KATIKA hatua ya kupambana na utovu wa nidhamu na ukiukwaji wa maadili, Idara ya Mahakama imetangaza kumfukuza kazi hakimu mkazi mmoja na kumstaafisha kwa manufaa ya umma hakimu wa wilaya.
Aliyefukuzwa kazi ametambuliwa kuwa ni aliyekuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa Arusha, Seleman Komba na aliyestaafishwa alitajwa kuwa ni hakimu wa wilaya daraja la pili, Victoria Elizabeth Saduka.
Taarifa iliyoyolewa jana na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Sophia Wambura, ilisema kuwa katika kikao chake cha Oktoba 11 na 12 mwaka jana, Tume ya Utumishi wa Mahakama, ilifikia uamuzi wa kumsimamisha kazi Komba kutokana na ukiukaji wa maadili.
Taarifa ilisema kuwa tume hiyo ilimfukuza kazi Komba baada ya kujiridhisha kuwa hakimu huyo alitoa hukumu mbili kwa kesi moja.
Kwa mujibu wa taarifa nyingine ya Mahakama ya Rufani iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Sam Rumanyika, Hakimu Victoria Elizabeth Saduka, ambaye ni Hakimu wa Wilaya Daraja la II, amestaafishwa kazi kwa manufaa ya umma tangu Desemba 6 mwaka jana.
Tume ya Utumushi wa Mahakama ilifikia uamuzi huo katika mkutano wake namba 2006.3, uliofanyika Desemba 6 na 7 mwaka jana.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Sadula alistaafishwa kuanzia Desemba 6 mwaka jana baada ya kubainika kuwa alikiuka maadili ya kazi yake.
Ilithibitika mbele ya tume kuwa hakimu huyo alivichukua kwa nguvu vifaa vya nyumbani kutoka chumbani kwa mtumishi wake, Serafini Kassian.
Taarifa hiyo ilivitaja vifaa hivyo kuwa ni kitanda, pasi ya umeme na meza ya kulia chakula, ambavyo vilikuwa mali ya Kassian.
Pia hakimu huyo kwa makusudi anadaiwa kuwarubuni askari wa Jeshi la Polisi kumfungulia Kassian kesi mbili za jinai ambazo ni za uzushi, vitendo ambavyo vimeidhalilisha Mahakama ya Tanzania pia kumdhalilisha hakimu huyo.