MOJA ya habari zilizochapishwa katika ukurasa wa mbele wa gazeti hili leo, inahusu nia ya Serikali kuharakisha kuupeleka bungeni muswada wa sheria mpya ya rushwa.
Muswada huo unatarajiwa kujadiliwa na wabunge katika kikao kijacho cha Bunge, kinachotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Taarifa ya serikali iliyotolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, ilieleza kuwam serikali imedhamiria kuuharakisha muswada huo, ili upitishwe kuwa sheria, ambayo itaanza kutumika mwaka ujao wa fedha, 2007/2008.
Serikali imeuelezea muswada huo kuwa utasaidia kupanua uwezo wa uchunguzi, upelelezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Kwamba mambo mengine yaliyomo katika muswada huo ni kuanzishwa kwa Bodi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, badala ya Kamati ya Udhibiti na Tathmini iliyokuwa chini ya sheria namba 16 ya mwaka 1971, iliyounda Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini (TAKURU).
Lakini, serikali ambayo awali ilikuwa ikisuasua kuhusu muswada huo, imetahadharisha kuwa, mabadiliko ya haraka ya sheria ya rushwa, hayana msukumo wowote kutoka nje, bali ni nia yake ya dhati ya kutaka kufanyia marekebisho sheria hiyo ili itoe matokeo yanayokusudiwa.
Maelezo yaliyotolewa na serikali kama ni ya dhati, yanatia moyo na kutoa matumaini, lakini mabadiliko ya muundo na baadhi ya vipengele kwenye sheria hiyo peke yake, haviwezi kuwatia matumaini wananchi kama kweli tatizo hilo sugu, linaweza kuondolewa kwenye jamii.
Serikali inaposema ina nia ya kupanua uwezo wa TAKURU ili iweze kufanya uchunguzi na upelelezi katika masuala yanayohusu rushwa, inaonyesha walakini wa nguvu ya taasisi hiyo.
Hivyo, wananchi wanachotegemea ni mabadiliko, wanataka kuona nguvu ya TAKURU katika kupambana rushwa kubwa kubwa, ambazo taasisi nyingine za usalama za serikali, zimeshindwa hata kuwanyooshea kidole wahusika.
Hapa tunapenda kuikumbusha serikali kuwa, wananchi hawajali kama uharakishwaji wa muswada huo ni msukumo wa mataifa kutoka nje au la, wanachotaka kuona ni dhamira ya kweli ya serikali katika kupambana na rushwa.
Watanzania wamekwishashuhudia mabadiliko mengi yaliyofanywa katika taasisi hii, ikiwemo kupanuliwa kwa kuongezwa idadi ya watumishi wa kada mbalimbali, vifaa na ofisi, ambazo sasa zimesambaa mpaka katika ngazi za wilaya.
Hata hivyo, mabadiliko hayo yamekuwa na matokeo butu, ambayo yamewafanya walio wengi kuvunjika moyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa watumishi, ambao wamekuwa waoga kushughulikia rushwa kubwa kubwa zinazowahusu vigogo.
Serikali inapaswa kutambua kuwa, dhamira yake ya kweli kupambana na rushwa, haitafanikiwa kwa kubadilisha muundo wa TAKURU, na kuongeza makosa yanayopaswa kushughulikiwa, bali kinachotakiwa ni utashi wa dhati katika mapambano ya udhalimu huo unaoliangamiza taifa.
Na kwa watendaji wa TAKURU, nao tunawaambia shime, serikali imeonyesha nia ya kufanya mabadiliko hayo adhimu, nyinyi kama kiungo muhimu mchukue jukumu hilo kama wana wa Tanzania mliovishwa jukumu hilo kubwa, mvae sura ya ujasiri na mtende yale Watanzania wanayotarajia