MKUU wa Mkoa wa Kagera, Kanali Enos Mfuru, amekiri kupokea taarifa zinazoonyesha ukiukwaji mkubwa wa maadili, unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watumishi wa hospitali ya mkoa, wa kufanya ngono kwenye chumba cha matibabu.
Akizungumza katika kikao cha wafanyakazi wa hospitali hiyo, Mfuru alisema, alipokea barua mwezi Mei mwaka jana, inayodai kuwa, baadhi ya wafanyakazi hospitalini hapo, wanakiuka maadili na wamebobea katika suala la kuomba rushwa.
Zaidi ya hayo, alisema kuwa, mwandishi wa barua hiyo, ambaye hakumtaja jina, alidai kuwa chumba cha kuhudumia wagonjwa wa macho, kimegeuzwa cha kutolea mimba na kufanyia ngono.
Kanali Mfuru alisema kuwa, baadhi ya wafanyakazi wa hospitalini hapo na wananchi, wamekuwa wakimpelekea malalamiko mbalimbali kuhusu kubobea kwa vitendo vya ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi yao, akiwamo Muuguzi Mkuu wa Mkoa (patron), ambaye pia ni mganga wa macho, Dk. Abdallah Mbaraka.
Alisema baada ya kupokea barua hiyo, alikaa na kamati yake ya mkoa na kuanza kuyafanyia kazi madai hayo, na kubaini kuwa, kulikuwa na ukweli katika mengi ya madai hayo.
Barua hiyo ilisomwa mbele ya wafanyakazi hao na kubainisha kuwapo kwa wafanyakazi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, lugha chafu kwa wagonjwa na wafanyakazi wenzao, uongozi wa hospitali kutotoa taarifa za kila mara kwa wafanyakazi hao, kuuzwa kwa chanjo ya mbwa na udokozi wa dawa.
Alisema, uchunguzi uliofanywa umeonyesha kuwa, tuhuma zinazomkabili Dk. Mbaraka ni za kweli.
Aliwataja wafanyakazi wengine wenye tuhuma nyingine kuwa, ni Dk. Byera Shwekerela na Dk. Batholomeo Katole, ambaye yuko katika kitengo cha dawa za kurefusha maisha.
Alisema wafanyakazi hao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba rushwa.
Mfuru alisema, wafanyakazi wengine wanaotuhumiwa ni wale wanaofanya kazi katika duka la dawa la hospitali hiyo, ambao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya udokozi wa dawa pamoja na walinzi, ambao wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa na ndugu zao.
“Mimi mwenyewe nimeishashuhudia wananchi wakinyanyaswa na walinzi, nilikuwa ndani ya hospitali, tukafukuzwa kutoka wodini kwa madai kuwa muda wa kuwaona wagonjwa umekwisha.
“Tukafika getini, tukafungiwa ndani na mlinzi, baadaye akatufungulia geti la kati na kwenda kufunga tena… tumekaa getini wee mpaka alipoamua kutufungulia, nikamuuliza, kwa nini unawanyanyasa wananchi hivyo? Akajibu samahani mkuu… kweli hiyo ni haki? Je, mimi nimefanyiwa hayo, mwananchi wa kawaida itakuwaje?” alihoji Mfuru.
Alisema kuwa, ipo pia tuhuma ya wananchi kuuziwa chanjo ya mbwa kuanzia sh 20,000 na kuendelea wakati inapaswa kutolewa bure.
Mfuru alisema kuwa, sasa wakati umefika wa kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na kuwashauri baadhi ya wafanyakazi wanaojihusisha na vitendo hivyo kubadilika mara moja.
Katika kile kinachoonekana kuwa yaliyosemwa na mkuu huyo wa mkoa ni kweli, alipowataka wafanyakazi hao wajitetee, hakuna aliyejitokeza kujibu.
Mmoja wa wafanyakazi hao, Anthony Lugemalila, alisema kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi, ambao wamekuwa sugu, hawataki kubadilika, kwa kuwa vimekuwa vikifanywa vikao vingi chini ya katibu tawala wa mkoa na kuwataka wajirekebishe, lakini imeshindikana.