Na Samuel Msuya, Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Meja Jenerali Mstaafu, Said Kalembo amekiri kuwa hali ya elimu mkoani kwake ni mbaya, na kuwahimiza madiwani kuwahamasisha wananchi kukamilisha ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari kabla ya machi 15, mwaka huu.
Kauli ya mkuu wa mkoa imetolewa siku chache baada ya kumuahidi Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuwa mkoa utakamilisha ujenzi wa madarasa ifikapo Machi 15, ili kuwawezesha watoto wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana kupata nafasi ya kujiunga kidato cha nne
Wito huo ulitolewa jana mjini hapa katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, ambapo alisisitiza kuwa viongozi wote kuanzia ngazi ya wenyeviti wa vijiji, watendaji, waratibu wa kata na madiwani wawajibike kufanya kazi hiyo.
Amewataka viongozi hao kuwa na uchungu na elimu huku akisisitiza kwamba, madiwani wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa ujenzi wa sekondari za kata unakamilika kabla ya Machi 13.
Awali Meya wa manispaa hiyo, Profesa Romanus Ishengoma, alisema katika kukabiliana na jambo hilo, manispaa yake hadi kufikia Machi 15 itakuwa imeshakamilisha ujenzi wa shule nne za sekondari.
Profesa Ishengoma alisema mbali na kukamilisha shule hizo nne pia manispaa hiyo inatarajia kuongeza mikondo katika shule zake nane za sekondari, ili ziweze kuwachukua wanafunzi hao waliokosa nafasi kutokana na uhaba wa madarasa.
Aliongeza kuwa manispaa hiyo kwa sasa imeweka kipaumbele katika ujenzi wa shule hizo na kwamba, imesimamisha masuala mengine ili kufanikisha utekelezaji huo.
Meya huyo aliongeza kuwa endapo mipango hiyo itakamilika kwa wakati, manispaa hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua asilimia 77 ya watoto waliofaulu badala ya asilimia 70 ya awali