Na Mwandishi Wetu
TAARIFA za mauaji ya vijana wawili yanayowahusisha polisi, zimefika hatua mpya baada ya familia za marehemu kuja juu na kutishia kwenda katika Taasisi za Kimataifa za Haki za Binadamu kuishitaki serikali ya Tanzania iwapo idara yake ya polisi itashindwa kuwafichua askari waliohusika na mauaji hayo ya kinyama.
Familia hizo za vijana waliokuwa maarufu jijini Dar es Salaam ni ya marehemu Hija Shaha Salehe aliyeuawa eneo la Kimara Temboni kwa tuhuma za kupora gari na mauaji na nyingine ya Mine Chomba, aliyedaiwa kuuawa na majambazi katika baa ya Meeda iliyopo Sinza.
Wakati familia hizo zikija juu huku vifo hivyo vikitawaliwa na utata, uchunguzi wa Mwananchi Jumapili, umebaini kwamba gari moja la marehemu Mine aina ya Toyota Rav 4 , linatumiwa na mmoja wa kigogo wa polisi nchini ambaye anadai amelinunua katika mnada.
Tayari familia ya Hija Shaha imekwisha peleka picha zinazoonyesha mauaji ya ndugu yao tangu akiwa katika gari ya polisi na kisha baadae kuelezwa ameuawa na raia katika taasisi za kutetea haki za binadamu zilizopo Marekani.
Kama haitoshi familia zote mbili, tayari zimekwishamwandikia barua Rais Jakaya Kikwete, zikieleza kutoridhishwa na taarifa za polisi kuhusu vifo hivyo.
Barua kwenda kwa Rais Kikwete kuhusiana na kifo cha Hija Shaha ni ya Februari 3, mwaka jana ambayo pia nakala yake ilikwenda kwa Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu.
Nakala nyingine ni kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mwanasheria Mkuu Kitengo cha Haki za Binadamu, Mwanasheria Mkuu na aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti mapema wiki hii kwa sharti la kutotajwa majina yao, wanafamilia hao, walisema wanaipa muda tume ya serikali ifanye uchunguzi wake kisha itoe majibu.
Familia hizo zimeliambia Mwananchi Jumapili kwamba, tangu ndugu zao wauawe hadi sasa hakuna taarifa za kina zinazoonyesha kuhusu vipi ndugu zao walikufa na nani wako nyuma ya mauaji hayo.
"Tutafuatilia suala hili hadi katika mahakama ya haki za binadamu ya kimataifa, hatuwezi kukubali kuona ndugu zetu wauawe kinyama namna hii, wamekosa nini, wana haki ya kuishi," alisema mmoja wana familia ya Hija Shaha na kuongeza, huku akionyesha picha za mauaji hayo ambayo ni ya kinyama.
"Tunachosubiri ni tume ifanye kazi yake kisha imalize, tusiporidhika na majibu tutakwenda katika ngazi hiyo ya kimataifa kuonyesha ulimwengu kuhusu unyama na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na polisi dhidi ya vijana wetu," alisisitiza.
Hata hivyo, wakati ikisubiriwa tume ya uchunguzi wa sakata hilo iliyoundwa na Katibu Mkuu Wizara ya Usalama wa Raia, Bakari Mahiza, uchunguzi zaidi wa Mwananchi Jumapili, umebaini kwamba upo uwezekano mkubwa kwamba hata Mine hakuuawa na majambazi kama jalada la uchunguzi wa polisi linavyoeleza.
Kikubwa kinachotatanisha na kutia shaka iwapo Mine kweli aliuawa na majambazi, ni hatua ya polisi mkoa wa Dar es Salaam kushikilia magari yake wakati yeye ndiye aliyeuawa majambazi badala ya kufanya uchunguzi kubaini watuhumiwa wa mauaji hayo.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini zaidi kwamba, baada ya kifo cha Mine hapo Januari 13, polisi walitoa taarifa kwamba kijana huyo aliuawa na majambazi, lakini cha kushangaza wakafika nyumbani kwa marehemu Mwenge na kuchukua magari mawili ambayo ni Suzuki Vitara na Toyota Rav 4 huku wakisema nyumba hiyo ni chimbo jingine la majambazi.
Mwananchi Jumapili imebaini kwamba, Suzuki Vitara kwa sasa ipo kituo cha polisi Oysterbay na gari Rav 4 ukiacha inayotumiwa na kigogo, ipo polisi urafiki ikiwa na tundu la risasi katika moja ya kioo cha mbele .
Uchunguzi huo wa Mwananchi Jumapili umebaini kwamba, uwezekano wa Mine kuuawa na polisi unatokana na msimamo wake wa kudai gari ya awali aina ya Rav 4 iliyozuiliwa na polisi tangu mwaka 2003 wakati akiwa na kesi ya wizi wa magari kabla mahakama haijatupilia mbali.
Awali kabla polisi kueleza Mine ameuawa na majambazi mwaka jana, aliwahi kukabiliwa na shitaka la wizi wa magari ambalo jalada lake namba -OB/ IR/504/03C21/03 lilikuwa polisi Oysterbay katika kipindi hicho cha mwaka 2003.
Mwananchi Jumapili imebaini kwamba, baada ya polisi kumkamata Mine mwaka 2003 kwa kosa la uporaji, ilishikilia magari yake matatu ikiwemo hiyo Toyota hiyo Rav 4 inayotumiwa na kigogo, ambayo pamoja na magari mengine mawili ilipaswa kurejeshwa kwa amri ya mahakama baada ya kukosekana ushahidi.
Baada ya amri hiyo ya mahakama, polisi ilirejesha magari mawili tu ndipo ikazuia Rav 4 hiyo ndipo Mine alipoanza kufuatilia mali yake hiyo hadi alipofariki mwaka jana katika kifo hicho chenye utata kwa madai ya kuawa na majambazi lakini polisi kwa mara nyingine ikashikilia magari mawili zaidi.
Hata hivyo, jalada la uchunguzi la polisi lililopo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) linamtaja Mine kama aliyeuawa na Hija Shaha ambaye hakuwemo katika orodha ya watu wanaotafutwa na polisi kwa tuhuma za mauaji.
Awali alikamatwa Lucas Mfinanga kwa tuhuma za kumuua Mine kisha akaachiwa huru baada ya kubainika hakuhusika na baada ya kifo cha Hija hapo Januari 16, alikamatwa mtu mwingine anayefahamika kama Donat Shirima anayedaiwa kushikiliwa hadi sasa.
Hija Shaha ambaye alikuwa akisoma masomo ya Uhandisi umeme nchini Marekani alirejeshwa nchini mwaka 2001 kwa ombi la Jeshi la polisi nchini akidaiwa kuhusika na wizi lakini hadi anauawa kwa tuhuma hizo za kosa la kumuua Mine, hakukuwa na ushahidi kuhusu kesi hiyo ya wizi.
Mwananchi Jumapili itaendelea kuwaletea mtiririko wa sakata hili kadri itakavyopata taarifa zaidi hadi hapo tume ya Mahiza itakapomaliza kazi na kutoa majibu.