Ikiwa ni siku tano tu tangu kutokea kwa ajali mbaya ya basi iliyoua watu 54 kutokana na kujaza abiria kuliko uwezo wake mkoani Arusha, basi la Najimunisa limekamatwa eneo la Kongowe, wilayani Kibaha likiwa limefurika abiria 145.
Uwezo wa basi hilo lenye namba za usajili T 776 ACK aina ya Scania lililokuwa likitoka Jijini Dar es Salaam kwenda Mwanza, ni abiria 65.
Basi hilo lilikamatwa jana eneo la Kongowe, nje kidogo ya mji wa Kibaha likiwa limebeba abiria hao 145.
Hata hivyo, abiria wengine walipakiwa katika mabasi mengine mawili aina ya Coaster baada ya kuwasili mjini Kibaha na kwenda kupakiwa katika basi la Namjimunisa baada ya kufika Kongowe ikiwa kama njia ya kuwakwepa askari wa Usalama Barabarani.
Kukamatwa kwa basi hilo kulitokana na mmoja wa abiria baada ya kuibuka ugomvi wa kugombea kiti.
Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Pwani, Bw Ephaim Mrema, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kamanda Mrema alisema baada ya basi hilo kupimwa uzito katika eneo la mizani Kibaha, liliendelea na safari yake na lilipofika eneo la Kongowe, lilisimama na kuongezwa abiria wengine 80 kutoka katika mabasi mawili madogo aina ya Coaster.
Hata hivyo, mabasi hayo madogo aina ya Coaster hayakukamatwa baada ya kuteremsha abiria hao.
Lakini alisema baada ya abiria hao 80 waliokuwa ndani ya mabasi hayo madogo mawili kupakizwa ndani ya basi kubwa, ulizuka ugomvi wa kugombea viti ambapo kiti kimoja kiligombewa na zaidi ya abiria watatu wenye tiketi.
Hali hiyo ilisababisha mmoja wa abiria hao, kupiga simu polisi kuwaarifu juu ya tukio hilo.