Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tuzo yamwamsha Kawawa
Tuzo yamwamsha Kawawa
By Habari Tanzania | Published  01/24/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Peter Nyanje

WAZIRI Mkuu mstaafu, Rashid Mfaume Kawawa, amesema tuzo ya Martin Luther King Jr Drum Major, ambayo Ubalozi wa Marekani nchini umemtunukia mwaka huu, imefufua ari yake ya kulitumikia taifa.

Kawawa alikabidhiwa tuzo hiyo jana na Balozi wa Marekani, Michael Retzer, katika hafla iliyofanyika katika ofisi za ubalozi huo.

Katika hotuba yake kukubali tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka kwa mtu aliyejitoa kuitumikia jamii, Kawawa aliahidi kuwa licha ya kustaafu katika masuala ya uongozi, ataendelea kuisaidia serikali kwa ushauri atakapohitajika kufanya hivyo.

Alisema ingawa hayupo tena katika safu ya uongozi, bado anaendelea kutoa ushauri katika chama na serikali pale anapohitajika kufanya hivyo na kuahidi kuendelea kufanya hivyo kwa kadiri atakavyojaliwa na Mungu.

“Heshima iliyotukuka mliyonipa si tu imeniletea faraja, bali pia ni kichocheo cha kuendelea kuwatumikia Watanzania pale ambapo nitaweza kuwatumikia bila kujali itikadi zao za kidini au za kisiasa, kwa manufaa ya taifa kwa ujumla,” alisema Kawawa.
Kawawa, ambaye alistaafu katika uongozi wa umma katika miaka ya 1990, anajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

Mzee Kawawa analima mbogamboga, hususan uzalishaji wa uyoga, pamoja na ufugaji wa nyuki nyumbani kwake Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Aliieleza hadhara hiyo kuwa siku za hivi karibuni ameanza kupanda miti ya mbao, matunda na ile ya asili kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji kama sehemu ya kutekeleza wito wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais Jakaya Kikwete.

“Sasa nafuga nyuki na nipo tayari kumfundisha mwenzangu yeyote ufugaji wa nyuki wa kisasa,” alisema na kuongeza kuwa shughuli hizo zinaweza kumwongezea mtu kipato.

Kawawa aliushukuru Ubalozi wa Marekani hapa nchini kwa kumtunukia tuzo hiyo na kuitaka nchi hiyo tajiri kuendelea kuisadia Tanzania ili ipige hatua katika kujiletea maendeleo.

“Naomba mtupie macho makundi madogo madogo ambayo sauti zake hazijasikika, yapatiwe misaada ili yapate uwezo wa kujikwamua kiuchumi, yapate fursa sawa katika jamii ili uwezo walionao utumike kuleta maendeleo,” alisema.

Katika hotuba yake, Balozi Retzer alisema Kawawa, kama alivyofanya Dk. King, amesaidia kuleta mabadiliko katika fikra za watu wengi.

Alisema harakati alizozisimamia mzee Kawawa wakati wa uongozi wake, zinamfanya afanane na mwanaharakati huyo, kwani yale waliyoyapigania yanafanana.

Akisoma wasifu wa kiongozi huyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Mahusiano ya Jamii), Kingunge Ngombare -Mwiru, alimmwagia sifa mzee Kawawa na kusema nyuma ya ucheshi na ukarimu, unaoonekana nje, ndani yake yupo Kawawa ambaye aliwezesha mambo makubwa kufanyika.

“Kawawa, kijana niliyemfahamu, alikuwa ni mtu ambaye aliweka moyoni mwake na kutumia muda wake mwingi kuwatumikia Waafrika ambao walihesabika kama watu wa daraja la tatu wakati wa ukoloni,” alisema Kingunge.

Kutokana na kuguswa kwake na maisha ya Mwafrika wakati huo, alisema, Kawawa alikuwa mwanzilishi wa chama cha wafanyakazi wa serikali ya Tanganyika kilichokuwa na lengo la kutetea masilahi ya watumishi wa umma wakati huo.

Baadaye Kawawa alishiriki kuanzisha lililokuwa shirikisho la wafanyakazi, ambalo lilileta mageuzi makubwa hasa katika harakati za kudai uhuru.

“Komredi Kawawa alishika nyadhifa mbalimbali ndani ya serikali; uwaziri mkuu na umakamu wa rais. Anaheshimika kama mfanyakazi hodari na mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi haraka,” aliongeza Kingunge.

Awali, baadhi ya watu waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani, walitokwa machozi kufuatia sehemu ya hotuba ya hayati Martin Luther King, iliyotolewa kwa hisia kali na Yoseph Ayele, kutoka Tanzania Education and Information Services Trust (TanEdu).

Aliposimama jukwaani, tofauti na watu waliomtangulia, Yele hakuisoma sehemu ya hotuba hiyo, bali aliitoa kichwani, kama kuwahutubia watu waliopo mbele yake.

Hotuba hiyo inayojulikana kama ‘Nina Ndoto’, ambayo King aliitoa Agosti 28, 1963, jijini Washington, ni moja kati ya hotuba zake zinazoheshimika duniani, kwani imebeba ujumbe mzito unaoonyesha ndoto za watu waliodhulumiwa haki zao na matumaini yao kuwa siku moja watakombolewa.

Baadhi ya watu maarufu waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Katibu Mkuu mstaafu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye alitunukiwa tuzo hiyo mwaka jana.

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, ambaye alikuwa Mtanzania wa kwanza kupewa tuzo hiyo mwaka 1999, Balozi Daudi Mwakawago na watu kadhaa kutoka familia ya mzee Kawawa.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.