Na Mwandishi Wetu, Mbeya JESHI la Polisi Mbeya limetangaza kampeni kambambe ya kukabiliana vitendo vya uhalifu ukiwamo ujambazi wa kutumia silaha kwa kufanya msako kwa kushirikiana na wenzao wa Iringa na Rukwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya kugundua mbinu mpya ya kuwanasa watu wanaojiuhusiaha na vitendo hivyo ambayo vimeonyesha kuitikisa Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Jeshi hilo, litafanya hivyo kwa kuweka doria katika mikoa hiyo, kata zote zinazoizunguka, kufanya msako wa nyumba kwa nyumba na kwenye mabasi.
Akitangaza kampeni hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Suleiman Kova alisema kuwa, msako huo umeanza mapema wiki hii ukiongozwa na makachero wa jeshi hilo.
Watakahusishwa ni watuhumiwa wa ujambazi, watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, wizi wa mafuta ya transfoma, magari na wizi wa nyaya za simu ulioibuka kwa kasi jijini Mbeya.
Msako huo pia utafanyika katika mipaka Tanzania, Malawi na Zambia ambako kumekuwa kukiripotiwa kutokea kwa matukio ya uhalifu.
"Jeshi la polisi limejiandaa kwani vitendo vya uhalifu vimeibuka kwa kasi kubwa hadi kupelekea amani na utulivu kutoweka katika jamii nzima ya jiji la mbeya na kuliweka kwenye historia mbaya ya kipekee kimkoa," alisema na kusisitiza kuwa:
" Ni lazima amani irudi kama miaka ya nyuma na kwamba si vyema kwa mkoa kutawaliwa na uharifu na ujambazi uliokithili jijini."
Aliwataka wakazi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha polisi au katika ofisi yeyote ya afisa watendaji kabla ya msako kuanza.