Kwani wanaishi kwenye stoo iliyojaa mabomu na milipuko aina aina. Hebu soma safu hii.
Ukikiliza kisa kizima cha tukio lililotokea mwishoni mwa mwaka jana kuhusu wananchi wa Vijibweni huko Kigamboni kupinga ujenzi wa mradi wa gesi,kama huzingatii unaweza kuchukulia suala hili kama suala dogo la kawaida na la kupita.
Kwa haraka haraka ni kwamba wananchi wa Vijibweni walikutana na mwekezaji na kumwambia wazi wazi kuwa hawako tayari kumruhusu ajenge miundo mbinu ya mradi wake. Maana ni kuwatia hatarini iwapo lolote litatokea.
Kwa safu hii suala la wananchi wa vijibweni kujua madhara ya gesi na kuachana na tamaa za kuhongwa na ahadi za maendeleo ni somo kubwa kwa wananchi wengine na watawala kwa ujumla. Pia kisa hiki kwa safu hii ni stori kubwa kuliko hata ule ushenzi na unyama wa kujazana matumboni unga tena kwenye maiti! Kisa eti kupata vimilioni 26!
Turejee kwenye jinai waliyoigundua na kukataliwa wananchi wa Vijibweni pamoja na muhusika kujibaraguza kuwa ana vibali vyote. Kwanza vibali ni nini kama havizingatii haki na thamani ya binadamu? Mwambie mhusika atofautishe thamani ya maisha ya mtanzania ni tofauti na India ambapo mfumo wa caste umezalisha watu ambao thamani yao ni ndogo kuliko hata paka.
Pia kitendo cha Vijibweni kama watawala mtazinduka mkakifanyia kazi kinatoa fursa mpya ya kujua jinsi ya kupanga utekelezaji wa sera zao za uwekezaji. Kwanini?
Hebu piga picha ya eneo la Keko Mwanga kwenda hadi kule Kurasini. Ni ajabu kuwa sehemu ya viwanda imekaliwa na watu na viwanda, Hebu tujalie kuwa tanki moja au mawili ya mafuta pale Kurasini au hata pale Keko Mwanga limelipuka, kitakachofuata ni msiba ambao Tanzania haijawahi kuushuhudia.
Bahati nzuri safu hii inakumbuka kipindi fulani miaka ya 1999 mwekezaji mmoja mwenye asili ya kiasia alivyokuwa anawasumbua wananchi wa maeneo ya Keko Mwanga baada ya kuwa amewatia mfukoni baadhi ya watendaji kiasi cha kuruhusu mradi licha ya kuwa hatari kwa watu pia ni hatari kwa mazingira. Kwa bahati mbaya kutokana na ubabe na mtandao uliokuwepo wakati ule,safu hii iliishia kutimkia kwenye shughuli zake nje ya wigo mzima wa Dar es Salaam kiasi cha kushindwa kuendelea kushupalia suala hili.
Nini somo kubwa tunalopata kuhusiana na uwezo mkubwa wa wananchi wa Vijibweni? Kwanza kukengeuka huku kuwe ni taarifa ya ukumbusho kwako na serikali kuwa kama kweli unataka kuwafikisha watanzania salama kule "Kanani" na watu wa maeneo ya Kurasini na Keko Mwanga wakiwemo, basi tuamue moja au wananchi wa maeneo hayo wahamishwe au viwanda vya mafuta na matenki yake vihamishwe.
Tuseme bila kumung'unya maneno kuwa hapa anayeweza kuhamishika kirahisi ni Wananchi. Kwani hata msiba ukitokea watakao athirika zaidi ni wao maana hata wenye viwanda na matenki hawaishi hapo. Pia viwanda na matenki yamelipiwa bima tofauti na wao ambao hawana bima hata kama wangekuwa nayo kulipwa fidia kwa watakaowaacha kwaweza kuchukua vizazi kama siyo karne nyingi.
Kama serikali inataka usalama wa wananchi wake, tungeishauri haraka iwahamishe watu hawa vinginevyo tusilaumiwe litakapotokea la kutokea hasa ikizingatiwa kuwa siku hizi watu wamezidisha vichwa ngumu. Mfano kuna watu pale Keko wanafahamika kwa mchezo wao wa kwenda baharini kuiba mafuta.
Kadiri uingiaji wa bandarini unavyozidi kuwa mugumu kuna siku watu hawa wachache na waroho kama watendaji waliofumbia macho jinai ya watu na viwanda kuishi eneo moja,watakuja kujaribu kuiba mafuta kwa kutoboa mabomba yaliyopo maeneo ya karibu na matenki. Hatuichulii nchi yetu lakini tuna uhakika kuwa hili ni jambo ambalo huwezi kuuliza kama litatokea bali litatokea lini.
Kwa bahati mbaya zaidi hali ya watu kuishi kwa kukalia mabomu siyo maeneo tajwa hapo juu bali ukifanya uchunguzi wa kina unabaki kushangaa. Hebu kwa mfano angalia kile kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kula kilichogundulika kuwa kilikuwa kinaiba maji ya DAWASA. Kipo katikati ya makazi ya watu pale Ubungo nyuma ya TANESCO. Hebu angalia hata maeneo ya Kipawa viwanda vinavyozidi kuwavamia watu. Hatujui hapa nani anamvamia nani watu wanavamia viwanda au viwanda vinawavamia watu?
Nenda mbele. Angalia kiwanda kama vile Karibu. Kimevamia watu wa Mbagala na kinachafua mazingira kwenye mto Kizinga ambao ni sehemu mojawapo ya mapafu ya jiji la Dar es salaam ambayo yakiendelea kuchafuliwa na kuzibwa Dar itakumbwa na mafuriko kisa eti watu wachache waroho wanataka kuchuma pesa.
Kimsingi hapa inabidi wasimamizi wa sera na sheria wawe macho. Kitendo na mazoea ya wananchi kujichukulia maeneno na kujenga au watendaji kugawa maeneo kwa wawekezaji bila kujali upembuzi na mpambanuo wa nani anapaswa kujenga wapi,kuna siku tutakuja kuamkia kwenye msiba ambao hatutausahau.
Juzi safu hii ilikumbushia juu ya vituo vya mafuta katikati ya makazi ya watu. Leo tunakumbushia juu ya kadhia hii ambayo kwa kila mwenye kuona mbali ni zaidi hata ya bomu maana bomu huweza kuteguliwa na uhatarisha sehemu ndogo.
Kuna haja ya kuwa na sehemu zamani zilokuwa zikujulikana kama viwandani. Hizi ni sehemu maalum kwa viwanda. Hakuna anayeruhusiwa kujenga wala kuishi eneo hili kama ambavyo na kwa viwanda haviruhusiwi kujengwa kwenye makazi ya watu kama mifano tuliyoona pale Ubungo.
Hebu tuhitimishe kwa kunukuu maneno ya mwekezaji na watoaji wa vibali vya uwekezaji. Ukisoma kwa kina unagundua kuwa kwa mwekezaji kinachoingia akilini ni kuwa na kibali hata kama ni kujenga juu ya kaburi. Mwekezaji kama huyu ana kila dalili za baadaye kuwa bomu.
"Mimi si kwamba nimevamia eneo hili bali nimefuata taratibu zote za uwekezaji nchini Tanzania na ninavyo vibali vyote vinavyoniruhusu kuendelea na uwekezaji huu," alisisitiza na kuongeza: "Itakuwa ni jambo la kushangaza kama vibali nilivyopewa vitakuwa si halali kwa sababu tangu nimeanza kufuatilia vibali hivi imenichukua karibu mwaka mzima, mimi nafuata sheria za nchi."
Baadhi ya vibali hivyo ni vile vya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Manispaa ya Temeke, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi pamoja na kibali cha Msaidizi wa Msajili wa Makampuni. Alipoulizwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel ole Naiko, alikiri kutoa kibali kwa mwekezaji huyo lakini akaahidi kutoa ufafanuzi zaidi atakaporudi kwa kuwa sasa yuko nje ya nchi.
"Ni kweli tulitoa kibali kwa mwekezaji huyo lakini mimi niko India narudi kesho (leo) hivyo nitaweza kutoa ufafanuzi zaidi," alisema ole Naiko kwa njia ya simu. Vyanzo vya habari vilishuhudia mitungi mitano kwa ajili ya kuhifadhia gesi hiyo ikiwa tayari imeshawekwa katika eneo hilo huku ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji ambayo yatatumika endapo itatokea hatari ya gesi kulipuka, ukiendelea.
Kituko kingine na cha mwaka, tangu lini maji yakatumika kuzimia gesi tena kutoka kwenye bwawa?