Na Mwandishi Wetu, Arusha
WAFANYAKAZI wawili waliokuwa watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha wanashikiliwa na polisi na wengine saba, akiwamo aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wanatafutwa ili wahojiwe kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa Sh36,950,000 za Manispaa hiyo.
Mbali na wafanyakazi hao, pia yuko mkurugenzi wa kampuni moja ya ukandarasi ya mjini hapa ambayo ilipewa zabuni ya kutengeneza barabara katika Manispaa ya Arusha.
Mpaka kufikia jana mchana watumishi wawili na mkandarasi huyo tu ndiyo waliokuwa wanashikiliwa na kuhojiwa kuhusiana tuhuma hizo wakati wengine saba walikuwa hawajapatikana.
Kamanda wa Polsi Mkoa wa Arusha, Balisilio Matei, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watumishi wanaotuhumiwa kuhusika na upotevu wa fedha hizo ni kutoka idara za Mipango Miji, Hazina, Uhasibu, Ujenzi, Ugavi, Uhandisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa.
Kwa mujibu wa Kamanda Basilio, miongoni mwa watuhumiwa hao wamo wahasibu wanne, mhandisi, mweka hazina, afisa ugavi na afisa mmoja wa idara ya ujenzi, baadhi yao wakiwa tayari wamehamia katika mikoa mingine.
Kamanda Matei alikataa kutaja majina ya watumishi kwa madai kuwa upelelezi upo katika hatua za mwanzo kabisa na kwa kufanya hivyo kunaweza kuharibu mwenendo wa upelelezi wa kesi hiyo.
Akizungumzia juu ya watumishi waliohamishiwa mikoa mingine nchini, Basilio alidai kuwa taarifa zimekwisha kutumwa katika sehemu walizohamishiwa watumishi hao ili waweze kukamatwa na kuletwa Arusha kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma hizo kabla ya kufikishwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake.
Kashfa ya upotevu wa fedha hizo zilitolewa katika kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Arusha cha Januari 5, mwaka huu.
Katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Engutoto, Alfred Kimani, alidai kuwa fedha hizo zilichotwa na kulipwa mkandarasi ambaye hata hivyo hakufanya kazi iliyokusudiwa.
Diwani huyo alisema kilichomshangaza ni mkandarasi huyo kusaini mkataba wa ujenzi siku hiyo, kupewa cheti na kulipwa fedha zote kwa siku moja kinyume cha utaratibu wa kawaida, ambao mtu au kampuni inayoshinda zabuni hulipwa baada ya kazi kukamilika au kulipwa pesa nusu kabla ya kuanza.
Hata hivyo, mkurugenzi wa kampuni hiyo ya ukandarasi siku mbili baada ya kikao cha madiwani, aliita kikao na waandishi wa habari na kukanusha tuhuma hizo na kusema bado alikuwa anadai Sh17 milioni.
"Mimi kweli nilikuwa nadai fedha hizo tu nyingine zote nilipewa, sasa anayedai kuwa nimepokea aonyeshe ushahidi...kawaulizeni mimi nasema sijapokea malipo hayo, unapopokea hundi manispaa huwa kuna daftari la kusaini na huwa mimi na meneja wangu ndio huwa tunaenda kupokea hundi yoyote, sisi hatujaenda ... fuatilieni nani kachukua hundi hiyo," alisema mkurugenzi wa kampuni hiyo ya ukandarasi.
Hii ni hatua mpya kuwahi kuchukuliwa na serikali katika siku za hivi karibuni katika kupambana na ubadhirifu wa mali ya umma.
Jumatatu wiki hii katika ukurasa wa mbele wa gazeti hili tulimkariri Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, Mizengo Pinda, akisema kwamba wameamua kuondoa kesi zilizokuwa zimefikishwa mahakamani dhidi ya maafisa wa halmashauri nchini, kutokana na mlolongo wa urasimu mahakamani.
Badala yake, serikali imeamua kutumia taratibu za kiutumishi kuwashughulikia watuhumiwa wa ubadhirifu ili kuweza kumaliza kesi zao kwa haraka ili kutoa nafasi hatua nyingine za kiutendaji kuchukuliwa.
Mionongoni mwa hatua kiutumishi zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya maofisa hao ni pamoja na kuhamishwa vituo vya kazi, kushushwa vyeo, kusimamishwa kazi au kufukuzwa kazi. Hatua zitakazosaidia kuajiri watumishi wengine.
Hata hivyo, Waziri Pinda alisema kwamba hatua za kimahakama zinaweza kuchukuliwa dhidi ya watumishi hao baada ya kukamilika za kiutumishi.