Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Reginald Mengi, amesema wana imani na Rais Jakaya Kikwete kwamba muswada wa marekebisho ya sheria ya vyombo vya habari unaoandaliwa kupelekwa bungeni utasitishwa.
Mengi alisema imani yao inatokana na Rais Kikwete kuwa mtu mwenye kupenda uhuru wa kujieleza na kuongeza kuwa wamiliki na wadau wa sekta ya habari wanajitahidi kusimamisha muswada huo.
Akizungumza na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Yale, Marekani jana, Mengi alisema hivi sasa uhuru wa vyombo vya habari sio mbaya, ila muswada unaondaliwa kupelekwa bungeni utarudisha nyuma uhuru wa kujieleza.
"Mpaka sasa hali ni nzuri, lakini iwapo muswada wa sheria unaoandaliwa utapelekwa bungeni kitakuwa kitanzi kwa vyombo vya habari. Tunajitahidi kusimamisha muswada huo, tutafanikiwa kwa sababu rais wetu anaamini katika uhuru wa kujieleza," alisema Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat).
Mengi alikuwa akijibu swali la mmoja wa wanafunzi hao, aliyetaka kujua jinsi uhuru wa habari ulivyo nchini. Alisema iwapo utapitishwa, ni vigumu kupigana na rushwa na unawanyima wananchi kujua serikali yao inachofanya.
Kuhusu mtazamo wa Watanzania dhidi ya Wamarekani, Mengi alisema Wamarekani na nchi nyingi zilizoendelea zimekuwa zikitangaza masuala yanayotoa taswira mbaya kwa Afrika.
Alisema masuala mazuri ya Afrika hayatangazwi kwenye nchi hizo na kwamba, Watanzania au Waafrika hawawezi kupendezwa na tabia hiyo.
Akizungumzia biashara, Mengi alisema wananchi hawatakiwi kukata tamaa bali kuona matatizo kama changamoto kwao na kuongeza kuwa, hofu ni adui mkubwa wa mafanikio.