Na Mwandishi Maalum
MAKAMU wa Rais Dk. Ali Mohamed Sheni, anatarajia kuondoka nchini keshokutwa kwenda Djibouti kuhudhuria mkutano utakaowahusisha Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Mashariki ya Afrika kuhusu masuala ya nishati inayotokana na joto la ardhini barani Afrika.
Dk. Sheni atamwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika mkutano huo utakaofanyika kuanzia keshokutwa katika hoteli ya Djibouti Palace Kempinski nchini Djibouti .
Mkutano huo unatarajiwa kujadili kwa kina uwezo wa kuzalisha nishati hiyo ya joto la ardhini ambayo inapatikana katika bonde la ufa barani Afrika kwa ajili ya manufaa ya matumizi ya majumbani na viwandani na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi katika Afrika.
Dk. Sheni atakuwa miongoni mwa viongozi wa kitaifa watakaohutubia mkutano huo wakati wa ufunguzi. Viongozi wengine watakaoshirki na kuhutubia ni pamoja na Rais Mwai Kibaki wa Kenya , Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi.
Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na ile inayohusu fursa ya wafanyabiashara kuwekeza katika sekta ya nishati inayotokana na joto la ardhini.
Kauli mbiu ya mkutano huo ambao umeandaliwa na Serikali ya Djibouti kwa ushirikiano na Iceland na Mradi wa Milenia wa Umoja wa Mataifa ni kupata raslimali ya nishati iliyo safi na ya kipekee katika karne ya 21.
Mkutano huo utashirikisha wawekezaji wa kimataifa na wataalam wa masuala ya nishati ya joto la ardhini.
Katkia msafara huo, Dk. Sheni atafuatana na mkewe Mwanamwema Sheni, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Waziri wa Maji, Ardhi na Nishati katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mansour Yusuf Himid na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Seif Idd.
Dk. Sheni na ujumbe wake wanatarajiwa kurudi nchini Januari 19 mwaka huu.