Na Ramadhan Semtawa
WAKATI Shirika la Posta (TPC) nchini linazidi kuchungulia kaburi Wizara ya Fedha na Miundombinu zinavutana juu ya namna bora zaidi ya kunusuru shirika hilo kongwe nchini, Mwananchi imebaini.
Mkutano huo unatokana na kila wizara kutaka kulinda shirika lililochini yake kati ya TPC na Benki ya Posta (TPB) yanayotakiwa kuunganishwa pamoja.
Wizara ya Fedha inaonekena kukataa mpango wa TPB kuunganishwa na TPC kwa hofu kwamba ufanisi wa benki hiyo ambayo ni hivi karibuni tu imeanza kujiendesha kwa mfumo wa kisasa, utayumba na hatimaye kushinda kukabilia ushindani wa kibenki nchini.
Hadi sasa serikali haijaweka bayana ni lini hasa TPC itaanza kushirkiano na TPB kama hatua ya shirika la posta lililo mahututi kiutendaji.
Hadi sasa TPC na TPB zinaendeshwa kwa sheria tofauti, yote yakiwa ni mashirika makongwe yaliyozaliwa baada ya kutenganishwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu (TPTC) lililoundwa baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Wizara ya Miundombinu inajitetea kuwa kuchelewa kwa mchakato wa kuunganisha mashirika hayo kunatokana na sheria tofauti zinazohusu vyombo hivyo, huku wizara ya Fedha ikisema inafanya tathmini ya kina kuona kitu gani kipya kitapatikana baada ya kuunganisha taasisi hizo mbili.
TPC inakabiliwa na hali mbaya kutokana na sababu kuu mbili, moja ni kwamba kazi zake nyingi sasa zinatolewa na sekta binafsi na pili ina madeni ya mamilioni iliyorithi ambayo yalikuwa bado hayajahakikiwa.
Madeni hayo ni ambayo imerithi wakati ilipotenganishwa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na TPB kutoka lililokuwa Shirika la Posta na Simu hapo mwaka 1994, fedha za malipo ya akiba (NSSF) kwa wafanyakazi wake waliokuwa chini ya Jumuiya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika mwaka 1977.
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alithibitisha kwamba TPC ina hali mbaya, lakini akasema ni vema ikafanyika tathmini ya kina kuona nini hasa kitakuwa ni kitu kipya baada ya kuunganisha shughuli za shirika na benki.
"Hakuna asiyejua kwamba posta ina hali mbaya, lakini kinachofanyika sasa ni tathmini ya kina, tunataka kuona baada ya kuunganishwa shughuli zao kitu gani kipya hasa kitakuwepo," alisema Mgonja.
Mgonja alifafanua kwamba, kitu kipya ambacho kinafanyiwa tathmini ya kina ni pamoja na kama kutakuwa na huduma mpya zaidi ambayo sasa haipo.
Naibu Waziri Miundombinu, Dk Maua Daftari kwa upande wake alisema licha ya sheria tofuati zilizounda taasisi hizo mbili, bado kuna suala jingine gumu la kuhakiki madeni, kuangali jinsi ya kupata mtaji wa shirika na uwezekano wa kufutwa kwa deni hilo.
Dk Daftari alisema hadi sasa tayari Tume ya Rais ya Mashirika ya Umma (PSRC) imekwisha kutathmini madeni hayo, ambayo hata hivyo alisita kutaja kiasi halisi.
Naibu Waziri huyo aliongeza kwamba, kinachosubiriwa sasa ni waraka wa kunusuru shirika hilo kupelekwa katika kikao cha baraza la mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa maamuzi.
Alisema katika mchakato huo jambo ambalo limekuwa likiangaliwa ni jinsi ambavyo TPC itaweza kusaidia huduma za benki kwenye maeneo ambayo benki haijafika na jinsi ambavyo benki itaweza kusaidia shirika maeneo ambayo halijafika.
Uchunguzi unaonyesha ingawa serikali kupitia wizara hizo mbili inajitetea kufanya tathimini hizo za kina, bado kuna msuguano ambao unaonyesha kwamba TPC ikijipenyeza ndani ya TPB itakuwa mzigo kwa benki hiyo.
Imebainika kwamba, upande mmoja ambao ni Wizara ya Fedha unaona kwamba hadi sasa hakuna athari za upatikanaji huduma ambazo wananchi wamezipata licha Posta kuwa katika hali mbaya.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa Wizara ya Fedha imekuwa ikiangalia zaidi kama TPC kuwa hoi kunaweza kuathiri huduma kwa wananchi na si kuangalia njia za kulinusuru shirika.
Msimamo wa Wizara ya Fedha katika mchakato huo, unaangalia zaidi pia kwamba kuwapo ukiritimba wa TPC katika kutoa huduma hakuwezi kuchochea ushindani wala kukuza sekta hiyo.
Wakati Wizara ya Fedha ikiamini hivyo, Miundombinu ambayo ndiyo yenye dhamana na TPC imekuwa ikiangalia zaidi kulinusuru shirika ingawa inafahamu kwa sasa hakuna athari za ukosefu wa huduma kwa wananchi kwani sekta binafsi inatoa huduma kama za shirika hilo.
Mchakato wa serikali kulinusuru shirika ulianza tangu mwaka juzi kufuatia shirika hilo kukabiliwa na ushindani mkubwa huku likiwa na mzigo huo wa deni