KAMISHNA wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, amelazimika kukatisha likizo na kujisalimisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyokuwa inamtafuta ili kutoa ushahidi wa utetezi katika kesi ya wizi inayowakabili wafanyabiashara watatu.
Kabla ya kutoa ushahidi huo, Tibaigana, aliwaambia askari polisi waliokuwa mahakamani hapo kuwa ilimbidi akatishe likizo yake mkoani Kagera, baada ya kusoma kwenye magazeti kwamba alitakiwa kukamatwa ili kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Akiwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Neema Chusy, mahojiano kati ya wakili wa utetezi Julius Msafiri na Kamishna huyo yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Shahidi ni mshitakiwa yupi unayemfahamu kati ya watatu waliopo mahakamani hapa?
Tibaigana: Namfahamu Stanley Damgoba, ni mshitakiwa wa pili.
Wakili: Unamfahamu kivipi?
Tibaigana: Huwa namuona pale ofisini kwangu…anafika mara kwa mara.
Wakili: Unakumbuka nini kati ya Mei na Juni 2005? Ulikutana na nani kipindi hicho.
Tibaigana: Siwezi kukumbuka kwa vile nakutana na watu wengi.
Wakili: Unaelezea nini kuhusu ushahidi wako hapa mahakamani.
Tibaigana: Sina cha kueleza…kama nilivyosema awali nilisoma kwenye magazeti kwamba hakimu ananiita mahakamani, kesho yake nikamuona anakuja Damgoba, akaniambia kuwa naitwa hapa mahakamani kutoa ushahidi.
“Nikamuuliza nikatoe ushahidi gani? Damgoba akaniambia kuwa wakili wake ataniuliza, haya wakili hebu niulize wewe.
Wakili: Kabla ya hapo Damgoba alikuja kwako kukulalamikia kuwa hakutendewa haki kutoka katika Kituo cha Polisi Oysterbay. Je, suala kama hilo mtuhumiwa aliwahi kulileta kwako?
Tibaigana: Inawezekana, kwa kuwa kuna watu wengi wanapokuwa wanaonewa katika vituo vya Polisi huwa wanakuja ofisini kwangu kutoa malalamiko.
Mara baada ya Tibaigana kutoa majibu hayo wakili alimwambia “ahsante”, akashuka kizimbani na kuondoka.
Inadaiwa na Inspekta Msaidizi wa Polisi Maximilian Birigi, kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la wizi wa vifaa mbalimbali.
Birigi, aliwataja watuhumiwa hao kuwa, ni Michael Daniel (25), mkazi wa Mbezi Beach, Stanley Damgoba (54), mkazi wa Kinondoni na Cornel Ernest (37) mkazi wa Kunduchi.
Mei 5, 2005 watuhumiwa wanadaiwa kuiba luninga mbili aina ya Sony, dvd mbili aina ya Sony, deck mbili aina ya Sony, video deck mbili aina ya Sony, video kamera, digital kamera, simu za mezani tatu, luninga aina ya Hitachi na music system mali ya Dk. Hamza Muhula.