KAMA unataka kumgusa Rais Jakaya Kikwete, kuna watu unaopaswa kukaa mbali nao. Orodha yao ni ndefu kidogo. Baadhi yao wamo serikalini, wengine wamo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); wengine ni wafanyabiashara. Wanajijua, nami nawajua. Kama unamwogopa Kikwete, kaa mbali nao.
Lakini wakati mwingine ni vema kukaa nao karibu; si kujiingiza katika ‘mtandao’ wao, bali kuwajadili, kwa kuwa wengi wao wameshikilia nyadhifa nzito, dhamana kubwa, zinazojihusisha moja kwa moja na maisha ya kila siku ya Watanzania.
Hatuna sababu ya kuwaacha watu wanaoathiri maisha yetu, kwa uzuri au kwa ubaya, wafanye watakavyo, hasa pale tunapojua wamepotoka. Tuwasahihishe. Kama nilivyoanza, tusisahau kuwa ukimgusa mmojawapo wa ‘maswahiba’ wa rais, unamgusa rais mwenyewe, hata kama hukudhamiria!
Uchambuzi huu utamgusa Rais Kikwete kwa kumtaja Spika wa Bunge, Samuel Sitta. Anamhusuje Rais Kikwete?
Sikiliza. Inaaminika kwamba Sitta ni mmoja wa waasisi wa kaulimbiu ya Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya. Kwamba waliasisi kaulimbiu iliyotangazwa na baadaye kutumiwa na akina Kikwete katika kuutafuta urais; na ambayo sasa inaimbwa na kila anayetaka kuisifu Serikali ya Awamu ya Nne.
Bila shaka, Sitta ni rafiki pia wa Edward Lowassa, Waziri Mkuu, na rafiki wa Kikwete. Si ajabu kwamba ukaribu huo ndio uliomfanya Kikwete awafikirie wote wawili katika nafasi ya uwaziri mkuu, na hatimaye akampa Lowassa ambaye alizungumzwa sana hata kabla ya kampeni kwisha.
Inasemekana kwamba nguvu ya Kikwete ‘iliyosambazwa’ kitaalamu siku alipokuwa anajipongeza kwa kuingia Ikulu, Desemba mwaka jana, ndiyo iliyosimika ‘kukubalika’ kwa Sitta na ndiyo ‘iliyomng’oa’ Pius Msekwa – aliyechelewa kujua kinachoendelea.
Kwa nguvu ya Kikwete, Sitta na Lowassa wamejikuta wakiwa na nafasi nyeti katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Wakati Sitta akiwa kiongozi wa Bunge zima, Lowassa ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.
‘Kimbunga’ kilichomwondoa mzee Msekwa katika Uspika - huku ‘walevi wa Ari mpya’ wakimwita Agano la Kale - ndicho kilichomwingiza Sitta; mwasisi wa Ari mpya aliyefananishwa na Agano Jipya.
Dharau na kejeli alizopata Msekwa kutoka kwa wanachama wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zililingana kwa uzito na heshima aliyopewa Sitta. Kukata tamaa kwa wabunge kulikowekwa mgongoni kwa Msekwa, kulilinganishwa na matumaini makubwa waliyokuwa nayo kwa Sitta.
‘Uzee’ ulioonekana ndani ya Msekwa, ulipimwa katika ‘ujana’ wa Sitta. ‘Udikteta’ uliohusishwa na Msekwa, ulilinganishwa na uvumilivu, uelewa na upeo wa kidemokrasia wa Sitta. Maneno haya yote, na mengine, yalitumiwa na ‘wanamtandao’ kumng’oa Msekwa na kumsimika Sitta.
Walichokosea (bila shaka kwa makusudi) mashabiki wa mwasisi wa Ari mpya, ni kwamba hawakuwahi kuzungumza waziwazi hata mara moja juu ya ubora wa Sitta. Waling’ang’ania ubaya wa Msekwa. Lakini inasemekana kwamba walio wengi hawakusukumwa na uzuri wa Sitta, bali nguvu ya Kikwete.
Je, Sitta amejitofautishaje na Msekwa? Nakumbuka alijaribu kujitofautisha mwanzoni. Mara alipoanza tu kazi, alitangaza kuwa asingevumilia majibu yasiyoridhisha kutoka kwa mawaziri bungeni. Alipoziangalia kanuni za Bunge, akakereka, akanuna!
Akafanya uamuzi mzuri wa kuzirekebisha. Akaunda timu ya ‘wataalamu’ wa kuziangalia na kuzitengeneza upya ili ziendane na Bunge la zama hizi, linaloongozwa kwa kasi na viwango. Alitamani ajenge Bunge lenye heshima ya kuitwa mhimili wa dola, lisilokaa katika kwapa la dola, na lenye nguvu ya kuisimamia serikali; Bunge la Watanzania si la wana CCM.
Hakujua. Wenzake hawakuipenda kasi yake. Inasemekana kwamba mashabiki wake hawakupendezwa na viwango vyake, na kwamba aliwakera wakubwa wenzake, akawakera wabunge wengi wa CCM wanaofaidi matumizi mabaya ya kanuni zilizopo. Tume yake ikaanza kuwekewa mitego ya chini chini na wanamtandao wale wale, tena wakubwa!
Baadhi ya wakubwa wakaanza kusema chini chini kwamba Sitta amewasaliti. Eti anawalinda wapinzani – kana kwamba wapinzani si wabunge! Wakaunda mkakati wa kumshughulikia, na hata kuzuia kanuni mpya kupitishwa, au zipite zikiwa zimehaririwa na kuwa kama wanavyotaka! Nasikia wamejipanga kuzuia Ari mpya ya Sitta!
Pole pole, Sitta naye akaanza kugundua kinachoendelea. Inavyoelekea, naye sasa ameanza kuwaogopa wanamtandao. Yawezekana ndiyo maana kanuni mpya hazijatangazwa, ingawa taarifa zinasema kwamba kamati hiyo ilikwishamaliza kazi muda mrefu. Zipo wapi? Zinafanyiwa uhariri? Zinachunguzwa na kupangiwa hoja ya kuzipinga?
Kwa kuwajua wanamtandao wenzake, na kwa kuwaogopa, Sitta sasa ameanza kubadilika. Anaanza kuwa kama Msekwa. Anataka kupima, kuongoza na kutawala mawazo na kauli za wabunge nje ya Bunge. Anatamani kuwaridhisha wakubwa. Heshima ya Bunge aliyotaka kujenga inaelekea kumshinda. Anataka kuendekeza uanamtandao, si utaifa. Anaanza ushabiki wa vyama ndani ya Bunge.
Mawaziri wameanza kutoa majibu yasiyoridhisha mbele yake, kwa kuwa wanajua mambo yakiharibika, waziri mkuu atawatetea kwa kishindo. Viwango vimeanza kupotea. Kasi haionekani. Kuna nini?
Hapana. Huyu si Samuel Sitta tuliyemjua na tuliyemtarajia. Si lile Agano Jipya tuliloletewa na wanamtandao. Maana kama ni yeye, yametokea wapi haya? Kwa nini asijenge utukufu wa Bunge, akahakikisha linajiendesha lenyewe bila kuingiliwa na serikali?
Leo hii tukiwahoji waimbaji wa Agano Jipya, Sitta ana tofauti gani na Msekwa? Inawezekanaje hata mwasisi wa kaulimbiu ya Ari mpya anashindwa kuonyesha makali? Yawezekana ari hii haimo ndani mwa wanaoiimba; bali midomoni mwao?
ansbertn@yahoo.com
+447828696142