NAIBU Katibu Mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, amesema hababaishwi wala kutishwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kupinga na kukashifu uteuzi wake.
Akizungumza na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) jana, Dk. Migiro alisema kuwa, akili yake yote sasa inafikiria jinsi atakavyotekeleza majukumu yake, hasa kuzisaidia nchi zinazoendelea kufanikisha malengo yao kupitia Umoja wa Mataifa.
“Wanaosema waache waseme… nimewasikia, lakini hilo si jambo linalonisumbua hivi sasa… zipo kazi na majukumu makubwa yaliyopo mbele yetu, na hayo ndiyo ninayoyafikiria,” alisema.
Dk. Migiro alisema, ni azma yake kuona kuwa nchi za dunia ya tatu zinapata nafasi yake inayostahili katika Umoja wa Mataifa, na mkazo katika kufanikisha hilo utawekwa katika kuhakikisha kuwa, mapendekezo ya kuimarisha umoja huo yaliyotolewa, yanatekelezwa.
“Umoja wa Mataifa una wanachama wengi, si vema kuuacha ukawa ni sehemu ya nchi moja kusema na kutekeleza inachokitaka, tutajitahidi kuhakikisha kuwa, kila mwanachama anapata kile anachokitaka kupitia umoja huu,” alisema baada ya kuulizwa atafanya nini kukomesha dhana kuwa, Marekani imeutawala umoja huo.
Aidha, Dk. Migiro alibainisha kuwa, anaondoka nchini kwa huzuni kwani, kuna vitu vingi amevizoea, ambavyo atakuwa anavikosa katika makazi yake mapya.
Alibainisha kuwa, wapo ndugu, jamaa na marafiki ambao atapoteana nao kwa kipindi kirefu, hali kadhalika mambo kadhaa ambayo alizoea kuyafanya akiwa hapa nchini.
“Lakini kinachonitia moyo ni ile dhamira ya kuisaidia nchi yangu na bara langu. Nimetumwa na nchi yangu, nimetumwa na Afrika na azma ya kutekeleza kazi hii ndiyo inayonitia moyo,” alisema.
Wakati huohuo, mmoja wa mawaziri waandamizi katika Serikali ya Awamu ya Nne, Zakia Meghji, ameungana na Dk. Migiro na kusema, wanaobeza uteuzi wake hawana hoja za msingi.
“Sina wasiwasi na uteuzi wake, naamini atafunga midomo ya wanaomponda kwa kuchapa kazi bila ubaguzi,” alisema Waziri Meghji.
Alisema wanaoponda uteuzi huo, ni dhahiri hawautakii mema Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wake, Ban Ki- moon, ambaye ndiye alijiridhisha na sifa na hatimaye akamteua Dk. Migiro kushika wadhifa huo.
“Ifike mahala binadamu kote duniani tupendane na tuheshimu uamuzi wa Ban Ki-moon kwa kumteua Dk. Migiro kwa kuwa kila mtu ana haki ya kuwa kiongozi bila kujali rangi wala taifa alilotoka.
“Na hata wakimponda, haisaidii kwa kuwa tayari ameishateuliwa, na kinachotakiwa sasa mteule huyo apewe ushirikiano wa kutosha ili aweze kuchapa kazi kwa maslahi ya UN na si kumponda,” aliongeza.
Hata hivyo alisema, anaamini kuwa watu wanaopinga uteuzi huo, hawakufikiria kuwa mtu kutoka katika taifa maskini kama Tanzania, anaweza kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Alisema, hiyo ni dhana potofu na umefika wakati sasa watu waache kudharauliana, na pia waondokane na kasumba za kudharau watu wanaotoka kwenye nchi maskini.
Meghji alisema, yeye binafsi anamfahamu vilivyo Dk. Migiro kabla hajawa waziri, alisema mteule huyo ni msomi mzuri, mchapa kazi na anayependa kujifunza na kujituma kila kukicha, na asiyependa kujikweza.
Aidha, alisema changamoto zitakazomkabili ni juu ya hali ya amani na utulivu kwa nchi za Afrika na nguvu za mataifa makubwa, ambako anaamini kwa uwezo wa Dk. Migiro, hayo yanaweza kufanyiwa kazi na kuleta mabadiliko kwa nchi husika