Na Elizabeth Maoni, Sumbawanga
ZAIDI ya ekari 100 za mashamba ya wakulima 50 wa vijiji sita vya kata ya Mambwe kenya wilayani Sumbawanga vijijini zimesombwa na maji baada ya mvua kunyesha kwa zaidi ya saa tano katika kata hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na diwani wa kata hiyo, Edwin Msipi, wakazi wa vijiji sita wameathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha Januari 8, mwaka huu kwa zaidi ya saa tano na kuharibu mazao mashambani.
Msipi alitaja vijiji vilivyoathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua kuwa ni Kiundi Namema, Mambwe kenya, Mpanga, Kazozya, Mspazi na Madibila vyote vya Kata ya Mambwe Kenya.
Alisema kutokana na mvua kusomba ardhi ya mashamba, imewalazimu wakulima hao kuanza upya kilimo cha mazao ya maharage, mahindi, soya na ulezi huku wakiwa hawana uhakika kama mazao hayo yatastawi tena au yatasombwa na maji.
Aliwataka walioathirika na mafuriko kutokata tamaa na waendelee kupanda mazao hayo kwani msimu wa kilimo bado unaendelea na kuongeza kuwa wote wanaolima katika vyanzo vya maji waache mara moja.
Hata hivyo, alisema mvua hiyo haikutela madhara mengine zaidi ya kuharibu mashamba na mimea.