ASKARI Magereza sita wamekamatwa na kufikishwa mahakamani, wakihusishwa na kumpiga mfungwa hadi kumuua jijini Dar es Salaam .
Mfungwa aliyeuawa kwa kipigo ni Eradius Stanslaus, aliyekuwa akitumikia kifungo kwenye Gereza la Kilimo la Kimbiji, lililopo Kigamboni.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kapteni John Chiligati, alisema katika taarifa yake kwamba, hatua za kuwakamata na kuwashtaki askari hao, zimekuja baada ya tume iliyoundwa kuchunguza chanzo cha kifo cha mfungwa huyo, kubaini kilitokana na kipigo.
Askari waliokamatwa na ambao sasa wanasubiri hatma yao mahakamani, ni Sajenti David mwenye namba A. 9442, Koplo Michael (A. 7126), Koplo Rafii (A. 7680), Koplo Abdul (B. 2241), Wdr Heri (B. 2423) na Wdr Avith mwenye namba B. 3269.
Ilivyokuwa ni kwamba, alieleza Kapteni Chiligati, hayati Eradius na mfungwa mwenzake mwenye namba A 422/2006 Gome Christopher, walitoroka gerezani mwendo wa saa 5 asubuhi Juni 5 mwaka huu, na juhudi za kuwatafuta ziliendelea hadi saa 11 alfajiri ya kesho yake maeneo ya Feri, Kigamboni.
"Baada ya kukamatwa walirejeshwa gerezani mnamo saa sita mchana, na ilipofika saa 2 usiku, Eradius Stanslaus alikutwa amekufa katika moja ya mabweni ya wafungwa lililokuwa halitumiki.
"Baada ya tukio hilo , Kamishna Mkuu wa Magereza aliunda kamati ya kuchunguza chanzo cha kifo cha mfungwa huyo. Uchunguzi umeonyesha kwamba mfungwa huyu na mtoro mwenzake mara waliporudishwa gerezani, walifungiwa mahali na kupigwa sana na baadhi ya askari wa gereza hilo .
"Upo ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba askari wafuatao ndio walishiriki kuwapiga wafungwa hao wawili," alisema waziri, akawataja askari wanaoshtakiwa sasa na akatoa pole kwa ndugu na jamaa wa mfungwa huyo aliyeuawa.
Kipigo hicho kilikuwa kikubwa hivyo kwamba, kilisababisha kifo cha Eradius. Baada ya kupata matokeo hayo ya uchunguzi, Kamishna Mkuu wa Magereza aliamuru askari hao wapelekwe polisi ili sheria ichukue mkondo wake, na sasa wanapelekwa mahakamani kwa kosa la mauaji.
Taarifa hizi zimekuja wakati Jeshi la Magereza likiwa linalaumiwa kwa tabia ya baadhi ya askari wake kuwatesa wafungwa kwa kuwapiga au kuzembea na kuacha vitendo visivyofaa kufanywa magerezani.
Waziri Chiligati alisema kwamba, wizara yake imesikitishwa sana na kifo cha mfungwa huyo na inalaani askari hao kuwapiga wafungwa kinyume cha taratibu na maadili ya Jeshi la Magereza.
"Serikali inapenda kuwahakikishia raia wote, walio magerezani na nje ya magereza, kwamba magereza yetu yanaendeshwa kwa kuzingatia sheria na haki za binadamu, hivyo vitendo vyovyote vya askari wa magereza vinavyokiuka sheria na taratibu za kuhudumia wafungwa na mahabusu magerezani, havitavumiliwa kwani vinachafua jina la Jeshi la Magereza na sura ya serikali kwa jumla," alisema Kapteni Chiligati.