Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kuchangia maendeleo ni wajibu wetu sote
Kuchangia maendeleo ni wajibu wetu sote
By Habari Tanzania | Published  01/20/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

MWEZI huu nimepata fursa ya kuzitembelea kikazi wilaya za Kigoma, Kasulu na Kibondo katika Mkoa wa Kigoma. Nikiwa katika wilaya hizi, nilibahatika kutembelea maeneo mbalimbali, ambayo yalikuwa yamekumbwa na mvua kubwa, kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchi.

Nikiwa mjini Kigoma, nilipata fursa ya kuwatembelea jamaa zangu waishio katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo; lakini maeneo yaliyonisukuma niandike makala haya ni Bangwe, Mjimwema na Kilimahewa.

Kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mkoani humo, Desemba, mwaka jana na Januari, mwaka huu, maeneo mengi ya Mjimwema na Kilimahewa barabara zake zilikuwa zimechimbika kiasi kikubwa.

Hali hii ilinisukuma kuwauliza baadhi ya watu waishio maeneo haya kulikoni barabara zao ziharibike kiasi kile, bila ya wao kuchukua hatua thabiti kuzikarabati, ilhali ni wao wenyewe waliokuwa wakipata taabu ya kupita kwenda majumbani na makazini kwao pia.

Mmoja kati ya watu hao alinijibu kwa mkato: “Kwa nini wananchi tusumbuke kukarabati barabara hizi wakati serikali (bila shaka ya manispaa) ipo? Kukarabati barabara siyo kazi yetu bwana!”

Mimi nilimkumbusha kwamba, lakini waliokuwa wakipata taabu kupita katika barabara zilizochimbwa na nyingine kuzolewa kabisa na mvua walikuwa ni wao wananchi na si vinginevyo; alicheka na kuniambia: “Ndugu yangu kama huna jambo lingine la kuongea bora unyamaze. Iweje sisi tuhangaike kukarabati barabara wakati hiyo ni kazi ya serikali?”

Nilimpa mfano wa Mtaa wa Kiluvya katika Manispaa ya Kinondoni (kilomita thelathini hivi kutoka jijini Dar es Salaam), ambako Januari 13, mwaka huu, nilibahatika kuhudhuria, kwa mara ya kwanza, sherehe ya kuukaribisha mwaka huu nikiwa mwanachama mpya wa Kiluvya Development Association (KILUDEA).

Nilimweleza jamaa yangu huyo kwamba, kupitia KILUDEA, Mtaa wa Kiluvya umekuwa ukitumia nguvu na jitihada za wana-Kiluvya kutengeneza, kukarabati na hata kuweka miundombinu ya msingi ikiwamo barabara, mabomba na hata kujenga shule.

Nilichoambulia ni majibu ya kejeli kutoka kwa jamaa yangu huyo, kwamba maoni yangu yalikuwa hayana ukweli wowote, na kwamba wajibu wa kukarabati barabara zote, hata za pembezoni mwa miji yetu, ni wa serikali.

Nakubaliana na hoja kwamba, serikali (iwe kuu au ya mtaa) ina wajibu, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba miundombinu yote ya msingi, ikiwamo barabara, inakuwa katika hali nzuri.

Hata hivyo, napenda pia kusisitiza hoja kwamba kuna wakati au mahali ambapo serikali (kuu au ya mtaa) inapaswa kuungwa mkono na wananchi au asasi mbalimbali za kijamii katika jitahada zake za kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Hoja hii inasisitizwa hapa kwa kutilia maanani mambo kadhaa: Kwanza, kwa mujibu wa ibara ya 8(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika shughuli za serikali yake kwa mujibu wa masharti ya katiba hii na sheria zilizotungwa chini yake. Hii ni kwa sababu, chini ya ibara ya 8(1)(a) ya katiba ya nchi, “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii.” Na lengo la serikali yetu, chini ya ibara ya 8(1)(b), ni kuhakikisha ustawi wa wananchi wake – yaani, sisi Watanzania.

Aidha, wananchi wana wajibu, chini ya ibara ya 27(2) ya katiba, wa “kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu; na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Hali kadhalika, chini ya ibara ya 28(1) ya katiba, kila Mtanzania ana wajibu wa “kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa.”

Hivyo, kwa mujibu wa vipengele hivi vya katiba ya nchi, kila mwananchi anawajibika kushiriki katika shughuli zinazolenga kutimiza lengo la serikali la kuhakikisha ustawi wa wananchi wake.

Hoja ya pili inayotusukuma tusisitize kwamba wananchi wana wajibu wa kushiriki katika shughuli zenye lengo la kuboresha miundombinu mbalimbali katika maeneo yao na hivyo maisha yao wenyewe, ni uzoefu tuliokuwa nao sisi Watanzania wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Enzi hizo, kupitia siasa ya ujamaa na kujitegemea, wananchi tulikuwa tukishiriki katika shughuli za maendeleo yetu sote kwa pamoja kupitia mfumo wa bega kwa bega.

Kwa mfano, zama hizo, sisi Watanzania tulikuwa waumini wa siasa ya Ujamaa (na si Ukomunisti), sera iliyosisitiza kufanya kazi kwa bidii, kwa ushirikiano na kwa manufaa ya taifa letu lililokuwa changa.

Hii tulifanikiwa kupitia elimu ya kujitegemea tuliyokuwa tukipata mashuleni na baadaye kuitumia ‘mitaani’ punde tulipomaliza masomo au mafunzo yetu. Wakati huo, hakuna mtu aliyepinga kuhudhuria, japo mara moja moja, kwenye shughuli za umma kama vile kutengeneza au kukarabati barabara ya kijiji au ya mtaa; kuchimba kisima au mfereji wa kupitisha mabomba ya maji.

Lakini leo hii, wananchi (hata wa maeneo ya vijijini) wamefikia mahali ambako wakiambiwa na watendaji wa serikali za mitaa washiriki, kwa mfano, kuchimba mifereji ya kupitishia mabomba ambayo yametolewa au kununuliwa na wafadhili au serikali, wanakataa kufanya hivyo.

Huko maeneo ya vijijini mambo ndiyo mabaya zaidi, kwani wananchi wanataka kila kitu kifanywe na serikali za halmashauri za miji au za wilaya. Kwa mfano, katika baadhi ya maeneo ambayo nimebahatika kutembelea hapa nchini, utakuta wananchi wanakataa kujitolea kujenga madarasa ya shule za msingi au sekondari katika wilaya zao, eti kwa sababu ni wajibu wa serikali kufanya hivyo.

Lakini swali la kujiuliza hapa ni; hivi serikali ikiacha au ikichelewa kujenga madarasa ya kutosha kuingiza watoto wote waliomo katika maeneo yetu, ni watoto wa nani watakaokosa nafasi ya kusoma? Wa watendaji wa serikali au wa kwetu sisi (hohehahe) wenyewe tunaokataa kushiriki katika maendeleo ya miundombinu muhimu katika jamii zetu husika?

Ndiyo sababu safu hii inapenda kuipongeza KILUDEA kwa jitihada zake inazozifanya kuufanya Mtaa wa Kiluvya kuwa mahala pazuri, nadhifu na salama kuishi katika siku za usoni.

Kwa muda wa miaka sita ambayo KILUDEA imekuwa ikifanya shughuli zake tangu ianzishwe mnamo mwaka 2001, imeweza kushirikiana na uongozi wa Mtaa wa Kiluvya na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha kwamba, barabara za mtaa huo ni nzuri na zinapitika.

Ukirejea historia ya nchi nyingi zilizoendelea, serikali husika zilichofanya, au zinachokifanya, ni kutunga sera na sheria madhubuti, na kuweka miundombinu iliyowawezesha wananchi kufanya shughuli zao binafsi na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi zao kwa ufanisi.

Zilichokifanya serikali hizo, au zinachokifanya nchi za Asia ambazo sasa ndizo zinazopiga kasi katika maendeleo, ni kuwafundisha wananchi wake kuvua samaki na si kuwapatia samaki.

Kinyume chake, wananchi wengi hapa Tanzania tunataka serikali yetu kuu au zile za mitaa zitufanyie kila kitu, kitu ambacho ni sawa na kupewa samaki badala ya kujifunza kuvua samaki.

Ikumbukwe pia kwamba, wakati huko nyuma ilikuwa rahisi kwa serikali kufanya mambo mengi kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma zote za kijamii (kama elimu, matibabu, n.k.), sasa imekuwa ni vigumu kwa serikali yetu kufanya hivyo.

Ziko sababu nyingi zinazoifanya serikali isiweze kutoa huduma hizo kwa urahisi kama ilivyokuwa zamani, lakini kubwa hapa ni ongezeko la kasi la idadi ya Watanzania.

Wakati Tanzania ikipata uhuru mwaka 1961, idadi ya Watanzania ilikuwa milioni saba na ushee tu, leo hii, miaka 45 baada ya uhuru, Watanzania tumefikia zaidi ya milioni 30, asilimia zaidi ya hamsini kati yetu wakiwa watoto.

Hali hii imeifanya serikali kuwa na mzigo mkubwa katika kuwahudumia Watanzania katika nyaja zote za huduma za jamii. Kwa mfano, kutokana na ongezeko kubwa la watu katika Jiji la Dar es Salaam, serikali za manispaa zote tatu za jiji hili (Ilala, Temeke na Kinondoni), zimeshindwa kabisa kuweka miundombinu madhubuti, kama barabara na maji, katika maeneo mapya ya makazi hapa jijini.

Hoja ya msingi hapa ni; je, tuiachie serikali ifanye kila jambo – hata kama ni kukarabati barabara zetu za pembezoni tuishipo kama alivyosema jamaa yangu wa Kigoma, au tushirikiane na serikali pale tunapoweza kufanya hivyo ili tuyafanye makazi yetu yawe mahala pazuri pa kuishi kama wenzetu wa Kiluvya kupitia KILUDEA?

Ni rai ya safu hii kwamba, ili tuweze kuyafanya makazi yetu kuwa mahala pazuri pa kuishi, ni vema tukashiriki katika shughuli za kuboresha makazi yetu wenyewe kwa kushirikiana na serikali zetu za mitaa husika.

Aidha, ni rai yetu kwamba, sisi wananchi wa Tanzania tunao wajibu wa kushirikiana na serikali yetu kufanya Tanzania kuwa mahala pazuri pa kuishi, na hivyo kuwawezesha watoto na wajukuu zetu kurithi nchi yenye miundombinu thabiti. Jambo hili limewezekana sehemu nyingine hapa duniani; hivyo, hata Tanzania pia linawezekana kama tutanuia.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.