KATIKA makala yangu iliyokuwa na kichwa cha habari “Dk Shein na Lowassa wameitenga Mtwara”, nilijadili na kubainisha kuwa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wanafanya ubaguzi wa wazi kwa kutofanya ziara za kikazi katika mikoa ya Mtwara na Lindi wakati wamefanya ziara nyingi katika mikoa mingine, hasa ile ya Kaskazini.
Nimeamua kurudia kuandika juu ya mada hiyo ili kujadili yalijitokeza baada ya makala yangu ya awali.
Kwanza, nimepokea simu, ujumbe mfupi wa simu na barua pepe kutoka kwa watu mbalimbali, wengi wao wakiwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara. Wote wameonyesha kutofurahishwa na ubaguzi huo unaofanywa na viongozi wa kitaifa.
Pili, siku mbili baada ya makala yangu kutoka gazetini, ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa taarifa kwa umma kuhusu ziara ambazo amekwishafanya Waziri Lowassa tangu ateuliwe kushika wadhifa huo hadi sasa.
Japo taarifa hiyo haikueleza kuwa ilikuwa inajibu makala yangu, maudhui yake yanaonyesha dhahiri kuwa ilitolewa kwa lengo hilo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, hadi sasa Waziri Mkuu amekwishatembelea mikoa 18, lakini haikufafanua ametembelea mara ngapi kila mkoa.
Ni kweli Waziri Mkuu ametembelea mikoa 18, lakini hoja hapa si idadi ya mikoa tu. Ni je, hiyo mikoa ameitembelea kwa usawa na kama si hivyo ni kwa nini?
Katika makala yangu nilieleza kuwa, wakati Makamu wa Rais na Waziri Mkuu hawajatembelea Mkoa wa Mtwara hata mara moja kwa ziara rasmi ya kikazi, wamefanya ziara nyingi katika mikoa ya kaskazini, yaani Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Hicho ndicho kitu ambacho nilitegemea taarifa hiyo ingejielekeza kufafanua.
Taarifa hiyo ingeeleza viongozi hao wametembelea mikoa ya kaskazini mara ngapi ukilinganisha na mikoa mingine na kuleza kwa nini mikoa hiyo inatembelewa mara nyingi na viongozi hao.
Leo (Januari 27), Waziri Mkuu anatembelea tena Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake, atatembelea Kituo cha utafiti wa zao la kahawa cha Lyamungo.
Lowassa aliamua kufanya hivyo baada ya kuwa na kikao cha kazi na mawaziri kujadili uendelezaji wa sekta ya kilimo nchini, kilichofanyika ofisini kwake Januari 23, mwaka huu. Huu ni ushahidi tosha wa hoja yangu. Badala ya kutembelea mikoa ambayo hajatembelea, Waziri Mkuu, ameamua kurudia mkoa anaoutembelea mara kwa mara.
Kama huu si upendeleo wa wazi ni nini? Kwa kuwa kikao kilichomfanya atembelee kituo hicho kilikuwa kinajadili sekta ya kilimo kwa ujumla na si zao la kahawa pekee, kwanini hakuamua kwenda kutembelea kituo cha utafiti wa zao jingine kama vile korosho kilichoko Naliendele, Mtwara au kituo cha utafiti wa zao la pamba kilichoko Ukiriguru, Mwanza? Sisemi kuwa asitembelee kabisa Mkoa wa Kilimanjaro, bali afanye hivyo kwa usawa. Si wananchi wa Kilimanjaro tu wanaomuhitaji. Watanzania wote wanamhitaji, wakiwamo wananchi wa Mtwara. Wakati ofisi ya Waziri Mkuu imetoa tamko juu ya ziara za Waziri Mkuu, ofisi ya Makamu wa Rais haikufanya hivyo.
Sababu inayoweza kukubalika kuwa inamfanya Makamu wa Rais asiende Mtwara ni kwamba ametingwa na majukumu mengine.
Kutokana na ubaguzi wa dhahiri unaoonyeshwa na viongozi wa kitaifa katika kufanya ziara, isipokuwa Rais Jakaya Kikwete, hata mawaziri nao wanafuata nyayo hizo hizo. Mawaziri wengi hawafanyi ziara za kikazi Mkoa wa Mtwara hadi washinikizwe au litokee tatizo fulani, wakati mikoa mingine wanafanya ziara za kawaida bila shinikizo au tatizo kutokea.
Kwa mfano, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba, mwaka jana, alilazimika kufanya ziara katika ujenzi wa barabara ya kwenda Mtwara baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Waziri Lowassa aliyekuwa ziarani mkoani Lindi, alikokutana na matatizo yaliyohitaji kushughulikiwa haraka.
Naye aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Joseph Mungai alilazimika kwenda Mtwara baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Lowassa, kushughulikia matatizo ya pembejeo za kilimo na juzi, Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wassira, naye alitembelea Mtwara. Viongozi wa serikali mtaendelea kuibagua mikoa ya kusini hadi lini? Kumbukeni kuwa hata Mtwara wanaishi watu na wana thamani sawa na watu wa mikoa mingine.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu; 0754 405 582 au barua pepe; spshimbe@yahoo.com.