Premi Kibanga, London, Uingereza
MCHANGO wa serikali ya Uingereza katika bajeti ya Tanzania mwakani utaongezeka kutoka paundi 90 milioni za mwaka huu hadi paundi 105 milioni ili kusaidia juhudi za serikali katika kupunguza umaskini kwa wananchi wa Tanzania.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingerezai, Hilary Benn, alisema hayo jana baada ya mkutano wake na Rais Kikwete na pia kutangaza azma hiyo wakati wa mhadhara kuhusu Maendeleo ya Afrika juu ya Marekebisho ya Sekta ya Utumishi wa Umma.
“Afrika inamudu kujifanyia marekebisho ikidhamiria, demokrasia inatendeka, uchumi unakuwa, Tanzania ni ishara nzuri ya mategemeo barani Afrika na hasa katika nchi zilizo usini mwa Sahara, imeonyesha mfano, na imedhihirisha kuwa mageuzi makubwa...napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza kwa hilo,” Benn alimwambia Rais Jakaya Kikwete mara baada ya Rais kutoa mhadhara katika jumba la mikutano la Chattam, jijini London.
Benn aliyataja mafanikio ya Tanzania kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya watoto waliojiandikisha katika shule za msingi kuongezeka maradufu kutoka milioni 4 mwaka 2000 hadi milioni 8 hivi sasa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 96, kukua kwa pato la Taifa na uchumi kwa ujumla kutoka asilimia 5 tangu mwaka 2000 hadi asilimia 7 kwa sasa na kupungua kwa vifo vya watoto wachanga katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mapema katika Mhadhara kususu marekebisho ya utumishi serikalini, Rais Kikwete alisema Tanzania inafanya marekebisho kwa nia ya kuleta mawazo mapya, malipo mazuri na hatimaye kumpatia mtumishi wa umma maslahi mazuri yenye kutia ari na nguvu katika kufanya kazi.
Alisema tayari tume ya kuangalia upya maslahi ya watumishi wa umma imeshakamilisha kazi yake na serikali itaanza kuyatafakari mapendekezo yake, na kuwa ana uhakika kwamba mapendekezo hayo yatatumika katika maamuzi..
“Marekebisho haya ya utumishi wa umma yanahusishwa sana na juhudi za serikali kuondoa umaskini na pia yanahusishwa katika sekta zingine mbalimbali za serikalini” Rais amesema.
Mhadhara huo ulihudhuriwa na wanasiasa, wafanyabiashara, wasomi, watafiti na mabalozi kutoka sehemu mbalimbali Afrika na Ulaya ambao walipata nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa na Kikwete.
Rais aliwasihi Waafrika walioko ulaya kushiriki ipasavyo katika kuleta maendeleo na kuondosha umaskini barani Afrika kwa kuunganisha nguvu na mitaji yenye lengo la kuweka vitega uchumi barani.
“Wito wangu kwa Waafrika wote nje ya bara letu, mkusanye raslimali kwa nia ya kuendeleza Afrika kwani hata wao pia tunawahitaji na ni wenza katika maendeleo na kuondosha umaskini," alisema.
Mapema kabla ya kutoa mhadhara katika jumba la Chatam, Rais Kikwete alizungumza na wafanyabiashara wa Uingereza, hususan kwenye sekta ya Fedha na kuwahimiza kuleta vitega uchumi na kuwekeza Tanzania.
Akizungumza katika katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa kwa ajili yake na Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (BTS), Kikwete alisema Tanzania imejizatiti kupandisha uchumi wake, licha ya uchumi huo kushuka kufuatia majanga ya asili yaliyolikumba taifa mwaka jana.
Alisema uchumi wa Tanzania ulishuka mwaka jana lakini sasa mvua zilizonyesha zinaonyesha nuru mpya katika uzalishaji wa chakula na akaongeza kuwa, jitihada za kuandikisha wanafunzi wengi katika shule za msingi na sekondari zinzonyesha mafanikio makubwa hali inayoashiria ishara njema ya maendeleo ambayo serikali yake imepanga kuwapatia wananchi.
"Nilipoingia madarakani kulikuwa na wanafunzi 150,000 katika mashule ya sekondari. Tuliweka masisitizo mkubwa na kuweza kuongeza idadi hiyo hadi 234,000 katika miezi sita. Mwaka huu tunatarajia idadi hiyo kufikia 350,000," alisema.
Rais Kikwete alisema pia kuwa, serikali yake iko katika uchambuzi wa tatizo la umeme ili kuligeuza historia baada ya tatizo hilo kuathiri uchumi kwa kiasi kikubwa hapa nchini mwaka jana.
BTS imekuwa ikiichangia Tanzania katika sekta mbalimbali hasa elimu na afya na rais ameiomba jumuiya hii kusaidia katika kusaka walimu wa kujitolea kutoka Uingereza kuja nchini kufundisha hasa kipindi hiki ambapo kuna ongezeko la shule huku uwiano wake ukiwa haufanani na idadi ya walimu waliopo.