Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete awateua mawaziri wapya
Kikwete awateua mawaziri wapya
By Habari Tanzania | Published  01/12/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Hellen Ngoromera

HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete ametangaza rasmi mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kuziba nafasi mbili zilizo wazi.

Katika mabadiliko hayo, Kikwete amemteua Bernard Membe, kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akichukua nafasi ya Dk. Asha-Rose Migiro, aliyeteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo.

Kuteuliwa kwa Membe kushika wadhifa huo, kumehitimisha minong’ono iliyosambaa kwa siku kadhaa sasa, ambayo kwa kiwango kikubwa ilikuwa ikimtaja mwanasiasa huyo ambaye ana shahada ya uzamili katika masuala ya uhusiano wa kimataifa, aliyosomea katika chuo maarufu nchini Marekani cha John Hopkins kilichoko Washington DC.

Hii inakuwa ni mara ya pili kwa Membe kuguswa katika mabadiliko ya mawaziri, kwani Oktoba 15, mwaka jana, wakati alipofanya mabadiko madogo ya kwanza ya mawaziri, alimwamisha kutoka kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na akampeleka Nishati na Madini.

Sambamba na uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua Dk. Batilda Salha Burian, kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu). Kama ilivyokuwa kwa Membe, hii inakuwa ni mara ya pili kwa Burian kuguswa na mabadiliko.

Dk. Burian ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Juma Akukweti ambaye alifariki dunia nchini Afrika Kusini alipokuwa akipata matibabu ya ajali ya ndege iliyotokea mjini Mbeya.

Katika uteuzi huo, kwa mara ya kwanza, Kikwete amelazimika kuwateua wabunge wawili kuwa naibu mawaziri, mmoja akichukua nafasi ya Membe na mwingine ya Burian.

Wabunge waliopanda ni pamoja na mwanasheria kijana na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, ambaye anakuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Gaudence Kayombo, ambaye ni Mbunge wa Mbinga Mashariki, anayekuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya uteuzi huo, iliyotolewa na Ikulu jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, mawaziri na naibu mawaziri hao wataapishwa leo saa 10.00 jioni.

Gazeti hili katika toleo lake la jana, liliandika kuhusu Rais Kikwete kukamilisha uteuzi wa mawaziri wapya, na kwamba tayari alikuwa ameshawasiliana nao.

Katika habari hiyo ya jana, kama ilivyokuwa ile iliyotoka katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Membe alitajwa kwa uhakika kabisa kuwa angepandishwa na kuwa waziri kamili, akichukua moja ya nafasi mbili za uwaziri, ile ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa au kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora).

Aidha, gazeti hili lilisema bayana kwamba, katika uteuzi huo, Kikwete atalazimika kumteua mbunge mmoja kutoka mkoani Ruvuma au mikoa ya Kusini kuwa waziri (kama alivyofanya kwa Kayombo), akichukua nafasi ya Akukweti, ambaye alikuwa akitokea wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Amina Mrisho Saidi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mjini.

Oktoba 15 mwaka jana, alipofanya mabadiliko ya kwanza, Kikwete aliwahamisha vituo vya kazi mawaziri 10 na naibu mawaziri wanane.

Katika mabadiliko hayo, wizara zilizoguswa zilikuwa ni Nishati na Madini; Mambo ya Ndani ya Nchi; Viwanda na Biashara; Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Kilimo; Chakula na Ushirika; Maliasili na Utalii; Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Miundombinu; Maendeleo ya Mifugo na Maji; Habari, Michezo na Utamaduni; Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.

Mawaziri waliohusika katika mabadiliko hayo, Oktoba mwaka jana, na wizara zao za zamani kwenye mabano, ni Anthony Diallo (Maliasili na Utalii), ambaye alihamishiwa katika Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Profesa Jumanne Maghembe (Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana) akapelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Wengine, ni Dk Ibrahim Msabaha (Nishati na Madini) aliyehamia Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Nazir Karamagi (Viwanda na Biashara) akaenda Wizara ya Nishati na Madini, Basil Mramba (Miundombinu) aliyehamishiwa Viwanda na Biashara na Kapteni John Chiligati (Mambo ya Ndani) aliyehamishiwa katika Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana.

Mawaziri wengine, ni Andrew Chenge (Ushirikiano Afrika Mashariki) aliyehamishiwa Wizara ya Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa (Maendeleo ya Mifugo) aliyehamishiwa Wizara ya Maji, Stephen Wassira (Maji) aliyehamishiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Joseph Mungai (Kilimo, Chakula na Ushirika) aliyehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Naibu mawaziri waliohamishwa wizara zao na kupelekwa wizara nyingine, ni Dk. Emmanuel Nchimbi (Habari, Michezo na Utamaduni) aliyekwenda Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Daniel Nsanzugwanko (Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana) aliyehamia Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni, David Mathayo (Biashara na Viwanda) akapelekwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Hezekiah Chibulunje (Kilimo, Chakula na Ushirika) aliyehamia Wizara ya Viwanda na Biashara.

Wengine walioguswa wakati huo ni Burian (Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), ambaye sasa kapanda cheo, aliyekwenda katika Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Salome Mbatia (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji) aliyehamia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Lawrence Masha (Nishati na Madini) aliyekwenda Wizara ya Mambo ya Ndani na Membe (Mambo ya Ndani) aliyekwenda Wizara ya Nishati na Madini.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.