Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Dowans yashtua wabunge
Dowans yashtua wabunge
By Habari Tanzania | Published  01/27/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Irene Mark

KAMATI ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji, imeshtushwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mkataba wa megawati 100 za umeme kati ya Kampuni ya Dowans na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Hali hiyo ilitokea jana wakati kamati ilipotembelea eneo la miradi ya TANESCO, Ubungo Dar es Salaam, baada ya kutoridhishwa na hesabu za shirika hilo.

Wakihoji juu ya ufinyu wa utekelezaji wa mkataba huo, wabunge hao walitaka kufahamu kwa nini Dowans walioinunua Richmond iliyokuwa kwenye mkataba na shirika hilo, imeshindwa kutekeleza mkataba huo kwa wakati.

Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, alitaka kufahamu ni lini kampuni hiyo imeanza uzalishaji wake na kama tayari imeanza kuingiza megawati 100 za umeme kwenye Gridi ya Taifa ikiwa ni sehemu ya mkataba wao wenye kugharimu sh milioni 172.

Akijibu kwa niaba ya wakurugenzi wa Dowans, Meneja Uzalishaji wa TANESCO, Stephen Mabada, alijaribu kuwatetea wawekezaji hao kwa maelezo kwamba mashine zao zimeanza kuzalisha megawati 20 kwa majaribio tangu siku sita zilizopita.

Aliongeza kwamba, majaribio hayo yataendelea hadi wataalamu watakaporidhika na ufanisi wa mashine hizo kabla ya kuunganisha kwenye gridi ya taifa.

Katika hali ya kutoridhika na jibu hilo, mjumbe wa kamati hiyo, Siraju Kaboyonga, Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alihoji sababu za matumizi ya vinu vya kukodi vya kuzalisha umeme wakati nchi inazo mashine zake.

Mabada, alijibu swali hilo kwa maelezo kuwa, vinu vilivyopo ni vichache, vilivyo chini ya kiwango, chakavu na vyenye kuhitaji matengenezo ya gharama kubwa.

“Shirika halioni sababu ya kuvifanyia matengeneo kwa kuwa ni sawa na kuharibu fedha, hatua tuliyochukua ni kuagizia vinu vyetu… tayari utekelezaji wa mradi umeanza tangu Julai mwaka jana ambapo mashine 12 zitafungwa eneo la nyuma la ofisi za TANESCO hapa Ubungo, kila mashine itazalisha megawati 8.7.

“Tunatarajia kwamba, ndani ya kipindi cha miezi 11 utakuwa umekamilika na hapo tutaweza kukabiliana na uhaba wa mashine za uzalishaji umeme zetu wenyewe… mradi huo unagharimu Euro 57,550,000, mkandarasi wa mradi ni Kampuni ya Wartsila ya Finland,” alisema Mabada.

Aidha, Kaboyonga, alitaka kumfahamu mlipaji wa gharama za mkataba wa sh milioni 172 kati ya Kampuni ya Richmond na TANESCO, unaodaiwa kusababishwa na watendaji wachache walioamua kuingia mkataba na kampuni isiyo na uwezo.

Akijibu swali hilo, Mabada, alisema kutokana na shirika la umeme kuyumba kifedha, serikali iliamua kugharamia mkataba huo aliodai kuwa baada ya kushindwa kwa Richmond iliamua kuuza kazi hiyo kwa Dowans.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba, mkataba kati ya Richmond na TANESCO ni wa muda mfupi hivyo aliwataka wabunge hao kuondoa hofu kwa kuwa shirika linajipanga baada ya kipindi cha mkataba kwisha.

“Mkataba kati ya Richmond, Aggreko na mingine ni ya muda mfupi, hivyo hakuna haja ya kupata wasiwasi juu ya hilo… bado hawajaanza kulipwa hadi watakapoingiza umeme kwenye gridi ya taifa (hakuwa wazi ni lini wataanza kuingiza).

“Mkataba pia unaonyesha kwamba, wakianza kuzalisha umeme halafu wakashindwa kutoa huduma kwa siku moja, wanapigwa penati ya dola 10,000, ikiwa tutaweza kuzalisha umeme bila kutegemea mashine zao kabla ya miaka miwili hatutatumia wetu kwa vile waliongia kwenye mkataba wanalipwa,” alisema Mabada.

Pamoja na hayo, Dk. Mwakyembe, aliipongeza serikali kwa kuokoa jahazi wakati wa tatizo la umeme kwa kuweza kukodi mitambo ya dharura na kuliondoa taifa gizani.

Mbali na pongezi hizo kwa serikali, bado Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo alilishangaa Shirika la Umeme kwa kuwa na mitambo mibovu na chakavu aliyoifananisha na magofu yasiyo na faida.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.