MASIKIO ya Watanzania leo yanaelekezwa mjini hapa ambako Serikali ya Awamu ya Nne, kwa mara ya kwanza, inasoma bajeti yake ya mwaka 2006/2007.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu asubuhi, Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa, atasoma mweleko wa uchumi wa taifa.
Jioni, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, atakuwa mwanamke wa kwanza, kwenye wadhifa huo katika historia ya Tanzania , kusoma Bajeti ya Serikali.
Baadhi ya wachunguzi waliozungumza na Tanzania Daima , walisema bajeti Ilikuwa imelenga kuwapa faraja Watanzania, lakini imekuwa vigumu kutokana na mambo kadhaa mazito yaliyolikumba taifa.
Baadhi ya mambo hayo ni baa la njaa ambalo limeigharimu serikali mabilioni ya shilingi katika kuwahudumia wananchi, ambako serikali inaendelea kupigana na baa hilo , matarajio yakiwa mazuri kulishinda.
Mgawo wa umeme ni jambo jingine lililoifanya serikali iwe katika wakati mgumu. Uzalishaji unatarajiwa kuzorota, huku fedha nyingi zikitumika kununua mafuta.
Kupanda kwa bei ya mafuta ni pigo jingine ambalo Serikali ya Awamu ya Nne ilikumbana nalo muda mfupi baada ya kuingia madarakani. Kupanda kwa bei ya mafuta na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi, kunaifanya serikali ikune kichwa zaidi.
Vita dhidi ya uhalifu nchini, hasa ujambazi, imeifanya serikali itumie fedha nyingi kuhakikisha inakuwa na Jeshi la Polisi lenye wataalam mahiri na kuwa na nyenzo za kisasa.
Mahitaji ya fedha zote hizo yanakuja huku Watanzania wakiwa na shauku kubwa ya kuanza kuona utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya mwaka 2005-2010.
Ujenzi wa barabara, huduma za maji safi na salama, mawasiliano ya simu, afya, elimu na vita dhidi ya umaskini, ni mambo ambayo Watanzania wanataka kuona yakirekebishwa.
Kwa vyovyote iwavyo, bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne inasubiriwa kwa shauku kubwa.
Nchi za Kenya na Uganda nazo zinatarajiwa kutangaza bajeti zao. Kenya iko katika msuguano wa wanasiasa wakuu, wakiwania madaraka, ikiteswa pia na ukame, wakati Uganda, Rais Yoweri Museveni aliyefanikiwa kuongeza muhula wa uongozi, bado anakabiliwa na changamoto ya mapigano dhidi ya genge la Lord's Resistance Army (LRA)