. Mmoja hadi kichwa chatengana na kiwiliwili
. Kiongozi ahoji wamenyongwa au wamechinjwa?
BAGHADAD, Irak
WASAIDIZI waandamizi wa aliyekuwa Rais wa Irak marehemu Saddam Hussein, wamenyongwa kama ilivyofanyika kwa kiongozi huyo wiki mbili zilizopita.
Wasaidizi hao, kaka wa kambo wa Saddam aitwaye Barzan al-Tikrit na Awad Hamad al-Bandar, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Mapinduzi ya Irak, walinyongwa jana saa tisa alfajiri.
Saddam Hussein alinyongwa alfajiri ya Desemba 30, mwaka jana kitendo kilichofuatiwa na shutuma kwamba watu waliokuwepo wakati wa utekelezaji wa adhabu hiyo walimkejeli na kumdhihaki.
Msemaji wa serikali ya Irak Ali al-Dabbagh, alisema kichwa cha Barzan kiliachana na kiwiliwili wakati akinyongwa, tukio alilolielezea kuwa ‘ni la nadra kutokea’ na ‘ni kazi ya Mungu’.
Lakini alisisitiza sheria na taratibu zote ziliheshimiwa na kuzingatiwa wakati wa unyongaji.
Msemaji huyo alikuwa makini alipokuwa akizungumza, hasa ikizingatiwa kuwa kunyongwa kwa Saddam kulifuatiwa na shutuma na lawama dhidi ya serikali ya Irak.
Mkanda wa video wa kunyongwa kwa Saddam, unaoaminika ulipigwa kwa kutumia kamera ya simu ya mkononi, unaonyesha namna walioshiriki kumnyonga walivyokuwa wakimtupia maneno ya kejeli, wakati akiwa katika mhilimili wa kunyongea.
“Wale waliohusika walisaini nyaraka zenye kuwataka kufuata taratibu, la sivyo wangekiuka wangekabiliwa na hatua za kisheria na kuadhibiwa. Watu wote waliokuwepo walitekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na hakukuwa na ukiukaji wa taratibu,” alisema msemaji huyo wa serikali.
“Hakuna aliyetoa maneno ya kejeli au kusema neno la dhihaka katika unyongaji. Hakuna aliyetiwa hatiani ambaye alitukanwa,” alifafanua.
Khalaf al-Olayan, ambaye ni kiongozi wa wabunge Wassuni, alitaka kuonyeshwa mkanda wa video wa kunyongwa watu hao wawili, lakini haikuweza kufahamika mara moja kama kulikuwa na mkanda rasmi wa tukio hilo.
Wakati Saddam akinyongwa zilipigwa picha rasmi za video zikionyesha namna adhabu hiyo ilivyotekelezwa.
“Haiwezekani mtu akinyongwa kichwa kikatike na kuachana na kiwiliwili,” kiongozi huyo wa wabunge alisema alipozungumza na kituo cha televisheni cha Al-Jazeera na kuongeza, “hii inaonyesha wamemchinja na huu ni ukiukwaji wa sheria”.
“Tunataka kuuona mkanda wa video ambao ulipigwa wakati wakinyongwa watu hao wawili ili tuweze kuamini maneno ya serikali kwamba kichwa kilikatika wakati akinyongwa,” alisema.
Familia za marehemu hao zilitarajia kuchukua miili ya jamaa zao jana kwa ajili ya kuzika. “Miili yao ipo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema ofisa mmoja wa serikali.
Watu hao walinyongwa katika makao makuu ya kijeshi ya usalama wa taifa wakati wa uongozi wa Saddam, kaskazini mwa jiji la Baghdad, mahali ambapo pia Saddam alinyongewa.
Watu hao walikuwa wanyongwe pamoja na Saddam Desemba 30, mwaka jana lakini serikali iliamua kumnyonga Saddam peke yake kwa kile kilichoelezwa na mshauri wa masuala ya usalama wa wa taifa Mowaffak al-Rubaie, kuwa alitakiwa kunyongwa ‘siku maalumu’.
Barzan alikuwa mkuu idara ya usalama na Awad alikuwa mkuu wa Mahakama ya Mapinduzi ya Irak; sambamba na Saddam walipatikana na hatia ya maujaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia 148, baada ya jaribio la kutaka kumuua Saddam mwaka 1982 kushindwa katika mji wa Dujail, kaskazini mwa Irak.
Kutolewa kwa hukumu ya kunyongwa dhidi yao, kulizua chuki miongoni mwa waumini wa madhehebu ya Kiislamu ya Sunni, huku Washia ambao wakati wa uongozi wa Saddam walinyanyasika mno, wakiifurahia.
Wiki iliyopita Rais wa Irak, Jalal Talabani alitoa wito kwa serikali kuchelewesha unyongwaji wa watu hao.
“Kwa maoni yangu, tusubiri,” alisema Talabani Jumatano iliyopita katika mkutano na waandishi wa habari akiwa amefuatana na Balozi wa Marekani nchini Irak, Zalmay Khalilzad.
“Tutathimini kwanza hali ilivyo,” alisema bila kufafanua.
Balozi Khalilzad aliiomba serikali ya Irak kuvuta subira ya kunyongwa watu hao kwa siku 10 hadi 14, lakini serikali ya Irak ilikataa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, pamoja na Kamishina wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Louise Arbour, nao waliwahi kutoa wito wa kuitaka serikali ya Irak isiwanyonge Barzan na Awad.