POLISI mkoani Mara, wamefanikiwa kumuua mtu mmoja anayedaiwa kuwa jambazi tishio, Magori Tito, mkazi wa Kijiji cha Nyakunguru wilayani hapa.
Jambazi hilo limeuawa katika operesheni ya kuwasaka majambazi na wezi wa mifugo iliyokuwa ikiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tarime, Constantino Bandola na Inspekta Didas Ishengoma.
Akielezea tukio hilo jana kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani Mara, David Saibul, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi, saa nane mchana nyumbani kwa mganga wa kienyeji jirani na machimbo ya dhahabu ya Nyabigena.
Katika tukio hilo, Ishengoma alijeruhiwa na jambazi hilo begani kwa kutumia bastola na alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema kuwa mkuu wa operesheni aliingia ndani na kumwona Magori ambaye alijaribu kutoroka kwa kuruka ukuta, lakini hakufanikiwa baada ya kukamatwa mguu na Inspekta Ishengoma.
“Baada ya Inspekta Ishengoma kupigwa risasi alimwachia, lakini alipotaka kuruka ukuta kwa mara nyingine ili akimbie, askari wengine waliokuwa nje walimpiga risasi kichwani na kumuua papo hapo,” alisema.
Kamanda Saibul alisema kuwa bastola aliyoitumia jambazi huyo kumpigia risasi mkuu huyo wa Kituo cha Polisi cha Nyamongo iko mikononi mwa polisi.
Katika tukio jingine, polisi wamemuua Mrimi Chacha Gekondo, mkazi wa Kijiji cha Itiryo, Kata ya Nyanungu wilayani hapa wakati wa operesheni hiyo.