KWELI siasa mchezo mchafu. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yussuf Makamba, amebadili rangi akiwa Zanzibar na kuvaa sura halisi ya ukada, na kukichafua Chama cha Wananchi (CUF), akiwatumia wanachama waliokihama.
Makamba, mmoja wa makada wa CCM mwenye ushawishi, amechukua hatua hiyo, siku chache tu baada ya kukutana na viongozi wa juu wa CUF, walioongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika kufanikisha ajenda mahususi ya kujaribu kubomoa nguvu za CUF Zanzibar, mwishoni mwa wiki, Makamba aliwapandisha jukwaani, Tambwe Hizza na Ali Kinga Shamte, ambao wote kwa maneno tofauti walikivurumishia lawama nyingi chama chao cha zamani, ambacho wakati fulani walikuwa mstari wa mbele kukipigania.
Makamba alitumia mbinu hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mpendae, baada ya kukamilisha ziara yake ya mikoa mitatu ya Kisiwa cha Unguja kukagua uhai wa chama, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akihutubia umati wa wapenzi wa CCM, Tambwe ambaye alipata kuwa Mkurugenzi wa Uenezi wa CUF, kabla ya kuvuliwa madaraka hayo mwanzoni mwa mwaka jana, alieleza kuwashangaa Wapemba wanaoendelea kukikumbatia chama chake hicho cha zamani.
Katika hali iliyoonyesha dhahiri kumlenga Maalim Seif, anayeungwa mkono na watu wengi wa kisiwa hicho, Tambwe alisema ahadi nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa chama hicho cha upinzani, ni za uongo.
Alisema, uongo wa viongozi hao wa CUF kwa kiwango kikubwa ndiyo umekuwa sababu kuu ya wanachama wengi wa chama hicho kutoka Bara, kuamua kukihama.
Alisema kwamba, viongozi wa CUF kuanzia mwaka 1995 wamekuwa wakiahidi Dk. Salmin Amour hamalizi muda wake kwa madai amewaibia kura, lakini alimaliza muda wake na CUF imekuwa ikianguka katika chaguzi zote.
Kwa upande wake, Shamte aliitaka CUF kushughulikia kile alichodai kuwa, ni mpasuko ndani ya chama hicho, badala ya kudai Zanzibar kuna mpasuko wa kisiasa.
Alisema, kuna wajumbe wengi wa Baraza Kuu la CUF upande wa Bara wameondoka, hali inayoonyesha kuwapo kwa mpasuko ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, tofauti na makada hao wa zamani wa CUF, Makamba yeye aliwapa changamoto viongozi wa CCM Zanzibar, kuiga baadhi ya mambo yanayofanywa na Maalim Seif, kama mbinu ya kukiongezea chama hicho umaarufu.
Aliwaambia viongozi wa CCM kuwa, kwa kuanzia, ni vema wakaiga utendaji kazi wa kiongozi huyo wa upinzani, ambaye ametokea kupata umaarufu mkubwa.
Makamba aliwataka viongozi wa CCM kuiga mtindo wa Maalim Seif wa kutenda kazi ndani ya ofisi na nje kwani mambo hayo ndiyo yanayompandisha chati.
Akitoa mfano, alisema kuwa, Maalim Seif amekuwa na tabia ya kuwa karibu na wanachama wake kwa kuwatembelea wagonjwa hospitalini na vituo vya afya, kama njia ya kujiweka karibu na wananchi.
Aliwataka nao waige tabia hiyo, lakini katika hatua hiyo wasiende mikono mitupu, bali wabebe chochote kama vile matunda, ili kujenga uhusiano mzuri kati ya wananchi na chama.
“Kama umewekwa madarakani na watu, basi jipendekeze kwa watu, si familia yako,” alisema.
Mtindo wa kuwatembelea wagonjwa hospitalini umekuwa ukitumiwa sana na Maalim Seif na umeonekana kumpatia umaarufu mkubwa katika ulingo wa siasa za Zanzibar.
Makamba alisema kwamba, kama wao watashindwa kufika katika vituo vya afya na hospitali kutembelea wagonjwa, viongozi wa upinzani wataweza kuitumia fursa hiyo kujenga umaarufu wao na kutaka wakubalike.
Katibu Mkuu huyo wa CCM alijigamba kwamba iwapo yeye ataendelea kuwa katika nafasi hiyo, basi wapinzani wajue hawataingia Ikulu.
Aliwaeleza wafuasi wa CCM kuwa, yeye ni kiongozi makini na anaziweza siasa za ustaarabu na ubabe, na ndio maana akafanikiwa kuuongoza Mkoa wa Dar es Salaam kwa miaka 10 katika hali ya usalama