WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vimeanza mazungumzo ya siri kwa lengo la kutafuta muafaka wa mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar, CUF imeanza kujikanganya kwa kusema kuwa haipo tayari kusaini muafaka wa tatu.
Katika kile kinachoonekana kupiga chenga ya maneno, chama hicho kikuu cha upinzani Visiwani, jana kilitangaza rasmi kwamba mazungumzo yake na CCM hayatazaa muafaka mwingine kama ilivyokuwa mwaka 1999 na 2001.
Msimamo huo wa CUF wenye utata, ambao kimsingi hauendani na mantiki ya mazungumzo, ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kwenye mkutano wa waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.
“Hatutakubali kuunda tena muafaka wa tatu safari hii, kwa vile mazungumzo yetu yaliyopita tulikubaliana masuala muhimu, ambayo nao wenzetu wamekuwa wagumu kuyatekeleza,” alisisitiza Profesa Lipumba.
Alisema mazungumzo ya vyama hivyo yanayoendelea hivi sasa kuhusu mpasuko wa kisiasa Zanzibar, hayapaswi kufanyiwa mzaha na dharau kama ilivyotokea hapo awali.
Lipumba alisema, kutokana na mwenendo mzuri unaoonyeshwa hivi sasa kwenye mazungumzo hayo, vyama vyote viwili vinaamini uamuzi utakaofikiwa utakuwa unalenga maslahi ya taifa na si manufaa ya chama kimoja.
Hata hivyo, ingawa CUF inakataa kulitumia neno muafaka, iwapo mazungumzo yake na CCM yatafanikiwa, upo uwezekano mkubwa wa kufikia kwa maafikiano ya tatu kati ya vyama hivyo, ambayo kwa maana halisi yatazaa muafaka.
Mbali ya hilo, Lipumba alisema pia kuwa, anaamini Rais Jakaya Kikwete ana nia thabiti ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko huo, ambao CUF wanaamini ukiachwa ukaendelea, utaathiri amani, utulivu na mshikamano nchini.
Alisema hatua ya Rais Kikwete kusimamia suala hili kwa nguvu zake zote, ni dalali tosha kuwa, amedhamiria kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo.
“CUF tutaendelea kutoa ushirikiano katika kutafuta haki na suluhu ya kisiasa kwa Wazanzibari wote na kwa manufaa ya Watanzania wote,” alisema.
Alisema ni matarajio ya CUF kuwa, suala hilo litasimamiwa ipasavyo hadi mwisho.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu ni nini hasa kilizungumzwa, Profesa Lipumba aliwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi na pindi mambo yatakapokamilika, wataarifiwa juu ya hatua iliyofikiwa.
“Ndugu zangu, hata wakati ule Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere anatafuta uhuru wa Tanganyika, kuna baadhi ya mambo alikuwa hatangazi, sasa na sisi CUF na CCM tumechukua mfumo huu,” alisema Profesa Lipumba.
Kwa muda mrefu, utatuzi wa tatizo la Zanzibar umekuwa ukikwazwa na maneno ya kujikanganya ya wanasiasa, ambayo kimsingi yamekuwa sababu kuu ya kukomaa kwa hali tete visiwani humo.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 1995 na 1999, CCM ilikuwa ikikanusha kabisa kuwapo kwa mgogoro wowote wa kisiasa Zanzibar hadi baada ya Jumuiya ya Madola kujitokeza na kutangaza azma yake ya kuvisuluhisha vyama hivyo viwili.
Hali kama hiyo tena, iliendelea baada ya mwaka 2000 na ikawa hivyo hadi pale Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alipotangaza kuwapo kwa hali mbaya Zanzibar na akaagiza kuanza kufanyika kwa vikao vya makatibu wakuu wa vyama hivyo viwili.