MOJA ya habari nzito katika toleo hili ni kuhusu madai ya baadhi ya watu walijitokeza wakidai kuwa, ndugu zao wamekamatwa na kufunguliwa kesi za jinai kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni chuki binafsi.
Msako unaodaiwa kuwanasa watu hao ni ule ulioendeshwa hivi karibuni na Jeshi la Polisi katika mikoa mbalimbali nchini dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na ujambazi.
Walalamikaji hao, wanadai kwamba mmoja wa watu waliokamatwa katika operesheni hiyo mkoani Kagera, Deus Mzuri anayehusishwa na vitendo vya ujambazi pamoja na ufadhili wa kazi hiyo, wanasema kwamba, ndugu yao amekamatwa kutokana na chuki binafsi ya Mkuu wa Polisi wilayani humo (OCD).
Wamekwenda mbali zaidi katika kuelezea uhasama ulivyoanza kati ya mtuhumiwa na OCD huyo, hadi majuzi kabla ya kutiwa mikononi mwa polisi.
Katika kusisitiza madai yao, wameandika pia barua ya malalamiko kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Mkuu wa Mkoa wa Kagera (RC), Mkuu wa Polisi Mkoa wa Kagera (RPC), Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo (DC) na Ofisa Usalama wa Taifa (DSO) wilayani Biharamulo. Tanzania Daima imefanikiwa kuiona nakala ya barua hiyo.
Hatupendi kuingilia utendaji wa Jeshi la Polisi, hasa katika kipindi hiki kigumu, lakini kinachoonyesha mafanikio katika mapambano makali dhidi ya uhalifu nchini.
Hata hivyo, hatusiti kueleza kwamba, tuhuma dhidi ya jeshi hilo zinaongezeka kila kukicha.
Mbali ya aina ya lawama zilizotolewa na ndugu wa Mzuri, malalamiko kadhaa dhidi ya polisi yamekuwa hayakauki kutoka kwa wananchi, wakidai kuonewa na walinzi hao wa usalama wa raia na mali zao nchini.
Baadhi wanadai ndugu zao hufikia hata kupoteza maisha, ama kutokana na vipigo vya polisi, au kwa kubambikiwa kesi zinazowapeleka katika suluba kali katika mahabusu, huku wakiachwa kwa muda mrefu bila kufunguliwa mashitaka, hali inayowafanya wadhoofu kiafya.
Hatupendi kukumbushia matukio mbalimbali yanayohusu hoja hii, lakini tunapenda kuushauri uongozi wa Jeshi la Polisi nchini kutofumbia macho vilio vya wananchi, hasa katika kipindi hiki ambacho imani yao kwao ni kubwa.
Kinyume cha hapo, licha ya jeshi hili kujishushia hadhi kwa wananchi, kwa upande mwingine linaweza kusababisha kuibuka kwa uhasama mkubwa baina yao na raia.
Kwa hakika, tusingependa kuona mbegu za chuki zinachukua sura mpya, baada ya upande fulani kuchoshwa na uonevu na udhalilishwaji.
Ndiyo maana tunasema kwamba, Jeshi la Polisi lisifumbie macho madai ya aina hii, bali juhudi za dhati zifanyike kuhakikisha raia wanachukuliwa hatua kutokana na maovu yao, lakini si kinyume cha hapo