwa na matatizo katika utekelezaji wa mkataba huo hadi ilipouzwa kwa kampuni ya Dowans. Mradi utagharimu dola za Marekani 172,500,000 (sawa na Sh225 bilioni).
Vyanzo vya habari vinasema kwamba, timu ya serikali ilikuwa na udhaifu mkubwa katika uingiaji wa mkataba na kampuni hiyo kwani ilijihusisha tu na masuala ya kiufundi ya mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 100.
Uchunguzi wa muda mrefu baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, umethibitisha kwamba udadisi wa kina (due diligence) juu ya uwezo na nguvu za Richmond haukufanyika.
Hali hii ndiyo iliyosababisha matatizo makubwa kuibuka baada ya mkataba kusainiwa kwamba Richmond walishindwa kutimiza wajibu wao wa kuwasilisha nchini mashine za kuzalisha umeme ilipotimu Oktoba 8, mwaka huu.
Kulingana na vyanzo vya habari hata kabla ya Timu ya Serikali ya majadiliano na Richmond kumaliza mazungumzo, Richmond ilithibitisha kwamba tayari ilikuwa imekwisha kupata kampuni ya kuipatia mitambo yote kwa pamoja yenye uwezo wa kuzalisha migawati 100.
Richmond kwa kauli yao wenyewe waliweza kueleza wazi kwamba upatikanaji wa mitambo hiyo, yaani yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 ni wa asilimia 95, jambo ambalo lilikubaliwa na timu ya mashauriano bila hata mjumbe mmoja kuonyesha kuhoji uthabiti wa kauli hiyo ama kwa kupata taarifa mbadala juu ya kampuni hiyo iliyoonyesha kila kitu kikiwa rahisi kabisa.
Hata hivyo, baadaye ilikuja kuthibitika kinyume chake kwani hadi Richmond wanauza mkataba wake kwa Dowans walikuwa wameweza tu kuwasilisha nchini mashine zenye uwezo wa kuzalisha megawati 20. Kampuni ya Dowans nayo ilisema kwamba ilikuwa na uwezo wa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati, na kwamba mashine zenye uwezo wa kuzalisha megawati 66 zilikuwa tayari katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, juzi Ijumaa, Kamati ya Wabunge ya Biashara na Uwekezaji, ilipotembelea inakojengwa mitambo ya Richmond/Dowans, hawakukuta mtambo wowote na walielezwa kwamba mitambo hiyo itatolewa bandarini kesho.
Pia walielezwa kwamba katika kipindi cha siku tisa, ufungaji wa mitambo hiyo utakuwa umekamilika, hivyo kufanikiwa kutekeleza masharti ya mkataba ya kuanza kuzalisha megawati 100 ifikapo Februari 5, 2007.