Na Aloyce Geofrey
WAZIRI Mkuu Edward Lowassa, amelitaka Kanisa kuyaelekeza mataifa yaliyoendelea, taasisi za fedha za kimataifa na taasisi za kibiashara kuhakikisha Afrika inanufaika na rasilimali zake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 14 la Uinjilishaji wa Jumuisho la Mabaraza ya Maaskofu ya Afrika na Madagascar, Lowassa alisema: “Kwa kulisaidia bara la Afrika kunufaika na utajiri wake mwingi ilionao, mtakuwa mmetimiza maneno matakatifu ya biblia.”
Lowasa alisema Kanisa kama familia ya Mungu lazima lionyeshe ushuhuda kwa kukuza haki, amani na usalama kwa Afrika na duniani kote.
Alisema kumekuwa na marekebisho kadhaa kwa bara la Afrika katika miongo miwili iliyopita. Alisema kuwa Afrika imefanya jitihada za makusudi za kurekebisha uchumi, siasa na jamii katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili bara zima.
“Marekebisho hayo yamejumuisha mapinduzi ya biashara, siasa, ubinafsishaji, vyama vingi vya siasa na masuala ya soko kwa ujumla,” alisema.
Kuhusu mataifa makubwa kusaidia Afrika kunufaika na rasilimali zake, alisema ni vizuri kutambua kuwa Afrika imebarikiwa kwa kuwa na maliasili nyingi, ardhi kubwa na bora, na hali ya hewa nzuri, hivyo inahitaji inufaike nazo badala ya kunufaisha wageni tu.
Hata hivyo, Lowassa alisema licha ya kuwa na mambo hayo yote, inakera kuona kuwa Waafrika wanaishi chini ya dola moja kwa siku ikilinganishwa na ziada ya takribani dola za Marekani 2.5 zitolewazo kwa ng’ombe Ulaya na Marekani.
“Hali kama hii si ya kiutu, ni kinyume na maadili na haikubaliki kabisa kiutu katika jamii,” alisema.
Lowasa alisisitiza kanisa kuchangia katika kudumisha amani, haki, na usalama kwani ni wazi kuwa, pasipokuwa na mambo hayo matatu maendeleo ni vigumu kupatikana.