Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  CUF wasema Karume bora kuliko Salmin
CUF wasema Karume bora kuliko Salmin
By Habari Tanzania | Published  01/13/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Simon Berege, Pemba

WAKATI wananchi wa Zanzibar jana walisherehekea miaka 43 ya Mapinduzi, baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wameusifia uongozi wa Rais Aman Abeid Karume kwamba umepunguza machungu ya kisiasa kuliko ilivyokuwa wakati wa rais aliyemtangulia, Dk Salmin Amour.

Hata hivyo wamesema utawala wa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, ambaye wakati huo Waziri Kiongozi alikuwa Maalim Seif Sharif Hamad, ndiyo ulikuwa bora kuliko awamu zote.

Mwinyi pia ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Maalim Seif sasa ni Katibu Mkuu wa CUF.

“Mimi binafsi wakati wa Salmin nilifungwa mara tatu, lakini tangu Karume aingie madarakani sijawahi hata kuwekwa ndani,” alisema Omar Masoud Hamad ambaye ni mratibu wa CUF mkoa wa Kusini Pemba.Alisema ingawa katika siku zake za mwanzo Karume alionekana kutaka kuiga siasa za Salmin, alijibadilisha haraka huku mwafaka wa 2001 ukimbana kuweka mazingira mazuri zaidi ya kisiasa.

Hata hivyo, Hamad ambaye pia ni katibu wa CUF wilaya ya Chakechake, alisema kwamba mbali na kuwapo kwa mazingira yenye ahueni kisiasa, lakini hali ya uchumi wakati wa Salmin na Karume haina tofauti kwani maisha bado ni magumu.

Kiongozi huyo alieleza kwamba dosari kubwa iliyopo katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ya sasa ni kukataa kuwashirikisha wapinzani katika shughuli za maendeleo.

“Inashangaza kunapokuwa na shughuli za Serikali ya Jamhuri tunashirikishwa, lakini zile za SMZ hawatutaki,” alilalamika kiongozi huyo na kuongeza kwamba hali hiyo imekuwa ikiwafanya wanachama wao kuanza kusumbua kutaka kujua lini itakuwa hatima ya ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kushughulikia mpasuko wa kisiasa visiwani huko.

“Wananchi walifurahia sana kumsikia Rais Kikwete akisema kwamba yuko tayari kushughulikia mpasuko lakini sasa wameanza kuchoka maana wanaona hakuna wanaloambiwa,” alisema.

Alisema SMZ bado imewatenga wananchi wake katika madaraja manne ambapo daraja la kwanza ni la Waunguja waliyo wana-CCM, wakifuatiwa kwa ubora na wana-CUF waliyo Unguja na la tatu ni la wana-CCM waliyo Pemba na daraja la nne ni Wana-CUF waliyo Pemba.

Naye Mwakilishi wa jimbo la Micheweni linaloaminika kuwa ngome kubwa ya CUF Kaskazini Pemba, Subeti Khamisi Faki, alisema pamoja na nia nzuri ya Mapinduzi, bado hayaenziwi kwani viongozi wa serikali wamekuwa wakiwatenga wananchi waliyo katika upinzani.

“Hata kwenye shughuli za kuandaa sherehe za Mapinduzi hawataki kutushirikisha.... labda waseme kwamba hawataki vyama vingi,” alieleza mwakilishi huyo alipofanya mazungumzo na Mwananchi jimboni humo hivi karibuni.

Kuanzia Januari mosi mwaka huu kumekuwa na pilikapilika nyingi za uzinduzi wa miradi ya maendeleo iliyofanywa na viongozi mbalimbali wa SMZ, lakini viongozi wa CUF wamekuwa hawahudhurii.

Akihutubia wananchi wakati wa uzinduzi wa kituo cha afya cha Wesha hivi karibuni, Rais Karume aliwabeza watu aliyowaita wapinga maendeleo ya Zanzibar kwamba hawawezi kufanikiwa kwani serikali imejizatiti kuzindua miradi mingi visiwani humo.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake Mkuu wa wilaya ya Micheweni, Juma Abdallah Ali, alikanusha madai ya kutengwa kwa viongozi wa vyama vya upinzani kwenye shughuli za maendeleo, isipokuwa wapo baadhi ambao ni wakaidi na wengine watiifu.

“Wilaya yangu ina kata kumi na zote zinaongozwa na CUF, lakini madiwani wote wamekuwa wakishirikiana nasi vizuri na kwa miaka miwili wamekuwa wakishiriki maandalizi ya mwenge na kuupokea,” alieleza Mkuu huyo wa wilaya.

Hata hivyo alisema kwamba tatizo kubwa liko kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wabunge isipokuwa mbunge wa Jimbo la Konde, Ali Mohamed Suleiman na mwakilishi wa jimbo hilo Ali Taarab, ambao wamekuwa wakijituma sana kwenye shughuli za maendeleo.

“Kama tunaleta mradi wa afya, maji ama shule wananchi wote wanapata huduma hizo bila kuangalia anatoka chama gani... kimsingi tunaposema wananchi asilimia kubwa ni CUF kwani ndiyo idadi kubwa ya wakazi wa huku,” alieleza.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Micheweni, Omar Masoud Hamad, alisema CCM inatekeleza ilani yake ya uchaguzi bila kubagua mtu na si kweli kwamba imekuwa ikibagua wananchi.

Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini siasa za Zanzibar zimekuwa tete kutokana na mvutano wa kisiasa baina ya CCM na CUF vyenye ushawishi mkubwa visiwani humo.

Mivutano na vurugu zilizofuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 na ule wa mwaka 2000, ulisababisha kuwako kwa mazungumzo baina yao ambayo yalizaa mwafaka wa 1999 na ule wa 2001.

Kwa kiwango kikubwa mwafaka wa 2001 ulipunguza jazba ya kisiasa visiwani huko, na hali ya kutokuaminiana na uhasama wa kisiasa imeendelea hali iliyomfanya Rais Kikwete kutangaza kwamba Zanzibar kuna mpasuko na kuahidi kuutafutia ufumbuzi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.