Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Edward Lowassa, ameushangaa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa pamoja na kuwa na shule nyingi za sekondari, kuna wanafunzi wengi waliofaulu darasa la saba lakini wakakosa nafasi ya kuingia katika shule hizo mwaka huu.
Alikuwa akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro na wilaya zake ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa mikutano yake na mikoa kujadili mikakati ya kuwaingiza sekondari wanafunzi wengi waliofaulu mtihani wa darasa la saba.
Mkoa wa Kilimanjaro una shule ya sekondari katika kila kata, na kata nyingine zaidi ya shule moja, lakini umeingiza sekondari mwaka huu wanafunzi 17,170 ambao ni asilimia 47 tu ya wanafunzi 36,839 waliiofaulu na kuwaacha wengine 19,669 ambao ni sawa na asilimia 51, Waziri Mkuu alisema.
Maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete ni kwamba angalau asilimia 75 ya waliofaulu darasa la saba wawe wameingia sekondari za serikali katika awamu ya kwanza ya Januari na ya pili kabla ya Machi 15, mwaka huu.
Waziri Mkuu Lowassa alisema: “Nawashangaa kwa sababu ninyi Kilimanjaro mna shule nyingi za sekondari na mmefaulisha wananafunzi wengi mtihani wa darasa la saba…itabidi mjenge madarasa mengi zaidi na kwa kasi ili kuwaingiza wote waliofaulu kabla ya muda kupita”.
Katika mkutano huo, alisema hakuridhishwa na baadhi ya wilaya, hasa Moshi Mjini, Moshi Vijijini na Rombo kwa kuwa shule mpya zilizopangwa kujengwa kwa ajili ya kuwachukua waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza ili wachukuliwe awamu ya pili, bado majengo yake hayajaanza kujengwa.
Miongioni mwa sababu zilizotolewa kwa uchelewaji huo ni uhaba wa ardhi na kukosa viwanja vya kujenga shule, lakini Waziri Mkuu alisema kama wangejipanga vizuri mapema, wangeweza kupata viwanja kwa wakati.
“Sababu hizo sizikubali, kwa kuwa kila wilaya ina matatizo yake, lakini ni wajibu kukabiliana nayo na kuyatatua mapema…kazi hii ya kuwapeleka wote waliofaulu kuingia sekondari lazima itekelezwe bila ya visingizio,” alisisitiza.
Mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya mikoa 10 kati ya 21 ya Tanzania Bara ambayo imeitwa kujieleza kwa Waziri Mkuu kwa kushindwa kutekeleza maelekezo ya Rais Kikwete ya kuwapeleka sekondari wanafunzi wengi zaidi waliofaulu darasa la saba.