Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mtanzania aliyeyatafuna mabilioni ya rada atajwa
Mtanzania aliyeyatafuna mabilioni ya rada atajwa
By Habari Tanzania | Published  01/16/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

MTANZANIA aliyepokea mamilioni ya dola za Marekani kama kamisheni ya ununuzi wa rada, ametajwa.

Taarifa iliyoandikwa na gazeti moja la jijini London, Uingereza jana, zinaeleza kuwa, Kampuni kubwa ya usambazaji wa silaha nchini Uingereza, BAE System, inatuhumiwa kulipa kwa siri kamisheni ya dola milioni 12 (zaidi ya sh bilioni 14) kwenda akaunti moja ya Mtanzania, iliyoko Uswisi.

Kamisheni hiyo iliifanya Tanzania, moja ya nchi maskini zaidi duniani, inunue rada ghali ya kijeshi katika mazingira yenye utata.

Gazeti hilo linasema kuwa, kinara wa kashfa hii kwa upande wa Tanzania, ambaye kwa muda mrefu ana uhusiano wa masuala ya kijeshi na viongozi wa serikali, amekiri kwamba kiwango hicho cha fedha kilihamishwa katika akaunti yake iliyoko Uswisi, uhamisho uliofanywa na kampuni hiyo, ambayo inafanyiwa uchunguzi wa Ofisi ya Uchunguzi wa Rushwa Mbaya (SFO).

Mlango huo wa nyuma wa malipo hayo unawakilisha asilimia 30 ya thamani ya mkataba huo.

Taifa hili la Afrika Mashariki lilibidi kukopa fedha ili liweze kuingia mkataba wa ununuzi, ambao wakosoaji wanasema kwamba, haukuwa na lazima na ulikuwa ghali mno.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, mwaka 2002 aliunga mkono kwa nguvu mauzo hayo ya rada, lakini aliyekuwa mmoja wa mawaziri katika serikali yake, Clare Short, anasema kwamba yeye na Waziri wa Fedha, Gordon Brown, waliupinga.

SFO, ambayo hivi karibuni ililazimishwa kuachana na uchunguzi wa malipo ya kamisheni ya ununuzi wa silaha, yaliyofanywa kati ya kampuni hiyo na Saudi Arabia, kwa sasa imeapa kufa na suala la Tanzania.

Juzi, kinara wa mchezo huu kwa upande wa Tanzania, Sailesh Vithlani, alimuongoza Short kutoa mwito wa kufunguliwa mashitaka kwa BAE, iwapo tuhuma hizo zitathibitishwa.

Alisema kwamba, Waziri Mkuu, Blair, binafsi amehusika kulazimisha kutolewa kwa kibali kilichowezesha kufanikisha mkataba huo wa silaha na Tanzania kupitia Baraza la Mawaziri.

“No 10 (makazi ya waziri Mkuu wa Uingereza) alisisitiza suala hili liendelee, wakati suala lenyewe linanuka,” alisema na kuongeza: “Ilikuwa wazi mradi huu usiofaa ulinuka rushwa.”

Mjini Dar es Salaam, mshirika wa kibiashara wa Vithlani, Tanil Somaiya, aliliambia Guardian kwamba, polisi wa Uingereza tayari walishawasili na kuwahoji wote wawili, wakitegemea kuwa miongoni mwa mashahidi wao.

Alisema, BAE iliweka michakato miwili ya malipo, ikimhusisha kinara huyo. Katika mchakato wa kwanza, makubaliano na wakala huyo yalisainiwa. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, asilimia moja ya kamisheni ilitakiwa kulipwa iwapo mkataba wa ununuzi wa rada hiyo yenye thamani ya dola milioni 40 ungepitishwa, kwenda kwa kampuni iliyosajiliwa Tanzania, Merlin International Ltd.

“Vithlani alikuwa na hisa nyingi katika kampuni hiyo,” Somaiya alisema, huku yeye mwenyewe akiwa na kiasi kidogo cha hisa. “BAE ililipa dola 400,000 katika mchakato huo,” Somaiya aliongeza.

Lakini chini ya mchakato wa pili, makubaliano zaidi yasiyo ya kawaida yalifanyika, BAE inatuhumiwa kumiliki kwa siri Kampuni ya Red Diamond iliyopitisha dola milioni 12 nyingine, zikiwakilisha asilimia 30 ya thamani ya mkataba wa mauzo ya rada hiyo nchini Uswisi.

“Fedha hizo zilikuwa chini ya udhibiti wa Vithlani,” Somaiya alisema na polisi wa Uingereza wamethibitisha suala hilo.

Wakati alipoulizwa kuhusu fedha za BAE, Vithlani aliiambia Guardian kwamba, hajazitoa fedha hizo kutoka kwa akaunti ya Uswisi kwenda kwa maofisa wa serikali nchini Tanzania.

Alipoulizwa iwapo alizigawa dola hizo milioni 12 kwa upande wa tatu, yaani nje ya Tanzania, alishindwa kueleza. “Wakati polisi wa Uingereza waliposafiri kwenda Tanzania, tulikutana nao baada ya kututaka tufanye hivyo na tulijibu maswali yao yote,” alisema.

Vithlani alihusika katika suala hili kama wakala, si tu katika kusainiwa kwa mkataba wa ununuzi wa rada hiyo, bali pia alihusika na ununuzi wa ndege ya kifahari iliyotengenezwa Marekani mwaka 2002 kwa ajili ya Rais wa Tanzania, iliyokuwa na thamani ya dola milioni 40.

Wakati alipoulizwa iwapo atawaruhusu polisi wa Uingereza wakague matumizi yake yote katika akaunti yake ya Uswisi, alishindwa kutoa maelezo.

Kwa kawaida, katika mikataba ya siri ya silaha ya kimataifa, kamisheni ya asilimia moja kwa mawakala wa ndani kwa kiasi kikubwa huonekana kuwa halali.

Mawakala wa serikali wa mikopo ya uuzaji nje na idara za mikopo kwa wauzaji wa nje, huwa na sheria ambayo kamisheni ya zaidi ya asilimia 5 hadi 10 huzua maswali mengi.

Ulipaji uliofanywa na BAE System, wa asilimia 30 kwenda kwenye akaunti ya Uswisi, umevuka mipaka ya kiwango kinachotakiwa, si ajabu kuzua shaka ya kuwapo kwa rushwa, wachunguzi wa suala hilo wamesema.

Vyanzo vya habari vya polisi nchini Tanzania, vilisema kwamba, makubaliano ya kumtumia Vithlani kama wakala, yalisainiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa BAE, Sir Dick Evans.

Sir Dick, ambaye amekuwa kinara wa matukio mengi ya mikataba ya silaha zenye utata zinazochunguzwa, tayari ameshafanyiwa mahojiano na SFO wakati wa uchunguzi wao wa miaka miwili.

BAE Systems ilipoulizwa juzi kwanini ilifanya malipo ya asilimia 30 kwenda akaunti ya Vithlani nchini Uswisi, ilikataa kujibu ikisema: “Hatuko tayari kueleza lolote. Suala hili lisichukuliwe kuwa kigezo cha kutulazimisha kutoa habari hii.”

SFO pia imekataa kujadili uchunguzi wao.

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, aliyeko hapa, anatarajia kukutana na Hilary Benn, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza katika juhudi za kupambana na tatizo la rushwa Tanzania.

Baadaye wiki hii, Uingereza inatarajia kutetea vitendo vya BAE kwenye mkutano wa kundi linalopambana na rushwa la OECD mjini Paris, Ufaransa.

Norman Lamb, wa Chama cha upinzani cha Liberal Democrat na mkosoaji mkubwa wa mkataba huo, alisema: “Ni wazi wakati huu mkataba huu ulikuwa ukinuka, lakini Blair aliulazimisha kupita kinyume cha uamuzi wa wenzake. Sidhani kama alikuwa hajatahadharishwa.”


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.