WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta, jana alitangaza kuwavua madaraka walimu wakuu na baadhi ya maofisa elimu wa mikoa mine, ambayo imebainika kufanya udanganyifu katika mitihani ya darasa la saba mwaka jana.
Maofisa walioathirika wanatoka katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Shinyanga na Tabora, ambayo ilitembelewa na tume maalumu ya uchunguzi kuanzia Desemba 20, mwaka jana hadi Januari 18, mwaka huu.
Tume hiyo iliundwa na wizara hiyo kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina, ili kubaini ukweli na chanzo cha udanganyifu huo.
Waliovuliwa madaraka ni Ofisa Elimu wa Mkoa na Ofisa Elimu wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, wakati Ofisa Elimu wa Wilaya ya Dodoma Vijijini na Mpwapwa wamechukuliwa hatua za kinidhamu ambazo hazikutajwa.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro, waliovuliwa madaraka ni Ofisa Elimu Taaluma, Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu na Ofisa Elimu ya Watu Wazima katika Wilaya ya Same.
Mkoani Shinyanga, waliovuliwa madaraka ni maofisa elimu wa wilaya za Bariadi na Kahama wakati Mkoa wa Tabora maofisa wa elimu wa wilaya za Uyui, Urambo na Nzega wamechukuliwa hatua za kisheria.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ofisini kwake, Waziri Sitta, alisema baada ya tume kufanya uchunguzi wake, ilibaini udanganyifu mkubwa kutokana na taarifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na watahiniwa wapatao 120 waliokuwa na miandiko inayofanana.
Aidha, aliongeza kuwa walipotakiwa kurudia, watahiniwa wengi waliofanya maswali ya mitihani ile ile waliofanya awali, walipata alama za chini sana ukilinganisha na zile walizopata walipofanya mtihani huo Septemba 2006.
Mbali na alama, pia tume hiyo ilipata taarifa kuwa, baadhi ya maeneo wazazi walichangishwa fedha kuwahonga wasimamizi ili wawasaidie watahiniwa.
Hata hivyo, katika uchunguzi huo, baadhi ya wajumbe wa kamati za mitihani za mikoa na wilaya, walikiri kuwapo kwa udanganyifu kwa watahiniwa kutazamiana au kuwa na chanzo kimoja cha majibu ya mitihani.
Waziri Sitta, pia alisema baadhi ya watahiniwa walipohojiwa, walikiri kwamba walikuwa wakipewa majibu ya mitihani na wasimamizi wao na wengine walisema walikuwa wakisaidiana katika kujibu maswali.
Wakati huohuo, kadi za maendeleo ya wanafunzi zilionyesha uwezo mdogo wa watahiniwa ukilinganisha na matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Kwa mfano, kwa baadhi ya watahiniwa, wastani wa alama za maendeleo kuanzia darasa la V-VII ulikuwa chini ya asilimia 50 wakati katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi walipata wastani wa asilimia 80 hadi 95.
Katika baadhi ya shule zilizochunguzwa, kadi za maendeleo za wanafunzi zilikuwa ni mpya na zilikuwa zimejazwa na mtu mmoja kuanzia darasa V hadi VII.
Hata hivyo, Sitta alizitaja hatua nyingine zilizochukuliwa mbali na kuwavua madaraka walimu wakuu na maofisa elimu kuwa, ni pamoja na kuwafutia matokeo watahiniwa 820 ambao wamethibitika kuhusika na udanganyifu.
Aidha, alisema wanafunzi hao watapaswa kurudia mtihani na watakaofaulu wataweza kujiunga na elimu ya sekondari kabla ya tarehe 15 mwezi Machi ambayo ni ndani ya siku 194 za masomo.