NAITWA Mpayukaji mwana wa Msema hovyo. Januari 12, mwaka huu nikiwa napitapita kwenye mitaa ya Kariakoo pale Shule ya Uhuru mduara, jijini Dar es Salaam, kwa mara ya kwanza tangu mwaka huu uanze, nilinunua gazeti la Tanzania Daima.
Awali nilikuwa nimeamua kuacha kununua magazeti kitambo baada ya kuwa nasoma mambo ambayo sikutegemea kama yangemshughulisha mtu.
Kumbe nilikuwa nimekosea. Maana rafiki yangu alikuwa mara kwa mara akiniambia kuwa magazeti yamebadilika. Lakini mimi nilikuwa siku zote namkatalia.
Huyu rafiki yangu ni bingwa wa kuchungulia magazeti pale kijiweni kwa muuza magazeti. Huyu bwana, ili kubana matumizi, amelazimisha urafiki na muuza magazeti ili ajipatie huduma ya bure ya kusoma kwa njia ya kuchungulia. Hivyo mara utamuona akimnunulia kahawa. Mara akisifia shati lake chafu na chakavu ili mradi lake litimie.
Baada ya Bwana Mchunguliaji kuwa amekamilisha zoezi lake la kusoma magazeti bila kulipa, huyo alitoka mkuku kuja kijiwe chetu cha kahawa (Jina ni top secret maana wanoko wanaweza kuja kutuvamia na kuzusha varangati bure), akitweta utadhani kakimbizwa na nyati! Mara alianza kusema: “Mpayukaji, mwaka huu lazima ununue magazeti bwana.” Nilimuhoji kulikoni hadi nibadilishe msimamo wangu?
Kabla hata sijamaliza kuwaza na kuwazua, mara Makengeza, huyu ni mwanakijiwe chetu, bingwa wa kuona visivyoonekana kirahisi, alidakia. “Kwani kuna nini nawe?”
Mchunguliaji bila kujali anamjibu nani, alijibu: “Bwana we umeona zile nanga zilizoshushwa kwenye Tanzania Daima?”
Kusema ukweli, wote tulipigwa butwaa maana kawaida ya Mchunguliaji ni kusoma na kuja kututambia kuwa anazo kwani husoma magazeti kila siku asijue tunajua kuwa anachungulia.
“Eee Bwana, kwanza kuna Gabacholi kakiri kuponyoa madafu bilioni 125 kutoka kwenye dili lilee la Rada.” Aliangalia huku na huku kuona tumeipata vipi kisha akaendelea. “Pili ni maoni ya mhariri. Kazoza kuwa lazima Mkuu akumbushwe kurejesha nyumba zetu walizogawiana wale wezi kule kijiweni kwao nonihino.”
Uliwahi kuona siafu waliochokozwa na baiskeli? Basi ndipo jamaa mmoja aliyeonekana kuvutiwa na habari hizi, alitoa ofa ya kahawa na kashata kwa wanakijiwe wote. Mara tabasamu hizo.
Si unajua tena wengi wa watu wa Bongo kashata ni mkate na kahawa ni chai? Imetoka, hicho ndicho kifungua kinywa.
Kwa wanakijiwe wetu ambao kimsingi hatuna ajira, habari hii ni muhimu. Maana kila mmoja wetu lazima apate la kumzozea mama watoto wake kuwa umasikini wao si bure, kuna mkono wa mtu.
Baada ya kumaliza kikombe changu cha kahawa, nilitoka mbio kwenda kununua nakala ya gazeti la Tanzania Daima ili tuanze malumbano na mijadala juu ya jinai hii.
Kwa taarifa yako ni kwamba, kijiwe chetu ni sawa na Bunge. Kwani hujadili mada mbalimbali. Tofauti na Bunge, siye huwa hatukuchaguliwa, bali huletwa na ukosefu wa ajira. Ukipata ajira ubunge unakoma. Na mazungumzo yetu mara nyingi huwa hayaripotiwi magazetini hata kama tuna hoja.
Baada ya kurudi na gazeti. Nilizungukwa na wanakijiwe, angalau kila mmoja akijitahidi kuzipata habari zikiwa bado moto. Kitambo hiki kidogo kijiwe kilizingwa na kimya na tafakuri.
Mara sauti ya Mtukutu ikasikia: “We Pangu pakavu, lazima leo uwe mwenyekiti ili tujadili wizi huu na hizi nyumba zetu.”
Mara Mchunguliaji bila hata kupata amri ya mwenyekiti alidakia. “Hawa magabacholi wanaogawiwa uraia na wezi wetu watakuja kuuza hata wake zetu tusipoangalia.” Kabla ya kumaliza Mzee Kidevu alidakia na kumaka kwa ghadhabu: “Kijana chunga ulimi wako. Mke wa nani auzwe?”
Naye Mpayukaji hakungoja amalize kwani alimjibu. “Wauzwe mara ngapi? Hata kama wako hajauzwa, lakini watu wetu wengi wameishauzwa kwenye utumwa kama vile omba omba na kukopa kopa huku pesa zetu zikitoroshwa na magabacholi na wezi wenzao.”
Aliendelea: “Ukitaka kujua kama ameishauzwa au la nenda pale dukani anapokopa uulize kuaminiana kote kwasababishwa na nini?”
Kijiweni kuna mambo. Wakati mdahalo wa kuuzwa kwa watu ukiwa umesimama, Msema hovyo niliamua kuchokoza mada. Niliuliza kama yule Gabacholi atakamatwa na mali zake afanywe nini? Kabla sijamaliza nilisikia: “Afungwe hata kuuawa pamoja na hao wezi wetu wa nyumbani.”
Mkata tamaa, jamaa ambaye alihitimu chuo kikuu, lakini hakupata ajira, alikuwa amenyamaza akisoma gazeti ili aje achangie. Kila mtu hupenda kumsikiliza. Hivyo kabla hajachangia, tuliobaki ni kama tulikuwa tunapasha uwanja joto.
Mkata tamaa huyo kamaliza kubukua gazeti. Mara alianza kuchangia. “Pamoja na wenye nchi kutuzuga kwa kuahidi kurejesha nyumba za umma, tusijidanganye kwa kudhani kuwa ni rahisi kumnyang’anya paka maziwa uliyompa mwenyewe. Hivi ni nani hakugawiwa nyumba awe na ithibati ya kuzirejesha?” alikohoa kidogo akaendelea. “Kwa nijuavyo mie ni kwamba, wanakijiwe wote pale Dom walipewa ofa ya nyumba ili baadaye asipatikane wa kutoa ushahidi. Hebu nambie kama kuna hata mmoja aliyekataa kuchukua; sasa huyo wa kuzirejesha ni nani iwapo ni wale wale?”
Alivuta kikombe chake na kupiga funda moja mbili za kahawa na kuendelea. “Huyu Gabacholi mnamuonea. Kwani yeye ni kifaa tu anatumiwa, wenye chao wapo na saa nyingine ndiyo hao hao tunaowashinikiza wamkamate na kumtia adabu! Hapa ndipo unafiki wetu sie wananchi unapofichuka.
“Tuko tayari kumchoma moto kibaka huku tukiwaabudia na kuwasujudia mibaka. Kisa? Eti kwa vile wakati fulani tunatupiwa mabaki ya jinai yao na kupewa vibarua kwenye miradi yao michafu.”
Alipiga funda tena na kukatua kashata yake na kuendelea. “Ukitaka kujua kuwa kaya hii imekwisha na imelaaniwa, hebu jikumbushe mbwembwe na matusi ya Bwana Tunituni wakati tukilalama kupinga kununuliwa kwa mrada huu, alitutukana kuwa hatuna akili
na tuna wivu wa kike. Alituzuga na kuunda tume ya kupambana na ulaji halafu akainyonga baada ya kukuta kuwa ilitaka kuingilia ulaji wake.” Alikunywa kahawa yake na kuendelea: “Jikumbushe mbwembwe za juzi juzi juu ya kuwanasa vigogo wa bwimbwi. Yako wapi? Danganya toto bwana, hii ni Danganyika. Siku zinayoyoma na miaka itayoyoma na wahusika wataendelea kupeta. Jamani tukubali tunaliwa hata kama hatutaki. Hapa kinachoendelea ni usanii hamna jipya wala lolote.”
“Du!” Alisikika akimaka mzee Maneno ambaye alikuwa amekodoa macho akimsikiliza Mkata tamaa.
Mkata tamaa aliendelea kula Mic kama wasemavyo: “Leo kwa mfano mtu atakwambia upeleke taarifa kwenye taasisi ya kuzuia vijirushwa (TAKUVI). Kama kuna mama wa rushwa hii ndiyo yenyewe. Hebu watazame maofisa wake. Wengi tumesoma nao. Licha
Ya kuwa wezi wa peni walifeli. Wameajiriwa pale wakiwa wamekonda kama ng’onda, hebu kawatazame leo walivyo na viriba tumbo, misimu ya bei mbaya mavazi aghali. Wanapata wapi kama siyo kula rushwa waliyoajiriwa kuizuia?” Alikohoa na kuendelea:
“Watazame walivyonenepeana kama mapaka ya dukani kwa Mwarabu. Wanavaa saa za bei mbaya na kula kwenye mahoteli ya hali ya juu. Yote hii ni danganya toto ndugu zangu. Remi alisema wizi ndani ya wizi hatukumuelewa. Mchungaji alionya kuhusu kuchezewa uraia na mali yetu hatukumuelewa. Sijui tutamuelewa nani?” Alimalizia na kufuatiwa na makofi mengi tu na ofa nyingi za kahawa.
Kwa ufupi hizo ndizo taarifa toka kijiweni sehemu yetu muhimu ya kupotezea muda na kujifunza kuishi kwa matumaini.
Muhimu ni kukubali kuwa wanakijiwe nao ni raia wetu na wana hoja na wanapaswa kusikilizwa. Sisi letu ni kuwafikishia ujumbe wao kwa wananchi wenzao. Je, nyumba zetu kweli zitarudishwa au tumezugwa kama wanakijiwe tunavyodhani? Je, huyu gabacholi aliyekiri kuponyoa mabilioni yetu tutamkamata au kila mtu atajitenga kusema ahusiki? Sasa nani anahusika? Kwanini asibanwe mbavu akawataja washirika wake waliomo kwenye maofisi yetu?
Je, vita dhidi ya vigogo wa mihadharati ni kweli au? Wanakijiwe tunahisi ni nguvu ya soda, tena danganya toto. Je, kaya haina mwenyewe kiasi kugeuka chaka la kuzalia mipanya na mijoka? Mwenye macho haambiwi tazama. Tukutane kwenye maandamano ya kupinga kuibiwa mali zetu.
Wenu Mpayukaji mwana wa Msema hovyo.