NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, leo anatarajiwa kupata baraka za kimila nyumbani kwao Usangi, wilayani Mwanga, katika maombezi yatakayofanywa na wazee wa Chilla.
Habari kutoka Usangi zinaeleza kwamba, miongoni mwa watu mashuhuri watakaokuwa na Migiro huko ni mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo.
Migiro ambaye hivi karibuni aliteuliwa kushika wadhifa huo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, jana alikuwa Moshi mjini ambako alihutubia mkutano wa hadhara.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa ameongozana na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia, aliwataka Watanzania kuendelea kuuenzi umoja na mshikamano walionao na kuonya kuwa tofauti za kiitikadi isiwe chanzo cha kufarakana.
Migiro alisema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Moshi, akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani Kilimanjaro, yenye lengo la kuwaaga Watanzania baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Dk. Migiro aliwataka Watanzania kuendelea kuenzi amani na utulivu vilivyoasisiwa na waasisi wa taifa hili, Rais wa kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Alisema kuwa, waasisi hao, waliweza kuweka misingi mizuri ya kuheshimiana na kuaminiana na kuongeza kuwa, misingi hiyo mizuri imeifanya Tanzania kung’ara katika anga ya kimataifa.
“Nawaombeni Watanzania wenzangu tuendelee kutunza amani, umoja, mshikamano na haki za binadamu na pia tuendelee kujenga mshikamano wa kitaifa, kwani haya ndiyo malengo ya Umoja wa Mataifa,” alisema.
Alisema hivi sasa Tanzania inazidi kung’ara katika anga hiyo ya kimataifa, ambapo kwa sasa inao wanawake takriban wane, akiwamo yeye, ambao wanashika nyadhifa za juu katika taasisi za kimataifa.
Hao ni pamoja na Liberata Mulamula ambaye ni Katibu Mtendaji wa nchi za Maziwa Makuu, Amina Salum Ali, ambaye ni Mwakilishi wa Umoja wa Afrika, Marekani.
Wengine aliowataja ni Anna Tibaijuka, anayeshika wadhifa wa Mkurugezni wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT), na Gertrude Mongella, ambaye ni Rais wa Bunge la Afrika.