Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Viongozi wa CCM watunishiana misuli
Viongozi wa CCM watunishiana misuli
By Habari Tanzania | Published  01/22/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Mussa Juma, Arusha

Viongozi wa CCM mkoa wa Arusha wameanza kutunishiana misuli kutokana na kuhusika katika kashfa ya kuvamia viwanja na kukataa kujiuzulu.

Ukweli huo umeibainika juzi baada ya Meya wa Manispaa ya Arusha, Paul Laizer, anayekabiliwa na shinikizo la kutakiwa kujiuzulu kutoka kwa uongozi wa CCM Mkoa wa Arusha, kusema tuhuma dhidi yake ni majungu matupu.

Akizungumza na Mwananchi kujibu shinikizo la Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Arusha la kutamka ajiuzulu wadhifa huo pamoja na madiwani wenzake wawili, mbali ya kudai hajapata barua ya kumtaka ajiuzulu, alisisitiza kwamba mji wa Arusha umezidi majungu.

Laizer na madiwani wenzake wawili wiki iliyopita walitakiwa na Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Arusha kujiuzulu nyadhifa zao kwa madai ya kuhusika na ugawaji wa viwanja kinyume cha taratibu.

Hatua hii ya Laizer na wenzake imezidisha mgogoro ndani ya CCM wilayani ambao umekua ukichemka kwa muda mrefu sasa.

Madiwani hao, walipewa saa 24 hadi kufikia jana wawe tayari wamejiuzulu la sivyo, watafukuzwa uanachama wa CCM na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa nyakati tofauti, Laizer na Diwani Mussa Mkanga wa kata ya Sombetini, walisema kuwa taarifa za kuwataka wajiuzulu wamekuwa wakisikia tu, lakini bado hawajapata barua yoyote.

"Hata mimi nimesikia hilo, lakini nadhani kuna taratibu wanapaswa kufuata kwanza watupe barua za kujiuzulu na sababu zao na ndipo tutaamua cha kufanya," alisema Laizer.

Meya Laizer ambaye ni Diwani wa kata ya Baraa, alisema tuhuma zote ambazo zimekuwa zikitolewa dhidi yake ni majungu, lakini anamuachia Mungu.

"Mimi namuachia Mungu...nadhani hata wewe unajua majungu ya mji wetu wa Arusha...na tuhuma zote unazijua sasa mimi nisemeje," alisema Laizer alipotakiwa na mwandishi wa gazeti hili kueleza msimamo wake juu ya tuhuma zinazomkabili.

Hata hivyo, alisema uamuzi wa ama kujiuzulu au la atautoa mara baada ya kupokea barua rasmi.

Naye, Diwani Mkanga ambaye ni moja wa madiwani maarufu mkoa wa Arusha, alisema hadi kufikia jana alikuwa hajapokea barua yoyote ya kumtaka ajiuzulu.

"Mimi sina taarifa kamili za kunitaka nijiuzulu ndio nasubiri barua nikipata nitawapa jibu," alisema Mkanga.

Hata hivyo, alisema kama ni kweli yeye na wenzake wawili wametakiwa kujiuzulu ni uonevu mkubwa kwani maamuzi yote ambayo walikuwa wakifanya ni maamuzi ya baraza la madiwani na halmashauri.

"Sijui wametumia vigezo gani, lakini sisi tulikuwa tunafanyakazi kwa mujibu wa sheria na taratibu na kama tuna makosa kwanini tuonekane sisi pekee?" alihoji Mkanga.

Diwani mwingine wa viti maalum(CCM) toka jumuiya ya wanawake wa CCM, Mary Kisaka, hakupatikana jana kuelezea kama amepata barua au la, lakini juzi jioni alikuwa pamoja na wenzake mara baada ya kikao cha Halmashauri Kuu Mkoa.

Hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mohamed Mbonde, akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana alisema tayari madiwani hao wamepelekewa barua zao.

"Barua zimetolewa, lakini taarifa kamili tutatoa kesho (leo) saa 10 jioni naomba uwe na subira," alisema Mbonde.

Kuondolewa kwa madiwani hao kumetokana na tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya uongozi, kubwa likiwa ni ugawaji wa viwanja kinyume cha taratibu.

Moja ya viwanja hivyo, ni kiwanja kilichokuwa stendi ya muda wa mabasi ya jijini Arusha ambacho madiwani hao walikitoa kwa kampuni moja ambayo inamilikiwa na wafanyabiashara kadhaa maarufu akiwapo mawaziri mmoja wa serikali ya awamu ya nne.

Kiwanja hicho, tayari baraza la madiwani lilikipanga kitumike katika ujenzi wa sekondari ya jiji, ambayo ilipata wafadhili toka nchini Australia ambao waliahadi kugharamia zaidi ya asilimia 50 ya ujenzi wake.

Hata hivyo, kutolewa kwa kiwanja hicho, ambacho tayari kampuni hiyo, ilikwisha kukizungushia uzio, kuliibua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na kusababisha mkuu wa mkoa Arusha wakati huo Mohamed Babu kuagiza iundwe tume ya madiwani kufanya uchunguzi.

Hata hivyo, tume hiyo ambayo iliongozwa na Diwani Belina Kabuje, pamoja na kutoa taarifa yake miliki hiyo kwa kampuni binafsi iliendelea Mkuu wa Mkoa wa sasa, Kanali Samuel Ndomba, alisitisha kuendelezwa kwa kiwanja hicho sasa.

Mbali ya madiwani hao, tayari watendaji kadhaa wa manispaa ya Arusha wamekwisha kuchukuliwa hatua ikiwapo kufikishwa polisi na wengine kuhamisha kutokana na suala hilo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.