Na Midraji Ibrahim
KAMATI ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara imekataa kupokea ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) baada ya kushindwa kuingiza mwaka jana.
Kamati hiyo pia imesitisha kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na mahojiano yake na vigogo wa Tanesco hadi itakapofanya ukaguzi wa eneo na thamani ya uwekezaji uliofanywa na Kampuni ya Richmond Development.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Harison Mwakyembe, alisema ripoti iliyowasilishwa na Tanesco mbele ya kamati hiyo inaishia Desemba 2005 na kwamba, wanapata matatizo kuijadili wakati waliohusika hawapo.
"Hapa kuna mwaka mzima yaani 2006 hakuna ripoti yake, unatuletea ripoti ya kuishia Desemba 2005 tuilinganishe na nini? Pia, Netgroup waliohusika hawapo ni bora wakamilishe ripoti ya mwaka jana tukutane nao Novemba mwaka huu," alisema Dk Mwakyembe.
Mkutano huo uliofanyika jana kwenye ofisi za bunge Dar es Salaam, ulianza saa 3:30 asubuhi na kumalizika saa 10:00 jioni ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Balozi Fulgence Kazaura, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk Idrisa Rashid na maafisa wengine.
Dk Mwakyembe alisema walipitia gharama za uendeshaji wa shirika, uwekezaji uliofanywa, kupanda kwa bei ya umeme na umeme wa dharura uliongizwa kwenye gridi ya taifa.
Alisema walipitia vigezo ambavyo vilitumiwa na Tanesco kupandisha bei ya umeme na Novemba watafanya majadiliano ya kina ya hesabu za shirika hilo kwa sababu ni nyeti.
Taarifa kutoka ndani ya kikao, zilisema wabunge walitaka taratibu za uingiaji wa mikataba uliofanywa na shirika hilo na kudai kuwa ni kitendawili.
"Tumehoji maswali mengi ambayo yanahitaji majibu, lakini Tanesco wanaonekana kujivua lawama," kilisema chanzo chetu cha habari.
Katika masuala ambayo wabunge hao kujua ni hatua ya Kampuni ya Richmond kuuzwa kwa Dowans na iwapo walishirikishwa kwenye mkataba wa Richmond, lakini inadaiwa maafisa hao wa Tanesco walikana kuhusika na kudai kuwa walipokea amri kutoka serikalini kuingia mkataba huo.
"Wametuambia wao hawakuhusika, bali waliohusika ni kamati ya serikali ya majadiliano ambayo ilijumuisha baadhi ya makatibu wakuu wa wizara, ndio maana tumefikia uamuzi wa kwenda kuona eneo na uwekezaji uliofanywa na Richmond," kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, kulingana na vyanzo vyetu vya habari wawakilishi wa Tanesco katika mazungumzo hayo alikuwa ni Stephen Mabada; Mohamed Saleh; Godson Makia; James Mtei na Wangwe Mwita aliyekuwa kwenye sekretariati.
Vyanzo vyetu katika orodha ya maofisi wa umma walioshiriki majadiliano na Richmond yumo Singi R. Madata kutoka Wizara ya Fedha, na anaelezwa kwamba alikuwa Mwenyekiti wa Timu ya Serikali iliyongia katika majadiliano hayo.
Mwakilishi wa Wizara ya Nishati na Madini ni Theophillo Bwakea pamoja na Julius Sarota anayeelezwa kwamba alikuwa kwenye sekretariati.
Kampuni ya Lahmeter International iliwakilishwa na Klaus-Uwe Huhnke na Wolfgang Pauly; Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwakilishwa na Donald L. Chidowu na CTI iliwakilishwa na Gideon Nasari.
Kwa upande wa RDC vyanzo vyetu vinasema kwamba kulikuwa na Mohamed Gire na Naeem Gire; Gary Borges na Cuthbert Tenga.
Taarifa ya mipango ya baadaye inaonyesha, Tanesco inajenga kituo cha kuzalisha megawati 100 eneo la Ubungo na kingine cha megawati 45 eneo la Tegeta, vinavyojengwa na Kampuni ya Wartsila kutoka Finland.
Katika kujitetea kwa kupandisha bei ya umeme, Tanesco ilisema haina uwezo wa kutekeleza wajibu wake wa kulipa madeni kutokana na bei ya umeme kutoshabihiana na gharama za uendeshaji.