Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Khatib aishauri TFF kuzifuta Simba, Yanga
http://www.habaritanzania.com/articles/26/1/Khatib-aishauri-TFF-kuzifuta-Simba,-Yanga
By Habari Tanzania
Published on 05/14/2006
 
Serikali imeliagiza Shirikisho la Soka, TFF, kuziondoa kwenye orodha ya wanachama wake klabu za Simba na Yanga endapo hazifanya marekebisho ya katiba zake ili zifanane na ya shirikisho hilo.

Serikali imeliagiza Shirikisho la Soka, TFF, kuziondoa kwenye orodha ya wanachama wake klabu za Simba na Yanga endapo hazifanya marekebisho ya katiba zake ili zifanane na ya shirikisho hilo.
 
Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Muhammed Seif Khatib alipokutana na uongozi wa TFF kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea wa kukutana na kamati za utendaji za vyama vya ngazi ya kitaifa.
 
Khatib alisema katiba ya TFF ifanane na za wanachama wake wote, bila kuogopa majina ya klabu kubwa za Simba na Yanga, na mwanachama asiyetaka basi aondolewe katika orodha.
 
’’Hivi nyie mnaziogopa hizi Simba na Yanga? Kwa nini wao katiba zao zipo tofauti na yenu kabisa?’’ alihoji Khatib.
Alisema endapo katiba zote zitafanana itakuwa rahisi kumwadhibu mwanachama ambaye atakwenda kinyume na katiba hiyo, lakini kwa sasa haiwezekani kutokana na kila mmoja kutumia katiba yake.
 
Hatahivyo, akijibu hoja ya waziri rais wa TFF, Leodger Tenga alisema shirikisho lake haliziogopi klabu hiyo, ila baada ya kukamilika kwa marekebisho ya katiba ya TFF, sasa wanachama wamepewa hadi mwishoni mwa mwaka huu kukamilisha marekebisho ya katiba zao na klabu itakayoshindwa kufanya hivyo itafutwa kwenye uanachama.
 
Tenga alisema wanachama wake ni vyama vyote vya mikoa, klabu zote za ligi kuu ya Bara zikiwemo Simba na Yanga, chama cha makocha, TAFCA, chama cha waamuzi, FRAT, chama cha tiba michezoni, TASMA, na cha wachezaji wa zamani, SPUTANZA.
 
Awali Khatib aliibana TFF ieleze jinsi wanavyotumia shilingi milioni 26 kwa mwezi, baada ya kuwasilisha ombi la kuondolewa makato ya Baraza la Michezo la Taifa, BMT, ambayo yanatokana na mapato ya mechi za ligi kuu.
 
’’Sio kwamba ninawachimba ila mnaonekana ninyi fedha zote hizi mnazitumia kwa kuendeshea shughuli za ofisi pekee badala ya pia kusukuma programu yenu ya maendeleo ya soka,’’ alisema Khatib.
 
Tenga alisema fedha hizo zinatumika kulipia huduma ya simu, fax, mishahara ya wafanyakazi na vikao vya kamati za rufaa, nidhamu, utendaji na vikao vingine vya shirikisho hilo.
 
Hata hivyo, Khatib aliwapa majukumu TFF kuhakikisha kunaanzishwa chama cha soka cha vijana wadogo, ambacho kitakwenda sambamba na cha wanawake, na kuwe na mashindano yao ili kusaidia kuongeza chachu ya maendeleo ya soka nchini.
 
Pia aliwashauri kuwa na kitega uchumi, mfano kujenga hoteli au kutengeneza jezi za timu ya taifa ambazo zitakuwa zikiuzwa na fedha kutumika katika kuendeleza soka na sio kutegemea wafadhili wachache ambao wanajitokeza sasa.
 
SOURCE: Lete Raha