MAJINA ya vigogo wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, yaliyowasilishwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Chifupa katika Wizara ya Usalama wa Raia na kwa Rais Jakaya Kikwete, yataendelea kuwa siri.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohammed Aboud, alisema kuwa, wizara yake haina mpango wa kuyatangaza majina yaliyomo katika orodha hiyo.
Aliliambia gazeti hili kuwa, hakuna kiongozi yeyote nje ya wizara hiyo asiyehusika na taasisi za usalama, ambaye ameiona orodha halisi ya majina ya watu waliotajwa katika barua aliyotumiwa Rais Kikwete.
Alisema baada ya kupokea majina hayo, upelelezi ulianza mara moja na wananchi watarajie kuona matokeo ya kazi hiyo, hivi karibuni.
Aboud alisema, baada ya Rais Kikwete kupokea orodha ya majina hayo na kuyawasilisha kwa Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, ambaye pia alikayabidhi kwa viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanyiwa kazi, uchunguzi ulianza kufanywa kwa tahadhari kubwa na usiri, ili kutoharibu ushahidi.
Alisema baada ya kuanza kwa uchunguzi huo, ilibainika kuwa, kunahitajia usiri wa hali ya juu, ili kufanikisha kazi hiyo kwa ufanisi, kwa sababu wauzaji dawa za kulevya ni wajanja na wenye uwezo mkubwa kipesa, hivyo ni rahisi kuharibu ushahidi.
“Tunachukua hatua kwa uangalifu sana, vinginevyo tutaharibu, tunawaomba wananchi wawe wastahamilivu, vita inaendelea na sisi tunaelekea kushinda, lakini hatutataja mtu miongoni mwa wote waliotajwa.
“Watuhumiwa waliotajwa katika orodha iliyopelekwa kwa Rais Kikwete ni wengi na aliowataja Amina nao ni wengi, lakini watabaki kuwa siri, si kwa sababu yoyote mbaya ila ni kwa mujibu wa taratibu za kufuatilia kesi za aina hii,” alisema Aboud.
Alisema vyombo vya usalama vinafuatilia kila mtu aliyetajwa kwa makini na uangalifu na vikithibitisha kuwa anahusika, anakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aboud alisema, hatua iliyofikiwa ni kubwa na wengi wa waliotajwa wamekwishachunguzwa. Aliahidi kuwa, mpaka mwishoni mwa mwezi wa Februari, wananchi watashuhudia hatua kubwa zitakazokuwa zimechukuliwa dhidi ya wale watakaokuwa wamethibitika kuhusika na biashara hiyo.
“Wapelelezi wamefika mbali katika kuwachunguza wote waliotajwa, mpaka mwisho wa mwezi ujao, wananchi watashuhudia hatua kubwa zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakaokuwa wamethibitika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya,” alisema Aboud.
Alisema uchunguzi umekuwa mgumu kwa sababu biashara ya dawa za kulevya ni ya muda mrefu na wahusika wameota mizizi na kujichimbia ndani ya jamii, hivyo kuwaibua imekuwa vigumu.
Alikiri kuwa, kupambana na wauza dawa za kulevya ni kazi ngumu na kuna baadhi ya taarifa za uongo zinazofikishwa polisi ili kuchanganya na kubaribu upelelezi.
Alisema moja ya sababu za kutowataja wanaodaiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, ni kupokea taarifa nyingi za uongo, kwamba wahusika wamekuwa wakisambaza orodha za uongo, yakiwamo majina ya watu maarufu na mashuhuri kwa ajili ya kupotosha ukweli na kuifanya kazi kuwa ngumu.
Aboud alisema kuwa, tayari polisi wamekwishagundua kuwa lengo la kusambaza orodha nyingi za uongo ni kuwachanganya polisi ili waendelee kushughulika na watu wasiohusika, huku wahusika wakiendelea kuwa salama.
“Hizi ni mbinu zinazotumiwa sana na wauza dawa za kulevya, wanajua jinsi ya kuwachanganya polisi, wanasambaza orodha ya watu wasiohusika kwa lengo la kujisafisha, wanawapa muda mgumu polisi, wa kushughulika na watu maarufu na mashuhuri, wanaowataja katika orodha zao, huku wao wakiendelea kupumua,” alisema Aboud.
Hata hivyo, alisema polisi imekwishagundua ujanja huo na inaendelea na kazi ya kuwashughukia kwa tahadhari wote waliotajwa, huku ikiwachuja wanaohusika na wanaobainika kuwa hawahusiki kabisa na biashara hiyo.
Aliwataka watu maarufu kutulia na kutotishwa na orodha zinazosambazwa sasa mitaani, ambazo zinadaiwa kuwa na baadhi ya majina ya watu mashuhuri wakiwamo baadhi ya viongozi serikali.