Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  CCM yadaiwa kumlinda mbunge aliyeghushi vyeti
CCM yadaiwa kumlinda mbunge aliyeghushi vyeti
By Habari Tanzania | Published  01/23/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Charles Mullinda

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejenga mtandao wa kumlinda Mbunge wa Buchosa, Samuel Chitalilo, anayetuhumiwa kughushi vyeti vya elimu yake, Tanzania Daima imedokezwa.

Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya chama hicho tawala zinaeleza kuwa, tuhuma dhidi ya mbunge huyo zilijadiliwa katika vikao vya juu vya chama na maamuzi ya kimya kimya yakafikiwa.

Moja ya vikao vinavyotajwa kuwa vilimjadili mbunge huyo, ni Kamati Kuu ambayo ilipokea hoja hiyo kwa maelekezo ya kiongozi mmoja wa juu wa chama hicho.

Habari zinaeleza, uamuzi wa kuamua kulimaliza suala hilo ndani ya chama ulifikiwa, lengo likiwa ni kuzuia kile kinachoonekana kuwa ni kukipaka matope ya wazi chama hicho tawala.

Habari hizo zimeeleza kuwa, katika kikao hicho, Chitalilo, ambaye alikuwa amewasilisha ombi la kulindwa na chama dhidi ya madai ya tuhuma zake kwa kiongozi mmoja wa juu wa serikali, aliitwa akahojiwa.

Kwa mujibu wa habari hizo, wajumbe wa kikao hicho nyeti cha CCM, waliafiki tuhuma za Chitalilo zibebwe na chama, lakini walikubaliana kumwadhibu kwa kumpiga marufuku kugombea uongozi kwa kipindi cha miaka 10.

Habari zaidi zimeeleza kuwa, kauli zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa serikali kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya tuhuma za Chitalilo si za kweli, na zinalenga kuficha maamuzi hayo ya CCM, ambayo mtandao wake ndio unaongoza serikali.

Wiki iliyopita, Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, aliliambia gazeti hili, upelelezi wa tuhuma zinazomkabili Chitalilo umekwishakamilika na jalada lake limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye analipitia kabla ya kushauri hatua za kuchukua kuhusu tuhuma hizo.

Hata hivyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikanusha kuliona faili hilo, na kueleza kuwa idara inayohusika na kesi za jinai ni ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Vicent Lyimo, jana alizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake Dar es Salaam, na kueleza kuwa tuhuma zinazomkabili Chitalilo ni za makosa ya kughushi, ambazo kwa upande wa serikali, zinashughulikiwa na Mkurugenzi wa Mashitaka.

“Idara inayohusika na makosa ya jinai ni ya Mkurugenzi wa Mashitaka, lakini DPP anaweza kuleta jalada la aina hiyo kama ameona kuna ugumu, na anahitaji msaada wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Binafsi siijui kesi hiyo na wala sijaona faili kama hilo katika ofisi hii, nakushauri nenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka, nina hakika utapata taarifa za uhakika kuhusu mwenendo wa uchunguzi wa shauri hili,” alisema Lyimo.

Tanzania Daima jana iliwasiliana na Kaimu Mkurugenzi wa Mashitaka, Laurance Kaduri, ambaye alikiri kufika kwa faili hilo ofisini kwake, lakini alisema lilikwishashughulikiwa na kurudishwa kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, likiwa na maelekezo ya hatua za kuchukua.

“Mimi ni mgeni katika ofisi hii, lakini ninazo taarifa kuwa jalada hilo lilikwishafikishwa hapa na kushughulikiwa na mwenzangu aliyekuwepo, likarudishwa kwa DCI kwa ajili ya utekelezaji wa hatua zilizokuwa zimependekezwa na ofisi hii.

“Sasa kinachoendelea, muulizeni DCI, kwa sababu faili hilo liliondolewa hapa likiwa na maelekezo yote… ila sijui, wala sikuwahi kusikia kama liliwahi kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Kaduri.

Alipolizwa kwa njia ya simu, Manumba alikiri kwamba faili hilo limekwisharudishwa ofisini kwake kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka, likiwa na maelekezo kamili.

“Ni kweli DPP ameturudishia faili hilo na ameelekeza kinachotakiwa kufanyika. Hivi sasa tunajiandaa kuanza kuchukua hatua… tunajiandaa kutekeleza aliyotuelekeza,” alisema Manumba.

Hata hivyo, alikataa kusema ni lini hatua zilizopendekezwa na DPP zitaanza kuchukuliwa, na ni kwanini imechukua muda mrefu kutekelezwa kwa hatua hizo.

Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu madai ya chama chake kuweka mkakati wa kumkingia kifua Chitalilo, alihoji ni kwani nini vyombo vya habari vinafuatilia suala hilo.

“Suala hilo linawahusu nini waandishi wa habari? Kwa nini mnalifuatilia sana? Mimi sina taarifa ya kukupa kuhusiana na hilo,” alisema Makamba kisha akakata simu!

Habari nyingine ambazo gazeti hili lilizipata kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jana hiyo hiyo, zilikuwa zikieleza kwamba, mwamuzi wa mwisho wa sakata hilo ni Rais Jakaya Kikwete.

Hata hivyo, Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Maura Mwingira, jana jioni alilihakikishia gazeti hili kwamba, suala hilo lilikuwa halijafikishwa kabisa kwa rais hadi hivi sasa.

“Nimeuliza kuhusu suala hilo na katibu wake amenihakikishia kuwa, faili hilo halijafika kabisa kwa Rais Kikwete,” alisema Mwingira.

Awali, kabla ya kuwasiliana na gazeti hili jana jioni, Maura alieleza kushangazwa na suala hili kutakiwa kushughulikiwa na rais wakati ni la kisheria.

Chitalilo alifunguliwa kesi ya kudanganya wapiga kura na vyombo vya dola kuhusu elimu yake na mpinzani wake wa kisiasa ndani ya CCM, Alfred Ngotezi, ambaye alibwagwa katika kura za maoni.

Katika kesi hiyo namba sen/ir/104/2006 iliyofunguliwa wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, Chitalilo anadaiwa kutoa maelezo ya uongo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na 2005.

Katika madai yake, Ngotezi alimtuhumu Chitalilo akidai kutoa taarifa za uongo kuwa, alihitimu elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Katikamu iliyoko nchini Uganda mwaka 1991 na baadaye akapata Stashahada huko Manchester nchini Uingereza.

Kama hiyo haitoshi, Ngotezi alilalamika kwa Waziri wa Usalama wa Raia kuhusu Chitalilo kutoa maelezo ya uongo na akatoa vielelezo vinaonyesha kuwa hakuwahi kusoma nchini Uganda.

Ngotezi katika malalamiko yake alisema pia kwamba, jina la Chitalilo lilikuwa halitambuliwi na Baraza la Mitihani la Uganda wala haliko katika orodha ya wanafunzi waliofanya mtihani katika Shule ya Sekondari Katikamu mwaka 1991.

Awali, Mwapachu alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa, tuhuma dhidi ya Chitalilo ziliwasilishwa kwake na zinafanyiwa kazi na polisi wa hapa nchini kwa kushirikiana na wale wa kimataifa (Interpol).


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.