Na Mwandishi Wetu
BAADA ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa kusulubu uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushindwa kupeleka asilimia 70 ya wanafunzi waliofaulu darasa la saba, kuingia kidato cha kwanza, uongozi huo sasa umewageukia wazazi ukitaka kubeba msalaba huo.
Hatua hiyo ilionekana jana katika harambee ya uzinduzi wa ujenzi wa sekondari Kata ya Ilala, baada ya Katibu Tarafa, Omar Mwenda kudai kuwa, hawakubali tena kwenda kusulubiwa kwa ajili ya uvivu wa wananchi.
"Juzi tumesulubiwa kule kwa Waziri Mkuu kwa sababu ya mtoto wa Kitanzania...tutakapofika hatua tukaona hamchangi tutatumia nguvu, haiwezekani sisi watu wazima kuwa tunasulubiwa kwa ajili yenu," alisema Mwenda.
Kata ya Ilala ina shule za msingi tisa na mwaka huu, wanafunzi 903 walifanya mtihani kati yao, 850 walifaulu kuanzia alama 101, lakini ni 313 waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza.
Akizungumza na wananchi hao, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu alisema wanafunzi 537 waliokosa nafasi sekondari wakiachwa kuingia mitaani, kata hiyo itakuwa imezalisha jeshi kubwa la vibaka na wezi.
Zungu, alisema suala la mchango sio hiari kwa sababu sheria zipo na kuonyesha wasiwasi wa kiwango kilichowekwa kwa wafanyabiashara, huku akitaka kamati ya shule kuliangalia upya suala hilo.
"Wafanyabiasha pekee yao tunatarajia kupata Sh150 milioni na wananchi tutapata Sh51 milioni. Tukishapata hizi Tasaf (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii) watatupa Sh70 milioni zipo zinategemea tumechangia kiasi gani," alisema.
Mbunge huyo alisema wanatarajia kujenga sekondari ya ghorofa nne itakayogharimu Sh950 milioni na kwamba, wananchi wakichanga atatumia uwezo wake wa kutafuta marafiki nje na ndani kwa ajili ya kusaidiwa.
Wanafunzi 13,000 wa Wilaya ya Ilala walifanya mtihani wa darasa la saba mwaka jana kati yao, 9,400 walifaulu lakini ni 1,650 sawa na asilimia 18 ndio walichaguliwa kuingia kidato cha kwanza.
Zungu alisema kuna hatari ya fedha za halmashauri zilizotengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali katika kata hiyo, kutumika kwenye ujenzi wa shule kwa sababu hali ya kukosa sekondari haikubaliki.
Diwani wa Kata ya Ilala, Moshi Kondo, alisema mwaka juzi walipitisha uamuzi wa kujenga sekondari na kupanga kila nyumba kutoa Sh30,000 na wafanyabiashara Sh50,000, lakini walikwama baada ya wananchi kukataa.
Kata hiyo inakadiriwa kuwa na nyumba 1,740 zenye wakazi 32,799 kati yao, 7,000 ni watoto. Katika harambee hiyo zilipatikana Sh2.5 milioni.